Kuna mambo kadhaa mawili yaliyotokea katika Jiji la Dar es Salaam yenye kuakisi udhaifu wa baadhi ya watendaji katika serikali na idara zake.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza katika machinjio ya Vingunguti jijini humo na kustaajabu namna ujenzi wa machinjio ya kisasa unavyosuasua.

Katika hali ya kuumia moyoni, Rais Magufuli hakusita kuonyesha hisia zake. Alionyesha hasira za wazi kutokana na namna baadhi ya watendaji wanavyochelewesha miradi.

Baadaye hali kama hiyo ikawa kwenye ufukwe wa Coco, Oysterbay katika Jiji hilo hilo la Dar es Salaam. Licha ya fedha kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa, hakuna kazi iliyokuwa imeanza.

Baada ya Rais Magufuli kuonyesha hasira zake, tayari ujenzi umeanza kwa kasi ya ajabu katika maeneo hayo mawili. Ikumbukwe, hali ilikuwa kama hiyo kwenye ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Tunampongeza rais kwa mengi. Mosi, ni kwa kuhangaika kupata fedha kwa ajili ya kutengeneza miradi mingi ya kijamii. Pili, tunampongeza kwa ujasiri wa kwenda ‘maeneo ya matukio’ kujionea hali ya mambo.

Kiongozi wa kweli ni yule anayetoka ofisini na kwenda kukagua miradi ya maendeleo. Viongozi wamekuwa wakidanganywa kwa sababu hawataki kutoka ofisini, badala yake hujiegemeza kwenye ripoti ambazo mara kadhaa huwa zina hadaa na ghiliba.

Kuna jambo la kujiuliza, hivi kama Rais Magufuli asingekwenda Vingunguti na kama asingehoji mkwamo wa ujenzi pale Coco Beach, hali ingekuwaje?

Ni miaka minne sasa tangu Rais Magufuli ashike madaraka ya kuongoza nchi. Msimamo wake kwenye masuala ya maendeleo umekuwa wazi tangu mwanzo. Tunauliza, iweje hadi leo baadhi ya wasaidizi wake hawajamwelewa?

Zamani tulisikia kilio cha “serikali haina fedha…” Leo kilio hicho hakipo, na kama kipo, basi ni kwa sauti ya chini. Fedha za miradi ya maendeleo zipo tele. Miradi mingi inajengwa kwa matrilioni ya shilingi kote nchini. Haiwezekani katika mazingira haya ya kuibadili nchi, kukawapo genge la watendaji wanaotaka kuchelewesha mambo.

Haiwezekani rais ahangaike kukusanya fedha kutoka kwa walipa kodi kwa lengo la kuzitumia kujiletea maendeleo kitaifa, halafu wakawapo wengine wanaozembea, kwa makusudi, au hujuma kutekeleza miradi.

Miongoni mwa sababu za ucheleweshaji wa miradi hii ni urasimu na rushwa. Tunatoa mwito kwa wasaidizi wote wa Rais Magufuli kubadilika ili kuendana na kasi yake ya maendeleo. Pale mambo yanapokwamishwa bila sababu za msingi, hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wahusika. Tunauliza, mtumishi ambaye hajajua rais au nchi inataka nini, ana sababu zipi za kumfanya aendelee kuwa hapo alipo?