Uislamu ni mfumo kamili wa maisha yote ya mwanaadamu uliopangika kimwili na kiroho. Mafunzo ya Uislamu yanamfikisha mwanaadamu katika kuyajua yatakayomfaa hapa duniani na kesho akhera. Uislamu umeyaharamisha kwa nguvu kubwa yale yenye kuleta madhara ya kiroho na kimwili kwa mwanadamu mmoja mmoja na kwa jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa yaliyoharamishwa na Uislamu kutokana na madhara yake makubwa kwa jamii ni rushwa.
Pamoja na uwepo wa maelezo anuai ya wanazuoni wa Kiislamu juu ya maana ya rushwa, tunaweza kuhitimisha kuwa kwa mujibu wa Uislamu, rushwa ni: ‘Kutoa chochote chenye thamani, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, kwa lengo la kuifanya batili kuwa haki au haki kuwa batili kwa manufaa ya mtoa rushwa au pia mwenye haki kulazimishwa kuinunua haki yake.’ Inaposemwa chochote chenye thamani ina maana ya mali, hadhi, nafasi na hata manufaa mengine yoyote.
Hapana shaka yoyote kuwa rushwa ni jambo lenye madhara kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii. Uislamu umeipiga vita na kutangaza uharamu wake. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 Aya ya 188 kuwa: “Wala msiliane mali zenu kwa batili (kinyume cha haki) na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.”
Pia Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) amenukuliwa akisema: “Laana ya Mwenyeezi Mungu imethibiti kwa mtoa rushwa na mpokea rushwa.”
Katika upokezi utokanao na Swahaba Ibnu Umar (Allaah Amridhie yeye na baba yake) Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Mtoa rushwa na mpokea rushwa (makazi yao) ni motoni.”
Imenukuliwa pia kuwa: “Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) amemlaani mtoa rushwa, mpokea rushwa na dalali wa rushwa”.
Rushwa ina madhara makubwa sana kwa jamii ikiwemo haki kununuliwa na ufisadi kuenea. Rushwa inapotamalaki katika jamii huziharibu akili za wanajamii kiasi cha kila mmoja kuwa tayari kutoa chochote chenye thamani katika jicho la mpokea rushwa ili afikie masilahi yasiyo haki yake au kuzuia sheria isichukue mkondo wake dhidi yake. Rushwa huchochea kuenea dhuluma katika jamii kiasi cha kuwazuia watu kupata haki zao na kuwapa haki wasiostahiki na kustahili.
Hebu tuangazie mifano michache ya madhara ya rushwa kwa jamii:
(1) Rushwa hujenga mazingira ya kukubaliana kati ya mkandarasi na msimamizi wa kuhakiki ubora katika mradi wa ujenzi wa barabara na madaraja na hatimaye barabara isiyo na kiwango na ubora stahiki huharibika baada ya muda mfupi.
(2) Hali hiyo huitia Serikali hasara na jamii huathirika pale zinapotumika fedha kuikarabati barabara iliyoathiriwa kwa rushwa badala ya fedha hizo kutatua kero nyingine za jamii. Pia barabara na madaraja yaliyojengwa chini ya viwango na ubora stahiki husababisha ajali barabarani na kupoteza roho za wanajamii na kuwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.
(2) Rushwa humfanya asiye na ujuzi stahiki kutangazwa kumaliza kwake masomo na kutunukiwa vyeti asivyostahili na hatimaye kushindwa kutekeleza wajibu wake na kuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii na ustawi wake. Achilia mbali mtaalamu huyo ‘bandia’ kuaminiwa katika majukumu asiyoyaweza na akafanya uamuzi wenye madhara kwa jamii na taifa kwa ujumla.
(3) Rushwa inaweza kuipa jamii kiongozi anayeamini katika kulinda madaraka yake kupitia rushwa, hivyo akawa muda mrefu akiwa madarakani anashughulika kujilimbikizia mali kama nyenzo ya kununua uongozi kutoka kwa wanajamii wasiofahamu thamani na nguvu ya kura zao.
(4) Rushwa inapotamalaki katika vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki huleta migogoro isiyoisha katika jamii na kutikisa misimgi ya Amani, Utulivu na Utangamano. Jamii inapopoteza imani kwa vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji wa haki matokeo yake ni wanajamii kujichukulia sheria mikononi; tabia yenye kubeba dhuluma na madhara makubwa kwa jamii.
