Hiki ni kitabu ambacho kimesheheni matumaini, motisha pamoja na hamasa kwa vijana ambao waliona uthubutu katika maisha yao. Mwandishi ameamua kufikisha ujumbe kwa vijana ili kuwapa moyo na faraja, pia kitabu hiki kimezungumzia maisha halisi ya mwandishi wa kitabu hiki. Fuatilia hadithi hii hadi mwisho…

Ni asubuhi yenye kupendeza, jua likiwa limechomoza kuashiria siku nyingine imewadia. Noel alikuwa amebeba begi lake mgongoni akielekea shuleni, lakini alionekana kuwa mtu mwenye mawazo mengi sana, nyuma yake mzee mmoja alikuwa anakuja akiendesha baiskeli akipiga mluzi.

Kwa bahati mbaya alikuwa anapita karibu zaidi na upande aliokuwepo Noel, akamkwaruza na baiskeri yake mguuni. Noel hakuongea chochote, alikaa kimya: “Kijana samahani,’’ alisema yule mzee huku akishuka taratibu kutoka kwenye baiskeli yake: “Bila samahani mzee wangu,’’ alisema Noel, akiendelea kutembea huku akichechemea kidogo, kwa kuwa alipata maumivu ya wastani.

Yule mzee alipomwangalia usoni, aligundua kuwa ni mtu mwenye msongo wa mawazo. ’’Lakini mbona una mawazo sana kijana wangu?’’ aliuliza yule mzee, lakini Noel akawa mzito kidogo kuongea.

“Hamna mzee,’’ aliongea akionyesha uso wa tabasamu kijana Noel: “Punguza mawazo, mawazo ya nini wewe ungali kijana mdogo!’’ alisema yule mzee mwenye baiskeli kisha aliondoka na kumuacha Noel akiwa amesimama njiani.

Noel alikuwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Mwanza, alitokea katika familia ya watu wa maisha ya chini.

Mama yake alikuwa anauza pombe za kienyeji na baba yake alikuwa amewatelekeza tangu walipokuwa wangali watoto wadogo. “Maisha haya najua ipo siku nitaondokana nayo,’’ aliwaza akilini mwake kisha akaondoka na kuelekea darasani. Noel alikuwa na ndoto kubwa katika mpangilio wa maisha yake, mara nyingi aliwaza ipo siku moja atakuja kuwa mwandishi mzuri wa vitabu.

Lakini pia alipenda kutoka katika maisha ya umaskini. “Noeli’’ alimuita msichana mmoja aliyekuwa anasoma naye. Aligeuka na kuitikia kwa upole: “Naam!’’ huku akiwa bado angali amegeuza shingo yake kumtazama yule msichana.

Yule binti naye alikuwa amevaa sare nzuri za shule, daftari zake zilikuwa nadhifu, alikuwa ameziweka katika mafaili aliyokuwa ameyashika mkononi. “Duuuh! Leo tumechelewa,’’ alisema yule binti.

“Siku huwa hazilingani,’’ alisema Noel kwa utaratibu huku wakitembea mwendo sanjari na yule binti. “Kazi ya mwalimu ulifanya?’’ aliuliza yule binti. “Mimi natamani tu kumaliza shule,’’ alisema Noel akiwa amekata tamaa ya maisha ya nyumbani kwao ya kuuza pombe ya kienyeji.

Nyumbani kwao hali ya biashara hiyo ilikuwa mbaya sana kutokana na polisi kumsumbua mama yake kila siku, polisi walikuwa hawaishi kufika nyumbani kwao.

“Sijaifanya kazi yake,’’ alisema Noel. “Mwalimu atakufukuza kwenye kipindi chake,’’ aliongea yule binti akimsikitia Noel.

“Baadae nitaifanya,’’ alisema Noel. Uwezo wa masomo ya darasani alikuwa nao mkubwa lakini tatizo ni umaskini uliokuwa umekithiri, ulimuathiri kisaikolojia. Noel kila siku jua linapozama na kuchomoza alikuwa akiwaza atafanya nini ili aweze kulipa deni alilokuwa anadaiwa shuleni.

“Dah! Maisha magumu,’’ aliongea huku akishusha pumzi yake kwa nguvu. Kila ngazi ya elimu aliyokuwa akipitia alikutana changamoto nyingi sana.

Walianza kuingia katika eneo la shule, kwa mbali walianza kuona walimu wakiwa wamesimama na mhasibu wa shule. Pamoja na kuwa mbali, lakini walimu walikuwa wameshamuona Noel. “Hivi huyu kijana amegoma kutoa pesa?’’ aliuliza mwalimu mmoja. “Sijui, naona yuko kimya,’’ waliendelea kumjadili Noel.

Kila siku Noel alikuwa anaitwa ofisini kwa mhasibu, kusoma kwake kulikuwa kwa shaka, hakuwa na furaha. Aliishi kwa wasiwasi muda wote alipokuwa shuleni. “Nitafanyaje, nitafanyaje?’’ ndilo lilikuwa swali lake kila mara kijana Noel. Alipokuwa akitembea kuelekea shuleni alifika sehemu yenye uwazi ambapo walionekana walimu wake wakamuita kwa sauti: “Noeli?’’