Lazima wahakikishe kwamba kazi zote zinaendeshwa barabara, na pamba ya aina itakiwayo inapatikana na wakati ule ule inapoatakiwa; wahakikishe kwamba hakuna kipingamizi kutoka hatua moja hata nyingine; kwamba kuna uhusiano baina ya kazi mbalimbali, na kwa sababu hiyo hakuna mfanyakazi anayekaa bure kungojea mwenzake amalize kazi yake.
Wakubwa wa kazi hawana budi kuhakikisha kwamba wananunua pamba ya kutosha, na kwamba wana mahali pa kuuzia nguo zinazotengezwa; kwamba mishahara inalipwa bila ya kuchelewa; kwamba hesabu ya fedha zinazowekwa sawa sawa; kwamba mitambo inakaguliwa ipasavyo; na mambo mengine kadha.
Ili kiwanda kifanikiwe, kutimizwa kwa kazi hizo ni lazima kama vile vile ilivyo muhimu kwa wafanyakazi kujitahidi kuzuia nyuzi zisikatike au dosari katika nguo zinazofumwa. Vilevile wakubwa wa kazi wana wajibu wa kuweka lengo la bidhaa zitazotolewa na kwainda; na kweli bila ya kufanya hivyo hawezi kufanya kazi nyingine. Katika jambo hili nina mambo mawili ya kusema.
Kwanza kabla ya mwisho wa mwaka huu katika Tanzania tutaweza kutengeneza nguo za pamba yadi za eneo milioni 90 kila mwaka, pengine na zaidi. Kama nguo hizi ni madhubuti na za aina itakiwayo, na zinapatikana kwa bei wananchi wanayomudu, basi nguo zote zingeweza kuuzwa humu humu Tanzania bila ya shida yoyote. Lakini haina maana kama kila kiwanda kitatengeneza nguo za aina ileile. Kwa mfano, hatuna haja ya yadi milioni 90 za kanga tupu, bila ya vitenge na nguo za aina nyingine.
Lazima viwanda vigawane kazi, katika kutengeneza jumla ya nguo tunazohitaji, kiasi wanachohitaji. Na tuweze kufanya hivyo, bila kupoteza kitu kama kuna taratibu wa ushirikiano wa mipango kati ya viwanda vyetu vyote. Utaratibu huo ungepaswa kuanzishwa na Shirika letu la Maendeleo, linalomiliki viwanda viwili vikubwa.
Hivyo, wanapaswa kuweka mpango kuhusu aina ya nguo zitakazo tengenezwa, kwa kufikiria nguo ambazo watu wetu hupendelea kununua, na zile ambazo wataweza kuzinunua hapo baadaye, wakati mipango yetu ya uchumi itakapokuwa imeendelea zaidi. Jambo hili ni muhimu. Kama tunataka kutumia viwanda vyetu vipya kwa faida, basi yatupasa kuvifanyia mpango wa pamoja, siyo mipango minne au mitano tofauti, ambayo ikijumulisha pamoja haileti faida yoyote katika nchi yetu.
Lakini mara mipango hiyo itakapokuwa imetengenezwa, tusifanye kama mipango ya siri kubwa. Kwa hiyo neno langu la pili ni kwamba kila kiwanda chetu kipya (na hata vile vya zamani) kiwe na lengo la kiasi na aina ya nguo nguo zitakazotengezwa, na lengo hilo lijulikane kwa kila mfanyakazi anayehusika.
Sisi kuwaomba wananchi wafanye kazi kwa bidii. Lakini katika kiwanda cha siku hizi mtu anafanya sehemu ndogo sana ya kazi ya kutengeneza kitu. Anawezaje kuendelea hivyo mwaka hata mwaka, akijivunia kazi hiyo hiyo moja tu? Wale wenye maarifa zaidi wanaweza kutambua hivyo, lakini ni vigumu kwa walio wengi kufahamu jinsi kazi yao hii moja inayohusiana na idadi ya nguo zinazotengezwa katika kiwanda. Mara nyingi mfanyakazi hata hajui vipi kazi yake hii ndogo inavyoingia katika jumla ya kazi kiwandani; hajui shabaha ya kiwanda hicho. Katika hali hiyo haina maana kuwatarajia wafanyakazi kuwa na ari ya kazi zao.
Kwa hiyo, kila kiwanda tukiwekee lengo, lengo litakaloamuliwa kutokana na wingi wa bidhaa zitakazouzwa, na mahali zitakapo uzwa. Shabaha hizo zifahamike na kila mfanyakazi; yafaa ziandikwe kwa herufi kubwa ukutani; wala tusikomee hapo. Kila kikundi cha wafanyakazi katika sehemu yao nao wawe na lengo la mwaka, la mwezi, na siku. Na hapo basi, baada ya ya kufahamu lengo watu wajue jinsi juhudi yao inavyolingana na ya mwaka uliopita, na mwezi uliopita, au ya jana.
Mimi naamini kwamba wananchi wakiwa na lengo kamili mbele ya yao, na wakifahamu kiasi gani wamevuka lengo hilo, au wana upungufu kiasi gani, wametimiza wajibu wao katika kazi zingine nyingi mnamo miaka michache iliyopita. Watatamani kulivuka lengo hilo watajivunia kiwanda chao kivuka lengo, na wakati huo huo wanatengeneza nguo zilizo bora zaidi. Na watatambua kwamba wakati wanapofanya kazi zao wanatia jasho lao katika mafanikio ya lengo la Tanzania nzima, ambalo ni jumla ya shabaha mbalimbali za viwandani, mashambani na ofisini.
Waheshimiwa, Mabwana na Mabibi, nikiamini kwamba juhudi ya wafanyakazi wote kiwanda hiki kina sehemu kubwa ya kufanya katika kuleta maendeleo ya uchumi wetu nina furaha kubwa kutangaza kuleta maendeleo ya uchumi wetu, nina furaha kubwa kutangaza kwamba kiwanda hiki cha nguo sasa kimefunguliwa, kwa manufaa ya Tanzania.