Ndugu Rais, imeandikwa; samehe hata saba mara sabini. Umetufundisha wanao kusamehe. Baba mwema huonyesha mfano kwa wanaye kwa kutenda yaliyo mema.

Wanao yatulazimu kuiga mfano mwema uliotuonyesha. Hivyo, katika maisha yetu ya kila siku tujifunze kusameheana pale tunapokoseana wenyewe kwa wenyewe. Na ili msamaha wetu uwe wa maana mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya wanadamu waliowema lazima usiwe wa kibaguzi. Tunapowasamehe, tuwasamehe wote kwa makosa yao yote! Hivyo ndivyo anavyosamehe Muumba wetu.

Katika sala ya Baba yetu tunasali, “Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea!’’ Tunamthibitishia Muumba wetu kuwa tusiposamehe ni haki yetu nasi tusisamehewe. Lakini katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Kama Baba usingesamehe, kama ungetuhesabia makosa yetu yote, kati yetu sisi nani angesimama? Wakuiona Mbingu wangekuwa wachache!’’

Kwa kuwa mamlaka pekee katika nchi hii ya kutamka kuwa hii mali ni halali au ni ya kifisadi ni mahakama peke yake; na kwa kuwa mahakama haijapewa fursa ya kutamka hivyo, basi fedha zote tunazodai kuwa zinarudishwa tunafanya ufisadi ule ule. Kuyapuuza yote yanayosemwa haitakuwa busara. Utii wa kikondoo umeubebesha msamaha sura ya amri na maelekezo. Watu wateswe kwanza ili kuwalainisha. Tufanye basi, utaratibu wa kuwawezesha na vibaka kurudisha simu na kuku walizoiba ili nao watoke kama kidanganyio.

Malipo yetu kutokana na misamaha yetu tunayotoa kwa wengine ni thawabu kutoka kwa Allah na si vinginevyo. Kama msamaha wetu ukitanguliza tutapata nini kutoka kwa yule au kwa wale tunaowasamehe, msamaha wetu kwa Mwenyezi Mungu unapoteza maana nao unakuwa batili. Hiyo sasa inakuwa ni biashara ya nipe nikupe. Si vema kulitaja jina la Allah katika hali kama hii! Tuwasamehe wote wenye vya kurudisha na wale wasio na vya kurudisha. Wako watu ambao hawakukwapua popote wala hawakutuchukulia kitu, lakini nao wamezuiliwa. Kama tunasukumwa na moyo wa huruma hawa wafanye nini ili nao watoke?

Kwa utaratibu huu wale watu ambao walivyo navyo ni vyao kwa halali kabisa, hawakukwapua mahali, hawakukwepa kulipa chochote, wala hawakuiba wala kumdhulumu mtu, lakini nao wako magerezani, wanateseka isivyo halali! Inapotokea nafasi kama hii ambayo itawalazimisha wao wenyewe au ndugu na jamaa zao kuuza kila walichonacho ili kuwakomboa ndugu zao, laumu itashuka juu yetu.

Upelelezi haujakamilika ni kisingizio dhalimu. Kupeleleza ni kutafuta ushahidi. Sasa kama ushahidi hauko upelelezi utakamilikaje? Tutabaki kuzuga tu, lakini tutakuwa tunatesa watu huku dunia ikituangalia kwa jicho lisilo radhi! Ieleweke kuwa siku hata miaka itapita, lakini haki yao haitapita!

Mwanamwema aliniandikia, “Mwalimu Mkuu huyu Jaji Mkuu tuliyenaye anatamani makosa yote yawe na dhamana’’. Watanzania tuna bahati ya kumpata mwanamwema kuwa Jaji Mkuu wetu. Ndugu zetu Wakenya chini ya uongozi makini na mahiri wa Rais wao Uhuru Kenyatta sasa wanajinafasi kwa sheria njema zisizokandamizi. Makosa yote yana dhamana.

