Ukibadili maana ya maisha unabadili maisha yako
Maana ya maisha ni mtihani. Ukiyapa maisha maana ya kuishi, utabadili maisha yako. Maisha ni kuishi. “Tunaishi mara moja, lakini mara moja ukiitendea haki inatosha,” alisema Joe E. Lewis.
“Ukitaka kuaga dunia ukiwa na furaha jifunze kuishi; ukitaka kufa kwa furaha, jifunze kufa,” alisema Celio Calcagnini. Watu wengi wanasahau kuishi kwa maana ya kuifurahia leo.
Kuna aliyesema: “Nilifia kumaliza masomo ya sekondari na kujiunga na chuo, baadaye nilifia kumaliza chuo na kuanza kazi. Baadaye nilifia kuoa na kuwa na watoto. Baadaye nilifia watoto wangu kukua na kuweza kujiunga na shule ili niweze kurudi kufanya kazi ya kuajiriwa. Baada ya kuajiriwa nilifia kustaafu. Sasa niko kufani…na ghafla nimegundua nilisahau kuishi.”
Kila mara kuna watu ambao wanataka kuishi kesho wanashindwa kuifurahia leo. “Ishi kujifunza na utajifunza kuishi.” (Methali ya Ureno).
Maisha ukiyapa maana ya kuwa ni mafupi, utabadili maisha yako. “Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima.” (Zaburi 90:12). John Johnston akionyesha ufupi wa maisha alikuwa na haya ya kusema: “Kwa wastani mtu anaishi miaka 74.
Ni karibu miezi 888, wiki 3,848, siku 27,010, saa 648,240, dakika 38,894,400 na mapigo ya moyo 2,022,508,800.” Tukumbuke wastani wa miaka ya kuishi unategemea unaishi nchi gani. Ukijua kuwa mambo ni mengi, muda ni mfupi, utabadili maisha yako.
“Maisha ni mafupi na hatuwi kamwe na muda wa kutosha kuwafurahisha wale ambao tunasafiri nao njiani. Ee, uwe mwepesi wa kupenda! Uwe mwepesi wa kuwa mkarimu,” alisema Henri Frederic.
Kama umekuwa ukitenda kana kwamba una miaka elfu ya kuishi, ukiyapa maisha maana ya kuwa ni mafupi, unakuwa na hekima. Mtazamo huo utabadili maisha yako.
Ukiyapa maisha maana ya mshumaa, utabadili maisha yako. “Maisha ni mshumaa uso mkesha.” Ni methali ya Kiswahili, maana yake kama mshumaa ulivyo maisha hayadumu. Mshumaa haupotezi mwanga wake kwa kuwasha mishumaa mingine.
Haupotezi chochote kwa kuwasaidia wengine wang’ae. Mshumaa unaowaka unafukuza giza. Giza halifukuzi giza, mwanga ndio unafukuza giza. Tusi halifukuzi tusi. Upendo unafukuza tusi. Uhasama haufukuzi uhasama, bali msamaha unafukuza uhasama.
Ukiyapa maisha maana ya leo, utabadili maisha yako. “Leo ni siku ya mwerevu, kesho mpumbavu.” (Methali ya Kiswahili). Usiahirishe hadi kesho jambo ambalo unaweza kulifanya leo.
“Leo ni kabla ya kesho.” (Methali ya Kiswahili). Tunayoweza kuyafanya sasa tuyafanye. Mwanasaikolojia William Moulton Marston aliwahoji watu elfu tatu akiwauliza: “Unaishi kwa ajili ya nini?”
Alishtuka kugundua kuwa asilimia 94 ya watu walikuwa wanaivumilia leo wakiingojea kesho; wakingojea kitu fulani kitokee; wakingojea watoto wakue na kuacha nyumbani; wakingojea mwaka ujao; wakingojea muda ujao kutimiza ndoto yao ya kusafiri; wakingojea mtu fulani kuaga dunia; wakingojea kesho bila kutambua kuwa kila mtu alichonacho ni leo kwa sababu jana imeondoka na kesho haiji,” alisema Douglas Lurton.
Maisha yamepewa maana mbalimbali. Papa Fransisko amesema: “Maisha ni safari, tunaposimama mambo hayaendi sawa.” Methali ya Kiswahili inasema: “Maisha ni karata.” Kwa maana ya maisha ni kupata au kukosa. Katika kuishi mtu anaweza kufanikiwa au asifanikiwe. Yape maisha maana nzuri.
Maisha ni wimbo, uimbe. Maisha ni fursa, itumie. Maisha ni fumbo, lifumbue. Maisha ni lengo, litimize. Maisha ni kitendawili, kitegue. Maisha ni fumbo, lifumbue. Maisha ni mchezo, ucheze. Maisha ni vita, pigana vita vizuri. Maisha ni kuanza jambo jipya, lakini usisahau kuishi.