Kupanga ni kumaliza mwaka kabla hujauanza
Kupanga ni kuvuka daraja kabla ya kulipita, kupanga ni kukata kanzu kabla mtoto hajazaliwa. Kupanga ni kuhesabu mayai kabla ya kutagwa. Kupanga ni kuweka bati kwenye paa kabla ya mvua kunyesha, ni kuchimba kisima kabla ya kuwa na kiu.
Ni kulima mazao ya chakula kabla ya baa la njaa, kupanga ni kuzuia jambo baya kabla ya kutokea. Heri kuzuia kuliko kuponya. Hadhari kabla ya hatari, kupanga ni kutabiri.
“Njia nzuri sana ya kuutabiri wakati ujao ni kuumba,” alisema Stephen Covey. Kupanga ni kujiandaa. “Kwa kushindwa kujiandaa, unajiandaa kushindwa,” alisema Benjamin Franklin.
Kupanga ni kufikiria mapema jambo, kupanga ni kufanya mipango. Kupanga ni kutayarisha ramani. Kupanga ni kunuia, kudhamiria kufanya au kufanikisha jambo.
Kadiri ya kamusi kuu ya Kiswahili ‘panga’ maana yake ni kufanya utaratibu wa jambo. Mpango ni utaratibu wa kufanya jambo kwa hatua ili kufikia lengo linalokusudiwa. Mpango dira ni utaratibu wa kina au mapendekezo yanayoonyesha namna kitu fulani kinavyotarajiwa kufanya kazi.
Kupanga ni kumaliza mwaka kabla hujauanza, usianze mwaka ambao haujaumaliza kwenye karatasi. Usianze mwezi ambao haujaumaliza kwenye karatasi. Usiianze siku ambayo haujaimaliza kwenye karatasi.
“Kila mara panga kabla. Mvua ilikuwa hainyeshi Noa alipojenga safina,” alisema Richard Cushing. Kesho ni ya watu wale wanaojiandalia kesho.
“Tunaishi chini ya mbingu ile ile, lakini hatuna upeo mmoja,” alisema Konrad Adenauer. Kuna ambao wanapanga makubwa, na kuna ambao hawapangi. “Mtu asiyepanga ya mbeleni, atakuta matatizo mlangoni,” alisema Conficius.
Kupanga ni kuishusha kesho na kuiingiza katika leo. Ni kuifikiria leo wakati wa kesho. “Usipofikiria juu ya wakati ujao, huwezi kuwa nao,” alisema John Galsworthy. Kupanga ni kuifufua jana ikusaidie kupanga ya kesho.
Kupanga kunahitaji kuwa na nyuso zaidi ya mbili. Jina ‘Januari’ linatokana na jina la mungu wa Kirumi ‘Janus’, ambaye alikuwa na nyuso mbili, uso mmoja ukitazama yaliyopita na uso mwingine ukitazama yajayo.
Tunahitaji uso wa tatu wa kutazama ya leo, maana matunda ya kesho yapo kwenye mbegu za leo. Kesho inaanza leo, kupanga kunahitaji kuitazama jana iliyozikwa kuzimu, leo iliyo kwenye uso wa nchi na kesho iliyopo mawinguni.
Panga mipango mikubwa, usifikirie madogo yanayolingana na kichuguu. Fikiria milima mikubwa. “Usifanye mipango midogo, haina uchawi wa kusisimua damu za watu,” alisema Daniel Burnham.
“Mipango si chochote, kupanga ni kila kitu,” alisema Dwight D. Eisenhower. Mpango ni jina au nomino dhahania, lakini kupanga ni kitenzi. Kupanga ni kutenda, tena kupanga kunahitaji kufanyia kazi mpango.
“Matatizo ni mipango mingi, imeegemea juu ya mambo yalivyo sasa. Kufanikiwa mipango yako binafsi jikite kwenye kile ambacho unataka, si kile ulicho nacho,” alisema Nido Qubein, rais wa High Point University.
Kuwa na mpango ‘A’. “Kama mpango ‘A’ haufanyi kazi, alphabeti ina bado herufi 25. Kuwa na Mpango ‘A’, mpango ‘B’, mpango ‘C’ na kuendelea. Kuwa na maandalizi ya kushangaza.
“Mafanikio ya kushangaza yanatanguliwa na maandalizi ya kushangaza,” alisema Robert H. Schuller, mwandishi wa vitabu na mhubiri mashuhuri. Sasa hivi kuna mtu anakula embe kwa sababu miaka kumi iliyopita kuna ambaye alipanda mwembe.
Sasa hivi kuna mtu anakata miti ya kujengea kwa sababu miaka 12 iliyopita kuna mtu alipanda msitu. Tatizo kubwa ni kuwa hatupangi kushindwa, tunashindwa kupanga.