Imesemwa mara nyingi kwamba afya ni mtaji. Unapokuwa na ndoto kuwa na afya njema ni jambo la tija sana.
Usipokuwa na afya njema mara nyingi utatumia muda mrefu kuboresha afya yako kuliko kufanyia kazi zako.
Ndoto huhitaji mtu mwenye afya iliyotengamaa kwa sababu anapokuwa na ndoto hupitia katika vipindi mbalimbali ambavyo vinahitaji ukomavu wa mwili na akili.
Kichwa chako pia kinahitaji kuwa na afya bora. Kila kazi inahitaji mtu anayeweza kufikiri kwa viwango vya juu. Wale wanaofikiria zaidi ndiyo wanaopata ushindi. Mwana masumbwi maarufu duniani, Muhammad Ali, raia wa Marekani, aliwahi kusema wakati fulani kuwa bondia anaweza kuwa na mwili mdogo na bado akamshinda bondia mwenye mwili mkubwa na uzito mkubwa. Bodia lazima ajue ni wapi pa kumchapa bondia mwenzake.
Muda mwingine unapofanya kazi zako jiulize unaipa asilimia ngapi ya kufikiri. Kichwa kinachofikiri vyema na kutoa matokeochanya lazima kilishwe chakula bora. Unachokiingiza kichwa kila siku ndicho kinachotoa matokeo unayoyaonyesha. Kimuingiacho mtu ndani yake ndicho kimtokacho. Huwezi kula vitu vichafu na kutarajia tumbo lisiume. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kichwa. Ukiingiza uchafu, lazima utoe uchafu. Kama ni mtu anaongea, utasikia watu wanasema huyu anaongea nini mbona haeleweki? Au anaongea ‘pumba’.
Watu wanaosoma masomo ya kompyuta wanao msemo usemao,“Garbage In, Garbage Out,”- GIGO - yaani uchafu unaouingiza ndiyo utakaoutoa. Ukikosea kuingiza programu kwenye kompyuta lazima ikuletee matokeo usiyoyatarajia.
Kichwa kinachooingiza mambo hasi, kila siku kitaona mambo hasi hata kama mengine yatakuwa chanya. Ni jambo la muhimu kujiuliza unasoma nini, unasikiliza nini, na unatizama nini ambavyo vinakufanya uwe mtu wa kufikiri. Je, afya ya ubongo wako inakua au inadumaa?
Profesa mmoja aliingia darasani na kuweka alama ya nukta katikati ya ubao, kisha akawauliza wanafunzi, “Mnaona nini?” wakajibu, “Tunaona nukta.” Wanafunzi hao hawakuona sehemu kubwa ya ubao nyeusi, bali waliona ki-nukta kidogo cheupe kilichoandikwa kwa chaki. Uwezo wako wa kufikiri na kutazama mambo kwa sura mpya kutategemea akili yako imekomaa kiasi gani.
Jiulize mwezi huu umejifunza mambo mangapi zaidi ya mwezi uliopita. Je, mambo mangapi umejifunza mwaka huu zaidi ya mwaka jana? Kama mwaka jana umejifunza mambo mengi zaidi ya mwaka huu kaa chini jitafakari maana unarudi nyuma –husongi mbele.
Maisha ni shule. Jifunze kila siku. Jifunze kila uchao. Hata kamaunajua mambo mangapi, umesoma kiasi gani bado unahitaji kujifunza. Kuna mambo unahitaji kujifunza ambayo huyajui, kuna mambo unayajua, lakini unatakiwa kuyafuta (toa kichwani), lakini pia kuna mambo unahitaji kurudia kujifunza. Kila siku jiulize, “Leo nimejifunza nini?”
Unapokuwa na ndoto jitahidi muda mrefu mwili wako uwe imara na katika afya njema. Kuna mambo ambayo huchangia katika kusababisha ubovu wa afya. Miongoni mwayo ni tabia zetu za ulaji. Ukila bila kufuata utaratibu mara nyingi utaishiakupata unene usiokuwa wa kawaida.
Jitahidi kuwa mtu wa kufanya mazoezi kila mara ili kuuweka mwili wako sawa. Siku hizi ukichunguza watu \wengi wanafanya mazoezi ili wapunguze vitambi, lakini watu hao wangeanza mazoezi mapema hali hizo zisingewakuta.
Ukiwa kijana epuka mambo ambayo yanaweza kuhatarisha afya yako. Ni jambo la kusikitisha unapowaona vijana wadogo kabisawametumbukiwa kwenye matumizi ya mihadarati. Inasikitisha na kuhuzunisha. Watu hawa wamepoteza ndoto zao.
Napoleon Hill katika kitabu chake kiitwacho Think and Grow Rich, anasema watu wengi hawafanikiwi kabla ya miaka 40 kwakuendekeza mambo mawili - wanawake na pombe. Siku hizi hata jinsi ya kike tunaweza kusema- kuendekeza wanaume.
Pamoja na mambo hayo kusababisha mtu asifanikiwe mapema, lakini pia yamewafanya watu wengi kupata magonjwa yaliyosababisha ndoto zao zizimike kama mshumaa.
Ni jambo jema kutofautisha kati ya kuufurahia ujana wako na kuharibu kesho yako. Achana na maneno ya vijana mtaani wanaosema, “Maisha yenyewe mafupi, tunakula ujana.” Ukijidai kula ujana, kumbuka uzee utakumeza.
Kaa chini leo na jitafakari ni tabia zipi ambazo zinaiweka afya yako shakani. Ukiilinda afya yako umeilinda ndoto yako.