Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amejipambanua kama mmoja wa viongozi hodari wanaofuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watumishi wa umma.

Wengi watakubali kuwa waziri mkuu kila alipofika ameleta mtikisiko kwa viongozi wazembe, wala rushwa, wabadhirifu na wasiowajibika kwa mujibu wa miongozo, kanuni na sheria. Mtikisiko wa karibuni umetokea mkoani Morogoro ambako Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Maendeleo wameng’olewa.

Moto huu wa waziri mkuu umeshawaka kote alikopita, kiasi kwamba watumishi wa umma wanaposikia kiongozi huyo anakwenda katika maeneo yao hujipanga kweli kweli.

Tunampongeza Waziri Mkuu Majaliwa, si kwa sababu amekuwa chanzo cha ‘kutumbuliwa’ watendaji wasiofaa, bali ni kutokana na umahiri wake katika ‘kunusa’ madudu mbalimbali na kuyaanika hadharani.

Kinachofanywa na kiongozi huyu, kama kingekuwa kinafanywa na mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na watendaji wengine, hakika tungeyaona mabadiliko makubwa ya maendeleo katika taifa letu.

Kwa muda mrefu tumekwama kwa sababu ya viongozi wazembe, wala rushwa, wasiowajibika na walevi wa madaraka. Kuna viongozi wanaojiona miungu-watu, wasiotaka kutatua kero za wananchi.

Ni jambo la kusikitisha kuona mambo mengi ya ovyo yakiendelea katika ngazi mbalimbali za uongozi bila wahusika kuyashughulikia au kuchukua hatua kwa wanaoyafanya. Matokeo yake tunaona ziara za viongozi wakuu wa kitaifa – Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu – zikipambwa kwa malalamiko ya wananchi wanyonge.

Akiwa mkoani Iringa, waziri mkuu amewapiga marufuku wote wanaowazuia wananchi kuonyesha mabango yenye ujumbe unaoakisi kero zao. Tunampongeza waziri mkuu kwa sababu mabango ndiyo njia rahisi ya mnyonge kufikisha ujumbe wake.

Tunamsihi Waziri Mkuu Majaliwa aendelee kuchapa kazi bila hofu, kwani ameonyesha utii kwa aliyemteua, pia kwa wananchi. Aendelee na moto huo huo hadi watumishi wa umma wabadilike kifikra, watambue kuwa utumishi wa umma ukishaukubali hauna hiari, bali kuwatumikia wananchi tu.

Kuanzia sasa kule ambako kuna kero zisizotatuliwa na viongozi waliopo, wa kuwajibishwa wawe hao walio katika maeneo au ngazi husika. Kitu muhimu cha kumpa waziri mkuu na viongozi wenzake wachapakazi ni kuwaunga mkono kwenye mapambano haya.