Baada ya kupata Uhuru nchi nyingi za Afrika na Tanzania yetu ikiwamo, wapo wananchi hawakuamini wala kuthamini ule utawala wetu wa wazawa. Yapo bado mawazo ya uzungu-uzungu na tamaa ya wasomi kutambuliwa kama Wazungu.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuchoka kuelimisha wananchi tatizo hili ili waachane na kasumba ya uzungu na kujiona wako wenyewe watu huru kabisa. Alitumia njia nyingi kutuelimisha hili.

Mapema mwaka 1963 alitoa waraka aliouita “Pomposity”. Mle aliwarudi viongozi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na wa Serikali kuachana na tamaa za ufahari na ukuu, na wanapaswa wawatumikie wananchi kwa kutatua matatizo yao. Kama hilo halitoshi, aliunda wizara mpya katika serikali yake akaita Wizara ya Utamaduni na Vijana – kukuza uzalendo katika nchi yetu.

Lakini wazee wengi tunajua mpaka leo hii miaka 58 ya Uhuru wetu, bado katika nchi yetu wapo wananchi, tena wasomi waliobobea katika elimu ya kizungu ya nchi za magharibi wangali hawajafunguka kiakili juu ya kitu UZALENDO NA UTANZANIA. Kwao bado mambo ya uzungu na demokrasia ya magharibi ndio ustaarabu. Matendo, lugha yao na imani yao bado inawatuma kujali kila kinachoelekezwa na Wazungu, iwe kisheria, kielimu na hata kiutamaduni.

Mimi ningali najiuliza, pale Mei 20, 1974 wakati Mwalimu Nyerere anaeleza juu ya kujikomboa na akawaambia wasomi kwenye kongamano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba Waafrika bado hatujajikomboa; maana ukombozi wa kweli, Mwalimu Nyerere aliutaja ni ule wa “Mental Liberation”- ukombozi wa kifikra! Hawa wasomi kwa vipi mpaka leo hii bado wanasujudu uzungu?

Labda tu niwarudishe nyuma kimawazo wasomaji wa makala zangu juu ya jambo hili kwa kumnukuu Mwalimu alipofungua Semina ya maafisa wa JWTZ kule Bagamoyo Novemba 24, 1970 kwa kutumia maneno “KUWA KAMA BWANA” (Warumi walisemaga kwa Kilatini “quails servus talis dominus). Siwezi kunukuu hotuba ile yote, lakini hapa nitaeleza kiufupi sana yale maelezo yake muhimu.

Mwalimu alisema tangu kabla ya Uhuru “…Uhuru wetu si wa kukomboa nchi, tunakomboa utu wetu. Kwa hiyo tukasema lazima tujitegemee wenyewe Waafrika. Tungekubali Wahindi watusaidie na Wazungu watusaidie, Waswahili wangesema kuwa kama si Wahindi, au kama si Wazungu tusingepata Uhuru…”

Hayo ndio yalikuwa mawazo ya Mwalimu au niseme huo ndio ulikuwa mtazamo na msimamo wa Mwalimu miaka ile ya 1956 – 1958 alipokuwa Rais wa TANUalipoanzisha mchango wa ujenzi wa Makao Makuu ya Chama cha TANU pale Lumumba (Ujamaa ni Imani 1 uk. 44 ibara ya kwanza).

Basi, wakati anazungumza na wale maafisa wa JWTZ kule Bagamoyo aliwaelezea kwa urefu hayo mawazo ya kujikomboa kifikra. Sasa ninukuu kidogo mpate kuona tuliyoyasikia sisi siku ile kisha nitakuja kuwaelezea juu ya hao vibaraka wa Wazungu tulionao humu nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Kwanza Mwalimu alieleza kwa ujumla namna hii, namnukuu; “…Hakuna mtu anayeweza kutwambia kama iko njia maalumu iliyowekwa kutatua matatizo yetu hapa. Mafundi wa kutatua matatizo yetu ni sisi wenyewe…”

“…Wakati tunadai Uhuru wetu Waingereza walituambia kuwa demokrasia iko namna moja tu, nayo ni ya Kiingereza. Waingereza wanaamini kabisa namna yao hiyo na kwao kama haifanani na hiyo basi siyo demokrasia…” (Ujamaa ni Imani 1 uk. 44)

Fikra namna hii ndugu wasomaji, mpaka leo zipo bado humu nchini mwetu. Wanasiasa kadhaa bado wanaamini hivyo, na wangali wanadai demokrasia inayofanana na ile ya Uingereza kinyume chake kwao hiyo siyo demokrasia.

Hii ni kasumba iliyopata kutu miongoni mwa wasomi kadhaa katika nchi huru za Bara letu la Afrika. Serikali yetu kuanzia ile ya Tanganyika ya Awamu ya Kwanza, mpaka hii ya Tanzania ya Awamu ya Tano tumekuwa tunasema serikali yetu ni ya wananchi, wazawa wa Tanganyika na sasa wa Tanzania. Tuna Uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe. Hatupaswi kupokea maagizo kutoka “Westminster” kule kwa Mwingereza aliyetawala eti tufanye hivi au tusifanye vile! Ndiyo uhuru halisi huo wa sisi kujiamulia mambo yetu.

