Mwalimu anaumwa? Ni swali linalotuumiza. Hatuamini. Walio karibu wanazo taarifa, lakini wanatakiwa wawe watulivu maana kusambaza taarifa za ugonjwa wa Mwalimu kungeweza kuibua taharuki kwa maelfu na kwa mamilioni ya Watanzania waliompenda.
Mwalimu ametoka Butiama Septemba 23, 1999. Amewasili Msasani usiku. Amepumzika. Usiku wote ninawaza namna ya kufanya, maana tumenong’onezwa kuwa kesho atakwenda kwenye matibabu nchini Uingereza. Usiku huu ninakata shauri – kesho nichelewe kufika ofisini. Namtaarifu mhariri wangu, naye ananiruhusu.
Septemba 24, muda wa saa 3 hivi asubuhi, ninapanda juu ghorofani. Nasimama nje ya mlango wa chumba cha kulala cha Mwalimu. Namsubiri atoke nimsabahi, pia nimtakie heri huko aendako. Baada ya dakika kadhaa, daktari wake, Profesa David Mwakyusa, anatoka. Zinapita dakika kadhaa bila kumwona Mwalimu. Nami najiapiza kutoondoka hapa niliposimama hadi nimsabahi.
Punde Mwalimu anafungua mlango. Anajitahidi kuonyesha uso wa bashasha kama ilivyo kawaida yake, lakini anaonekana si Mwalimu niliyemzoea – Mwalimu wa vibwagizo, Mwalimu wa misemo, Mwalimu wa kucheka.
Ananipa mkono, nami nampa. Tunakumbatiana kama ishara ya upendo. Namwamkia. “Ooh! Meja salama?” Ananiuliza. Nampa pole na kumuuliza: “Mwalimu tumeambiwa unakwenda kutibiwa, pole sana.” Anajibu: “Ndiyo, naenda, lakini sijui …” Hilo neno ‘lakini sijui’ linanipa shaka. Ni neno la kuumiza kutoka kwa mtu niliyempenda na kumheshimu mno. Ni sentensi fupi inayonifanya ninyong’onyee. Nalengwa lengwa machozi nikiwa nimejaa hofu, maana si mimi tu, lakini wengi wetu hatukuwahi kumwona Mwalimu akiumwa kiasi cha watu kujua anaumwa!
Namwombea heri katika matibabu, naye anashukuru na kuanza kushuka ngazi. Chini, katika eneo alilopenda kuketi na wageni wake, Waziri Mkuu Frederick Sumaye, anamsubiri. Mwalimu anaketi na anazungumza na waziri mkuu kwa dakika kadhaa. Gari aina ya Benz lenye namba TZK 6902 liko tayari kumpeleka Mwalimu na Mama Maria uwanjani, tayari kwa safari ya Uingereza.
Tulizoea kumwona akisafiri ughaibuni akiwa mzima, lakini leo anakwenda akiwa mgonjwa. Sote tuliopo hapa ni kama tumemwagiwa maji baridi.
Kauli ile ya ‘lakini sijui’ inaendelea kuniumiza akilini. Inanifanya nimpigie simu mwandishi mwenzangu, Mbaraka Islam na kumwomba ampate mpiga picha Emmanuel Herman, ili wawepo uwanjani wakati Mwalimu akiondoka. Ni Herman pekee ambaye wakati huo akiwa Habari Corporation, alipata picha za mwisho za Mwalimu akiwa hai katika ardhi ya Tanzania. Pale uwanjani viongozi wawili tu waliagana na Mwalimu. Nao ni Andrew Chenge, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, na aliagana na Mwalimu kwa sababu naye alikuwa akisafiri. Lakini Mkuu wa Wilaya ya Temeke, John Chiligati, ambaye ni mmoja wa wafuasi wa Mwalimu, ndiye aliyekwenda mahususi kumuaga.
Kilichoendelea baada ya hapa kinasikitisha. Ilipotimu Oktoba 14, 1999 giza likatanda katika anga ya Tanzania na ulimwengu wa wapenda haki, amani na maendeleo.
Miaka 20 baadaye, msiba haujafutika na sioni wa kuufuta. Namshuruku Mungu kwa kuniwezesha kuwa miongoni mwa wale tuliopata bahati ya kuishi karibu na binadamu huyu wa aina yake.
