Kwanza napenda kuwashukuru wote waliotupatia pole ya msiba wa kijana aliyetoweka katika ulimwengu wa habari, mwenye nguvu ya kazi na mweledi wa kile alichokuwa akifanya. Mwenyezi Mungu alimpenda zaidi na hatuna namna nyingine zaidi ya kushukuru kwa kila jambo.
Katika maisha kuna mambo mengi sana ambayo yana nafasi katika maendeleo ya ustawi wetu, changamoto ni sehemu ya maisha. Kila tunapofikwa na jambo la hatari na huzuni tunaongeza ujasiri na kupanua fikra za kupambana na mambo hayo. Siku ikipita na jambo lake tunakuwa tumeongeza kitu katika maisha yetu hapa duniani.
Taifa ni kama familia na taifa pia linapitia masaibu mengi kila siku, yapo ambayo yanasababishwa na watu na yapo ambayo yanasababishwa na taifa jingine. Tanzania kama taifa tunapita katika vipindi vyote muhimu kwa ustawi wa taifa lenyewe, kuna wakati wa huzuni na hatari, tuna wakati wa furaha na amani kama taifa.
Taifa lina sifa zake. Kwanza, linatambuliwa na kusimama peke yake kama chombo kinachojitegemea. Katika kusimama ni lazima uongozi uwepo kwa maana ya kuenenda na msimamo wa pamoja katika jambo fulani.
Ndiyo maana taifa linaweza kupitia hatua kadhaa za maendeleo kwa kukinzana na baadhi ya watu ambao wana mtazamo tofauti na walio wengi. Vilevile walio wengi wanaweza kukinzana na walio wachache wenye msimamo katika mambo wanayoamini.
Leo nimeamua kushika kalamu na kuandika waraka huu nikijaribu kuangalia matawi ya umoja wetu kama taifa katika mambo mengi, hasa yahusuyo ustawi wa jamii yetu. Ninajua fika kwamba kuna mambo ambayo ni ya kitaalamu sana, lakini pia ninajua kuwa utaalamu huo kuna wakati ambapo huleta urasimu ambao hauna tija.
Urasimu wa madaraka ni pigo kubwa kwa maendeleo ya taifa, madaraka yapo mengi katika jamii yetu, wapo waliopewa dhamana ya kuwa viongozi na wapo waliopewa dhamana ya kuwa waamuzi na kutoa utaratibu, katika ngazi zote hizi kuna madhara yake ambayo yametokana na kudhibiti nyendo za wachache kuhodhi mambo au kujilimbikizia madaraka.
Miaka mingi iliyopita wakati taifa hili likipata uhuru, suala la taaluma ya mtu ilikuwa ni hadithi, kilichokuwa kikitazamwa ni uwezo wa mtu katika kuamua mambo kwa usahihi na kwa muda muafaka.
Hakuna kipindi ambacho taifa la Tanzania lilikuwa na uhitaji wa watu wa manunuzi ya umma kama kipindi cha ujamaa na kujitegemea, hakuna kipindi ambacho taifa lilihitaji watu wa kutunza stoo kama kipindi hicho.
Jambo lililo jema ni kwamba kila aliyejua kusoma na kuandika na pengine kuwa na sifa ya kumaliza darasa la nne au la saba alipata kazi na alifanya kazi kwa weledi wa hali ya juu sana. Wapo ambao hawakumaliza shule lakini walitokea wakapata ajira na walifanya vizuri sana.
Tatizo kubwa ninaloliona leo hata sielewi linatokana na nini, inawezekana suala la ajira likawa linapingana na dhana ya kujua akifanyacho mtu, lakini suala la mafunzo rasmi ya jambo fulani ili kuwa mtaalamu mbobezi katika uga fulani limekuwa ni kero kwa mfumo wetu wa kujiongoza mpaka unajiuliza maswali ambayo labda yanaweza kukosa majibu.
Si kweli kwamba kilichofanywa zamani na mtu wa darasa la saba katika bohari ya chama cha ushirika kina tofauti yoyote ile na kile ambacho leo kinafanywa na mtu mwenye digrii kadhaa za uga huo, lakini ubaya wake unakuja kujitokeza katika utumishi wa sasa katika suala la uadilifu na kasi ya kutekeleza majukumu yake.
Si kweli kwamba aliyekuwa akiagiza pembejeo zote za kilimo wakati huo alifanya kazi ambayo ni tofauti kabisa na huyu ofisa manunuzi mwenye shahada nyingi tena kutoka pande zote za dunia na kuwa na wasifu wenye kurasa mithili ya kitabu lakini huyu wa leo ndiye huyo anayechelewa kununua au kununua bidhaa ambazo soko lake linakinzana na mahitaji, huwa nikifikiria haya ninafikia mahali ninasema SHIKAMOO DARASA LA NNE.
Najua wasomi wapo, najua dunia inahitaji elimu, najua wasomi mnajua nasema nini, ila kwa ufupi usomi wenu msiulazimishe kutuletea ukiritimba na urasimu usio na maana katika kutuletea maendeleo huku mkijua kuna siri kubwa katika ukiritimba wenu.
Tunataka watu wanaojua, si waliokariri; tunataka wasomi wanaorahisisha maisha si kutuumiza katika maisha.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.