Serikali ya Marekani imempiga marufuku aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Uganda, Jenerali Kale Kayihura, pamoja na familia yake kuingia Marekani.
Marekani ilisema ina taarifa za kuaminika kwamba Kayihura, ambaye alikuwa mkuu wa Polisi wa Uganda kati ya mwaka 2005 na 2018, alihusika katika ukandamizaji wa haki za binadamu.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, inasema Jenerali Kayihura alihusika moja kwa moja katika kuwatesa watu, kufanya ukatili dhidi ya raia wa Uganda, kwa kuunda kikosi maalumu katika Jeshi la Polisi kilichopata amri ya moja kwa moja kutoka kwake na kuwadhulumu raia wa Uganda wakati wa uongozi wake.
Kulingana na sheria za kimataifa za Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inapokuwa na taarifa za kuaminika kuwahusu maofisa katika serikali za nje wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi au ukandamizaji wa haki za binadamu, maofisa hao na watu wa familia zao wanapigwa marufuku kuingia Marekani.
Mke wa Kale Kayihura, Angela Umurisa Gabuka, binti wake, Tesi Uwibambe, na mtoto wake wa kiume, Kale Rudahigwa, nao pia wamepigwa marufuku kuingia Marekani.
Serikali ya Marekani imesema hatua dhidi ya Kayihura inatokana na wasiwasi wa kuendelea kwa ukandamizaji wa haki za binadamu nchini Uganda na kuitaka serikali ya Yoweri Museveni kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa raia wake na kuwapa uhuru wa kuandaa mikutano ya umma kwa njia ya amani.