Ninakukumbuka Mwalimu kwa mengi ya kusisimua. Mara zote sikuwa na jina jingine kwako, isipokuwa ‘Mwalimu’. Ulikuwa Mwalimu wa kweli ambaye hukuchoka kuwapa elimu wenye kuihitaji. Nakumbuka wakati nikiwa kidato cha kwanza nilikuuliza maswali mengi ya baiolojia, na kwa sababu pengine ya utoto, nilikutega mengine, na wewe ukayategua. Nilipokuuliza maswali ya fizikia, ukarusha mpira kwa Emil Magige, ukisema yeye alikuwa bingwa wa eneo hilo. Wewe uliimudu baiolojia.
Mwalimu ulikuwa na upendo wa hali ya juu. Wewe na Mama Maria hata wakati mwingine mlibana haki za watoto wenu wa kuwazaa na kuwabeba ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa na mahitaji. Mmefanya kazi kubwa si kitaifa tu, bali hata kwa familia. Matunda yenu yanaonekana.
Nakumbuka nilivyokosa kwenda shule kwa sababu ya kuishiwa viatu, lakini wewe ukatoa jozi yako moja kati ya tatu ulizokuwa nazo, ukanipa ilhali ukijua unasafiri Ulaya. Hukunipa ili ukanunue nyingine Ulaya, bali ulinipa kwa sababu ulikuwa na upendo.
Bado ninakumbuka nilipoishiwa viatu tena mwaka 1989 nikakueleza, ukakaa kimya kwa siku kadhaa. Siku ambayo sikuitarajia ukamtuma Aloyce Tendewa aniite asubuhi mapema nikiwa chumbani kwangu. Nilipoambiwa ‘Mwalimu anakuita ofisini’ nusu nizimie, maana kuitwa ofisini kwako kulikuwa mtihani mkubwa mno. Mwalimu hukufoka wala hukupiga, lakini kitendo cha mtu kuambiwa anaitwa na Mwalimu, kilitosha kumtoa jasho hata bila kujua anaitwa kwa shauri gani. Hukuzoeleka. Ulipokaribiwa ulikuwa kama na nguvu za sumaku, na wewe kwa kujua watu walijaa hofu walipokukaribia, ulifanya kila liwalo wakuzoee.
Nilipobisha hodi ukaitika na kunikaribisha kwenye kiti huku ukinitazama kwa ule mtazamo wako wa kuinamisha kichwa ili miwani ishuke na macho yabaki yakinitazama! Baada ya kukusabahi na wewe kunitoa hofu ukasema: “Haya, lile ombi lako …msimamo huu ukanunue viatu.” Kwenye soga, Mwalimu alipenda kutumia neno ‘msimamo’ kumaanisha fedha.
Nikazipokea. Nikahesabu noti 15 za Sh 100 – hizi zilikuwa Sh 1,500. Nilikuambia kiasi hicho nisingepata kiatu, ukasema: “Basi, utafanya maarifa bwana…” Kweli, nilifanya maarifa nikaongeza nyingine 1,500 nikapata kiatu safi kabisa.
Mwalimu nikisema niandike ‘untold stories’ zinazogusa uungwana na ubinadamu wako kwangu, nitajaza kitabu. Leo wala sitazungumzia baiskeli aina ya ‘Swala’ uliyonipa ili imalize shida zangu za usafiri. Wala sitagusia kabisa zile sherehe za ufunguzi wa shamba kule Mibiru ambako nilikusomea risala ukiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano – mimi nikiwa hata sijaingia darasa la pili. Baada ya kusoma risala ile ulinibeba juu juu ukiwa umefurahi mno. Ulinitamkia maneno ya heri ambayo yamekuwa mwongozo wangu. Wala leo sitagusa ulivyobisha hodi nyumbani kwa mama ukiwa umechoka, ukamuuliza mama alichopika. Akakujibu amepika mahindi. Ukasema huondoki hadi yaive. Ukavuta kiti na kuketi kivulini hadi yalipopakuliwa, ukala, ukaomba maji ya kunywa. Ukaaga. Haya yanatendwa na wachache wa kariba yako katika ulimwengu huu.
Niseme nini Mwalimu? Jambo moja nimuombe Mola – anijalie maisha, niandike kitabu kidogo chenye kuwasaidia walimwengu kutambua kuwa nje ya siasa ulikuwa baba, babu, jirani, mwananchi, mpiga kura, Mzanaki uliyeenzi asili, na raia kama walivyo raia wengine. Ulifiti kwenye makundi yote – kuanzia kwa makabwela hadi kwa watawala wa dunia. Pumzika kwa amani Mwalimu.