Ndipo Mwalimu akawa anatoa mifano ya aina ya kasumba au mawazo waliyokuwa nayo baadhi ya wasomi wetu hapa nchini. “…Wengi hasa wasomi wanavyosoma vitabu hivyo vya demokrasia hizo, usipotekeleza mambo kama ilivyoandikwa katika vitabu vya ‘Westminster’ wao huona taabu sana…”

Ile tabia ya kuiga vya Ulaya, kimavazi, miondoko na hata matamshi ya baadhi ya majina, yaani muonekano wote wa msomi uelezee ustaarabu wa kizungu ndiyo kasumba yenyewe. Kwa kuchekesha wasikilizaji wake pale Bagamoyo Mwalimu alitoa mfano huu; Mswahili aliyesoma kule Uingereza (au Ulaya kwa ujumla) Ziwa “Nyasa” atalitamka “Nayasa” au amkio badala ya kusema “hamjambo” yeye atakenua midomo kwa kutamka “hamjamboni watu yote”.

Baada ya utani ule Mwalimu Nyerere akawa ‘serious’ na kutoa mfano wa tamaa za “kuwa kama bwana” kwamba mtumwa anapotamani kupata uhuru anajisemea moyoni, “Endapo nikipata uhuru wangu, nitakuwa hivi hivi kama bwana wangu (Mwarabu). Nitavaa kanzu, kama bwana, nitashika mkwaju mkononi kama bwana na nitafunga kilemba kichwani kama bwana wangu anavyofunga na kupachika jambia kiunoni kwa mbele kama vilevile anavyokuwa bwana.”

Na kweli, pindi akijaliwa kuwa huru, jambo lake la kwanza ni kuiga na kufanya hivyo kama bwana wake. Basi, huyu mtumwa anataka uhuru ili awe kama bwana wake. Kumbe hiyo siyo shabaha ya uhuru!  Uhuru shabaha yake yule mtu awe mwenyewe mtu kamili; na siyo kuwa kama bwana – kivuli cha mtawala! (pengine wanaita nokoa).

Hili linaonekana siyo kwa watumwa wa Waarabu tu, la hasha! Hata kule Marekani, watumwa katika yale mashamba ya Wazungu walikuwa wanalilia uhuru ili wawe kama Wazungu na wakubalike na Wazungu mabwana zao. Kwa miaka mingi mpaka leo hii manegro [Wamarekani weusi] kule Marekani wangali wanatamani na wanaomba watambulike na Wazungu (Wamarekani weupe) kuwa nao (manegro milioni 20 hivi walitokana na kizazi cha watumwa) watambulike kuwa wako sawa sawa kabisa na wenzao Wamarekani weupe; Jambo ambalo mpaka leo hii halijawezekana.

Manegro wanaitwa ‘colored’ na siyo ‘white’, basi wamediriki hata kuunda vyama kama vile Black Power kuwatetea hata mahakamani eti mahakama zitamke “Hawa sasa ni weupe!” Hapo nao wakubalike kama Marekani wengine. Yote hayo yameshindikana. Hili la kuwa kama bwana linawaumiza sana ndugu zetu kule Marekani.

Tangu karne ile ya 19 utumwa ulipokomeshwa Marekani ndugu zetu wote wenye asili ya Afrika eti walitakiwa kusahau Uafrika wao, wakalazimishwa kuyakana majina yao ya asili, lugha zao na ndipo sasa kwa ujumla wao manegro wale wakawa wanaitwa– ‘niggers’ kumaanisha rangi za ngozi zao.

Ni hivi karibuni tu mwaka wa 1988, jina hilo la nigger au nigro lilianza kuachwa kutumika na ni baada ya juhudi kubwa sana za viongozi wao kama Mchungaji Jesse Jackson Jr. Ndipo kukaanza kutumika neno ‘Wamarekani wenye asili ya Kiafrika’. Ni ujinga ulioje huo! Mbona hatusikii Wamarekani wenye asili ya Uchina, Uarabu, Uhindi au Ujerumani? Kwanini iwe wenye asili ya Afrika tu? Na bado hao ndugu zetu wangali wanatamani siku ije nao wawe “kama bwana” vile! Watambulike kama Wamarekani weupe.

Mwalimu akasema ugonjwa huu wa kutaka “kuwa kama bwana” rafiki zetu Wachina wanaita watu namna kama hao, ‘running dogs’ maana yake ni kuwa mithili ya vile vijibwa koko ambavyo tuendapo kuwinda vinatumwa kusaka wanyama. Ndipo akamalizia; “Sisi hapa Watanzania hatuwezi kuwa running dogs wa mataifa mengine.

Sisi tumejikomboa kutoka ile hali ya kuonewa, hali ya unyonge, hali ya kunyonywa na Wazungu – basi, kamwe hatuwezi kuwa running dogs wa mataifa mengine. Tulikataa kuwa ombaomba kwa Wazungu.

Kwa nini Mwalimu alitumia muda mrefu kuelimisha maafisa wale wa Jeshi kule Bagamoyo? Baadhi ya wasomi hapa nchini walikuwa wanadai vitu vya kijinga kama vile, ‘kwanini sisi watu weusi tunazuiwa kula katika mahoteli ya kizungu. Mbona tunazuiwa kunywa pombe za kizungu (bia). Mbona nasi tumesoma Uaya na tuna shahada kama wao?” Hayo Mwalimu aliwaelewesha maafisa wa JWTZ wale kuwa shahada siyo kigezo cha uzungu eti ndiyo ustahili kunywa pombe ile ya kizungu. Huo ni ufinyu wa mawazo, ni ulofa wa Wabantu.

Nadhani wengi hawajui tulikotoka. Mwalimu miaka ile ya ukoloni akiwa Pugu alikataliwa kuingia na kula chakula hapo New Africa Hoteli (mwaka 1954) ingawa alikuwa na shahada aliyopata huko huko Uingereza kwao Wazungu.