‘Hii ilikuwa aibu kubwa sana’

Tukiwa tungali katika kumbukizi ya “Miaka 20 bila Nyerere”, tumekuwa tukikumbushwa mambo mengi juu ya Mwalimu. Gazeti moja limekuwa linatoa historia ya Mwalimu Nyerere katika nafasi mbalimbali. Gazeti moja limetoa kisa kile walichokiita “Nyerere apata msukosuko”. Ni msukosuko gani huo? Ni yale maasi ya jeshi yaliyotokea Januari 20, 1964.

Tukio lile ni kubwa na ni la kihistoria katika nchi yetu. Na Mwalimu Nyerere hakulisahau kamwe. Yeye aliliita tukio lile kuwa lilikuwa ni la “aibu kubwa sana”. Aibu kwa nani? Aibu ile ilikuwa kwa Taifa zima, na yeye aliona kana kwamba lilikuwa ni aibu kubwa sana kwake yeye binafsi kama kiongozi mkuu wa nchi yetu.

Wapo wananchi huko nyuma wamejitokeza kuandika juu ya tukio lile la maasi ya jeshi. Mzee Bwimbo alikuwa mlinzi mkuu wa Mwalimu wakati ule, katika kitabu chake uk. 89 ameuliza swali namna hii; “Yalikuwa maasi au mipango ya mapinduzi iliyoshindwa?” Kisha akaeleza kwa ufasaha wanavyosema watu wengine kuhusu tukio lile.

Aidha, nilipata kusoma kwenye gazeti miaka kadhaa iliyopita maelezo yaliyotolewa na Bwana Eugine Maganga namna kesi juu ya washitakiwa 15 waliohusika na maasi yale na kuhukumiwa vifungo vya miaka mbalimbali na hukumu ya muda mrefu zaidi ilikuwa ni miaka 15 jela.

Si hivyo tu, tulikuja kusoma tena katika gazeti Novemba 10, 2011, tulielezwa na mwandishi maarufu Bwana Joseph Mihangwa katika makala zake zenye kichwa cha habari; “Nani alichochea jeshi kuasi mwaka 1964?”

Neno hili ‘maasi’ siyo zuri kulisikia na Mwalimu kwa aibu ya tukio lile aliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liandike historia ya maasi yale watu wajue. Agizo lile lilitolewaje na lilitolewa lini na matokeo ni yapi? Basi, tunapomkumbuka Mwalimu, katika mwaka huu wa 20 tangu atutoke ninaona ni vizuri tukaona maagizo yake kwa Jeshi. Mwalimu alikuwa ‘very serious’ alipotamka maneno haya; “Hii ilikuwa aibu kubwa sana.” Mwalimu aliendelea kusema“…Lakini mpaka leo ni vigumu kujua chanzo hasa cha maasi haya ya mwaka 1964…

Hivyo, leo ninaonelea nimnukuu Mwalimu Nyerere kwa kinagaubaga kile alichowaeleza wanajeshi siku alipokuja kuwaaga kabla ya kung’atuka kwake hapo Novemba, 1985 na kumwachia Amiri Jeshi Mkuu Mzee, Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili.

Kikao cha Chama ndani ya Jeshi

Agosti 2, 1985 Mwalimu Nyerere akiwa Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa alifika katika Ukumbi wa Msasani Beach Club kufungua Mkutano Mkuu wa CCM, ndani ya Jeshi. Mkutano ule ulifanyika kwa siku mbili, yaani Agosti 2-3, 1985. Miongoni mwa nia zake za kuja kuzungumza na wanajeshi wale ilikuwa kuwaarifu rasmi kuwa yeye alikuwa anang’atuka mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 1985. Kwa kuwa alishapanga kuwaaga wanachama wa CCM mikoa yote na ule ulikuwa mkoa mmojawapo ulioitwa ‘Mkoa wa Majeshi’, alichukua fursa ile kuzungumza nao kwa kirefu historia yake na mpaka akafikiria lile tukio la maasi ya Jeshi la King African Rifles (KAR) ambalo aliliita lilikuwa la aibu kubwa sana kwake.

Mwalimu alianza hivi, namnukuu; “…Mimi nimekuwa miongoni mwa viongozi wachache sana wenye bahati kubwa kabisa ya kuaminiwa moja kwa moja na wananchi wangu…Nasema tangu kabla ya kujitawala mpaka tumejitawala, wananchi wa Tanzania kwa kweli wamenipa heshima ya ajabu sana, kubwa kweli, na hiyo ni bahati kubwa kweli kweli…”

Mwalimu Nyerere siku ile aliamua kuwa muwazi wakati wa kuongea na wanachama wake katika mkoa ule maalumu wa majeshi. Basi, aliendelea kusema haya; “…Halafu, kama nilivyosema Zanzibar, katika kipindi chote hicho, wananchi wenzangu wameniheshimu sana, watu wazima na vijana  na hakuna hata mara moja ametokea mtu na kusema kuwa anataka anitoe hapa nilipo, na yeye ashike nafasi yangu. Hata mmoja, kama alikuwepo labda alizungumza na mkewe tu wala haikutoka nje kwamba anataka anitoe hapo nilipo yeye ashike, hata mara moja (makofi).