Basi, wanawema somo hili litukumbushe kuwa sisi ni watoto wa baba mmoja. Mama yetu Tanzania ndiye tuliyepewa na Mwenyezi Mungu katika umoja wetu, kwa neema tu! Vyote na viwe, lakini nchi yetu kwanza! Kama ambavyo dini zetu hazijatugawa, basi asitokee wa kutugawa kwa kisingizio chochote. Tuyazingatie yanayotuunganisha na kamwe tusiyaabudu yanayotutofautisha hata kama ni vyama vya siasa! Tuunganishe nguvu zetu tuwe kitu kimoja ili tumpe nguvu baba yetu ya kuwabaini wote ambao ni vikwazo kwa katiba mpya kupatikana. Uchaguzi unakuja, hawa tuwakatae!

Waliokubali kurudisha fedha wanazotuhumiwa wanathibitisha namna vyombo vya dola vilivyoshindwa kuwatia najisi. Sasa wanashauriwa eti wakubali yaishe. Hii haiwezi kuwa haki, bali udhulumishi. Yawezekana katiba mpya ingesaidia kutunyoshea njia katika baadhi ya maeneo kama haya. Upelelezi usiokamilika ni upelelezi usiokuwapo.

Kuna watu wanaonekana wamegoma kufikiri juu ya mambo ambayo labda kwao yanaonekana ni madogo, lakini tafsiri yake ni kubwa. Naamini timamu hawezi akaamini kuwa kutenda kosa si kosa. Lakini meingine atakwambia kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa. Unamuuliza sasa kukosa ni kufanya nini au ni kutenda nini? Hajui. Sentensi kama hizi zinapotamkwa mara zote anayezitamka au wanaozitamka huwa wamesimama kufikiri.

Tunapokiri kuwa kazi ya kutafsiri sheria ipasavyo ni ya mahakimu, majaji na wanasheria wengine, hatusemi kuwa sisi tunaacha kufikiri sawasawa kuhusu sheria zetu.

Wengi wanafahamu kuwa napinga kwa nguvu zote adhabu ya kifo. Ninachopinga mimi siyo adhabu kama adhabu, bali tendo la kuua hata kama ni kwa kisingizio kuwa ni kutekeleza adhabu dhidi ya aliyeua. Ni kweli tangu kuzaliwa kwangu nimeshindwa hata kuchinja kuku sembuse kumuua mtu! Lakini wote tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu alimkabidhi Musa amri kumi, katika Mlima Sinai maarufu kama Amri Kumi za Mungu. Katika hizo amri kumi usiue imo. Haihitaji kufikiri sana kutambua kuwa si sahihi kumwadhibu muuaji kwa tendo lake la kuua kwa wewe kutenda tendo hilo hilo la kuua hata kama ni dhidi yake muuaji huyo huyo! Mimi siyo katibu mwenezi wa Mwenyezi Mungu, lakini dawa ya moto haiwezi kuwa moto! Ambao wanajiona ni halali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mwanadamu kunyonga au kuua wengine, sijajua Mwenyezi Mungu anawaweka katika kundi lipi.

Watanzania wanaambiwa kuwa Ndugu James Rugemalila msimamo wake ni kuwa hatajali atakaa miaka mingapi gerezani, lakini anaamini haki yake itapatikana kesi itakapofikia ukomo. Anasema hawezi kukiri jambo lisilo la haki ili awe huru. “Niacheni nibaki jela na waacheni wanihukumu ndo itakuwa mwisho wa hii kesi’’.

Sijui kwanini wakati wa shida Mungu huonekana amekaa mbali! ‘Serikali ina ushahidi wa kutosha’ ni kauli mufilisi. Ushahidi wa kutosha uliogandamana mfukoni mwako huu mwaka wa nne utaisaidiaje Serikali kushinda kesi kama siyo kuzidi kuichafua Serikali mbele ya wote wanaoheshimu utu wa mwanadamu na ambao bado hawajamuasi Mungu wao? Hawa ndiyo baadhi ya viongozi wetu ambao hawana upeo wa kuona madhara makubwa yanayoweza kuipata nchi iwapo Serikali itashindwa. Baadhi yao wamegoma kabisa kufikiri! Ah! Tanzania masikini! Yatakapokuwa yanakujiria msaada wako utatoka wapi?