Mtaalamu wa saikolojia, Dk. Joshua Grubbs, alifanya utafiti katika Chuo Kikuu cha Western Reserve kutaka kujua sababu inayowafanya watu wengi wasifanikiwe kutimiza malengo waliyojiwekea katika maisha yao.
Moja ya sababu kubwa aliyogundua ni kuishi bila malengo, hili ni jambo lililo wazi, watu wengi wanatamani kufanikiwa katika maisha yao lakini wanaishi bila malengo.
Wanaishi bila kujiandaa kufanikiwa. Aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Winston Churchill, alipata kutoa nasaha: “Mafanikio si ajali, ni kujifunza, kujituma, kujitoa mhanga, na kikubwa kuliko vyote ni kupenda unachokifanya.’’
Mafanikio yapo, hayawabagui watu. Wakati mwingine watu hujibagua wenyewe ili wasifanikiwe. Wanafanya hivyo kwa kujua au kwa kutokujua.
Wayner Dyer katika kitabu chake cha The Power of Intention anasema: “Nia yetu inaumba uhalisia wetu. Nia njema ni roho ya mafanikio, aliye na nia ya dhati ya kufanikiwa na anajua kuwa ana nia ya kufanikiwa atafanikiwa.”
Mwenyezi Mungu anataka tufanikiwe, hataki tuwe maskini na ombaomba. Tazama shauku ya Mungu juu ya mafanikio yetu. “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.’’ (3 Yoh 1:2).
Mungu anataka tufanikiwe katika mambo yote yaliyo ya halali. Anataka tufanikiwe katika mipango yetu yote iliyo ya halali. Nasi twatakiwa kukubali kufanikiwa.
Mwanamichezo kutoka Marekani, James Cleveland Owens, alikuwa anatamani kupata medali za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki, aliamua kufanya mazoezi ya hali ya juu sana.
Baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu alimwendea mkufunzi wake na kumuuliza: “Baba nitawezaje kushinda haya mashindano ya Olimpiki na kupata medali ya dhahabu?” Mkufunzi wake alimjibu: “Jitoe sadaka.” James alikubali kujitoa sadaka.
Katika mashindano yaliyofuata alishinda medali tatu za dhahabu nchini Ujerumani na rekodi yake haikuvunjwa kwa muda wa miaka 22. Hii ndiyo nguvu ya kukubali kujitoa sadaka kwa ajili ya mafanikio unayoyataka.
Watu wengi wanatamani kufanikiwa katika maisha lakini wanaogopa kujitoa sadaka kwa ajili ya mafanikio wanayoyataka.
Je, una nia ya kufanikiwa kimwili, kiroho, kiuchumi, kifamilia na kisiasa? Jitoe sadaka kwa ajili ya mafanikio unayoyataka. Fanyika gharama, kubali kuwa mkombozi wa maisha yako.
Mwandishi mashuhuri wa vitabu wa Marekani, Bud Wilson, anasema kama unataka kuwa mshindi lazima ukubali kulipa gharama kubwa.
Dunia inamilikiwa na watu wanaokubali kulipa gharama za mafanikio wanayoyataka. Mgunduzi wa mtandao wa kijamii wa facebook, Mark Zuckburg, anasema dunia inabadilishwa na kumilikiwa na watu wenye nia.
Kupanga ni kuchagua, usipopanga unapanga kushindwa.
Mwanafalsafa, William Ward, anatufundisha kuwa kabla hujazungumza, sikiliza kwanza; kabla hujaandika, fikiri kwanza; kabla hujatumia, pata kwanza; kabla hujalaumu subiri, kwanza; kabla hujasali, samehe kwanza; kabla hujastaafu, weka akiba kwanza; kabla hujafa, toa kwanza.
Mwaka 2012 niliandika makala yangu iliyokuwa inasema: “Krismasi bila Kristu si Krismasi.” Msomaji mmoja alinitumia ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani akisema:
“Ndugu yangu William Bhoke, hii ni Krismasi yangu ya 50, kwa maana hiyo nina miaka 50. Ninachosikitika ni kwamba sina hata mtoto wa kusingiziwa, sina uwanja wala nyumba. Niliajiriwa miaka 12 iliyopita, ninaelekea kustaafu kazi lakini maisha yangu hayana nyuma wala mbele. Nimekata tamaa kabisa, nimejikataa na kukataliwa. Siamini kama nitafanikiwa tena, ninaomba unipe muongozo mpya wa maisha.”
Mpendwa msomaji, usijikatae. Mungu hakuwa na muda wa kuumba mtu ambaye hana maana, bali mtu wa maana tu. Kataa kujikataa.
Kujikataa ni kuhisi kuwa wewe si mtu muhimu, ukweli ni kwamba wewe ni mtu mhimu sana katika sayari hii ya dunia.
Mwenyezi Mungu hakukuumba kwa bahati mbaya, kwa Mungu hakuna bahati mbaya, Mungu hana bahati na sibu.