Ipi njia bora ya kutokomeza rushwa katika jamii? Inapozungumzwa rushwa mara moja jamii inaangazia rushwa kubwa zinazotamalaki katika duru za wakubwa, lakini uhalisia ni kuwa kama ambavyo hutakiwi kuidunisha na ukaiacha kheri yoyote iwayo hata iwe ndogo kiasi gani kwa mtazamo wako, kama vile kuondoa barabarani chochote kinachoweza kumdhuru mpita njia (msumari au kipande cha chupa iliyovunjika), ndivyo hivyo hivyo unavyotakiwa kuiogopa dhambi yoyote iwayo bila kujali udogo wake.
Kwa muongozo huu wa Uislamu utaona kuwa njia bora ya kuhakikisha rushwa inatokomezwa na kwa jamii kuikataa rushwa na kukataa kuizoea na kuiona ni kitu cha kawaida bila kujali kiwango au aina ya rushwa husika.
Hapa nitoe mifano michache ya rushwa iliyozoeleka katika jamii na jamii kuikubali na kuiridhia na wakati mwingine kutoihesabu kuwa ni rushwa na ndio mbegu ya kumea kwa rushwa kubwa.
Kwa mfano, mtumishi anayekusanya mapato kupewa zawadi na walipa kodi.
Wakati wa Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) mtu mmoja alitumwa kwenda kukusanya kodi eneo fulani na aliporudi akawasilisha alichokusanya na kudai kuwa kingine amepewa zawadi.
Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) aliikataa mbegu hii mbaya ya rushwa na kumuamuru kukabidhi pia kile alichodai kupewa zawadi.
Utaona hapa kuwa Mtume amezuia mbegu mbaya ambayo ikizoeleka italeta madhara makubwa. Sasa tujiulize:
Pale mfanyakazi anapotimiza wajibu wa kutoa huduma anayolipwa na aliyemuajiri kisha akatarajia na hata kuomba ‘nauli’ kutoka kwa aliyemhudumia hiyo siyo rushwa iliyozoeleka hata ikiwa kiwango kinachotolewa ni kidogo?
Nini tafsiri sahihi ya tangazo lililotolewa kwa lugha ya Kiingereza katika gazeti la lugha ya Kiswahili au tangazo lililotolewa kwa lugha ya Kiswahili katika gazeti la lugha ya Kiingereza?
Nini maana ya mfumuko wa wapeleka zawadi kwa kiongozi baada ya kuteuliwa katika nafasi fulani? Ndio maana Uislamu ukaruhusu kiongozi aendelee kupokea zawadi kutoka kwa wale aliyekuwa akipeana nao zawadi kabla ya kuwa kiongozi, na si vinginevyo.
Kwa kuwa rushwa ingawa inafanywa kwa siri baina ya mtoaji na mpokeaji hudhihiri katika maisha ya mpokea rushwa, miongoni mwa njia sahihi ya kutokomeza rushwa ni jamii kuacha tabia ya kuwaona ‘wajanja’ wale wanaodhihirika kuwa na utajiri usiobebwa na historia ya vipato vyao. Jamii inapoonesha kuwakubali ‘wajanja’ hawa na kuwafanya ni mifano ya mafanikio katika kutafuta maisha ni tabia mbaya inayopanda maangamizi ya rushwa katika jamii.
Nihitimishe makala hii kwa kusisitiza kuwa Uislamu umeharamisha rushwa na kila aina ya ufisadi unaompa haki asiyestahiki na kumyima haki anayestahi au kumlazimisha mtu kuinunua haki yake anayostahiki.
Tukumbuke kuwa rushwa ina madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla na Uislamu umebainisha kuwa mtoa rushwa, mla rushwa na dalali wa rushwa wote wamelaaniwa na kwa hakika mtoa rushwa na mpokea rushwa wataingia motoni. Ndugu yangu, ikiwa moto huu wa duniani hatuthubutu kujiunguza nao, tutaweza kuukabili moto wa Mwenyeezi Mungu huko akhera?
Hivyo basi, kila mwanajamii atekeleze wajibu wake wa kujiepusha na kulaaniwa kwa kuiogopa rushwa kama ukoma na kila mwanajamii amnasihi mwanajamii mwenzake juu ya madhara ya rushwa na kila kiongozi wa familia afanye juhudi ya kuiepusha familia yake na moto wa Mwenyeezi Mungu kwa kuwa mbali na rushwa kama Mwenyeezi Mungu alivyotutaka na tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 66 aya ya 6 kuwa: “Enyi mlioamini jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyeezi Mungu kwa anayowaamrisha na wanatenda wanayoamrishwa.”
Acha rushwa utalaaniwa.
Acha rushwa itakupeleka motoni.
Haya tukutane Jumanne ijayo In Shaa Allaah.
Mwandishi wa makala hii, Sheikh Hamis Mataka, ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Baraza Kuula Waislamu Tanzania (BAKWATA). Anapatikana kwa namba: 0713 603050, na 0784 603050.