Bila shaka sisi sote tunajua kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki unaojumuisha nchi tano za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Watu husema ‘umoja ni nguvu’ kwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni umoja, basi watu wanalazimika kumshangaa mtu anayewahimiza wenzake wajitoe kwenye umoja. Ni kweli umoja ni nguvu. Lakini inategemea unafanya umoja na mtu wa aina gani. Hii ni kusema kwamba wakati mwingine umoja ni udhaifu na unaweza kumletea mtu madhara makubwa.

Kwa jumla ya nchi nyingine zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ni majirani wa Tanzania. Ukitaka kusema kweli utakubali kwamba nchi hizo si majirani wazuri wa Tanzania. Majirani wazuri wa Tanzania wako kusini mwa Afrika — nchi zinazounda Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki hazina malengo mazuri na Tanzania. Kwa mfano, Kenya haijaficha malengo yake mabaya kwa Tanzania. Ni majuzi tu baadhi ya magazeti ya Tanzania yalipoandika kwamba Serikali ya Kenya inajipanga kuipokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba na kukihamishia Kenya. Kwa vyovyote, Kenya ikitimiza lengo lake hilo itakuwa imevuruga amani na utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Unaweza ukasema kwamba tayari Kenya imetangaza vita dhidi ya Tanzania.

Mambo yako hivi, Serikali ya Somalia imefungua kesi katika Mahakama ya Sheria ya Kimataifa (ICJ) ya kutaka kuchorwa upya kwa mpaka wake na Kenya. Serikali ya Somalia inadai kuwa eneo lote la Ukanda wa Pwani wa Kenya ni lake. Hii ina maana kwamba madai hayo ya Somalia yakipita, basi mpaka wa bahari katika Bahari ya Hindi utatanda hadi pwani ya Tanzania.

Ikitokea hivyo, Kenya itakuwa imepoteza eneo lote la bahari, kwa hiyo itafidia hasara itakayopata kwa kunyang’anywa ukanda wake wa pwani na Somalia kwa kupokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba.

Tuanzie hapo. Tujiulize swali; mtu mmoja ana mgogoro wa shamba na mtu mwingine, katikati ya mgogoro mtu huyo anatangaza akinyang’anywa eneo la shamba lake na mtu mwenye mgogoro naye atachukua eneo la shamba la mtu ambaye hahusiki na mgogoro huo. Hiyo si dharau na uchokozi wa wazi tu wa Kenya kwa Tanzania, bali pia unaoendelea ni ushahidi kuthibitisha kwamba Kenya si jirani mzuri wa Tanzania.

Haiingii akilini Kenya inyang’anywe eneo lake na Somalia kisha ilipe kisasi kwa kuinyang’anya Tanzania eneo lake. Kwamba Kenya imepanga kuipokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba si jambo la uzushi. Ni kauli iliyotolewa hadharani na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Kenya, Karanja Kibicho. Kwa vyovyote Katibu Mkuu wa Serikali ya Kenya hawezi kukurupuka kutoa kauli kama hiyo. Hapana shaka uamuzi wa kuipokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba umepitishwa na Baraza la Mawaziri la Kenya chini ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, Rais Uhuru Kenyatta.

Ni katika mazingira hayo Tanzania ina kila sababu ya kulichukulia suala hilo nyeti kwa uzito wake. Tena kwa wazi kama Kenya ilivyotoa kauli yake kwa wazi. Tusije tukasahau kabla ya Vita ya Kagera ya mwaka 1978 hadi 1979, kilichotangulia ni kauli ya Uganda kwamba ingeipokonya Tanzania eneo la Kagera. Uganda ikatimiza lengo lake Oktoba 30,1978.

Kenya haijasema kama itaipokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba kwa kuwa labda huko nyuma Pemba ilikuwa sehemu ya Kenya. Na ukweli ni kwamba Pemba haijapata kuwa sehemu ya Kenya. Lakini kisiwa cha Witu kilichopo Kenya enzi za utawala wa Kijerumani kilikuwa sehemu ya Tanganyika. Witu iliendelea kuwa sehemu ya Tanganyika mpaka mwaka 1890 Mkataba wa Heligoland wa Ujerumani na Waingereza walipoweka Kisiwa cha Witu chini ya Waingereza.

Tanzania ilikuwa na haki ya kudai kuipokonya Kenya kisiwa chake cha Witu. Lakini Tanzania ni kisiwa cha amani kisichotaka kuvuruga ujirani wake na Kenya. Katika mazingira hayo, basi kama Kenya ingekuwa na nia njema kwa Tanzania isingetangaza sasa nia yake ya kutaka kuchukua Kisiwa cha Pemba. Ingesubiri imalizike kesi yake na Somalia.

Kama Kenya ingekuwa haina eneo la bahari, basi ingeiomba Tanzania tena kwa heshima kutumia eneo la pwani ya Tanzania. Lakini haikusubiri kitu imetangaza moja kwa moja kwamba eneo lake likichukuliwa na Somalia italipa kisasi kwa kuchukua eneo la Tanzania! Ni katika hali hii Tanzania ina kila sababu ya kujitoa sasa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania ikichukua hatua hiyo haitapoteza chochote bali italinda heshima yake na itakuwa imeondokana na majirani wachokozi na waliojaa hila na dharau. Kwa hivyo basi, huu si wakati wa Tanzania kukaa kimya na kuendelea kuivumilia Kenya ambayo uhusiano wake na Tanzania hauna historia nzuri. Hebu tujikumbushe angalau kwa ufupi historia ya uhusiano wa Kenya na Tanzania.

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Tanganyika ilipokuwa inakaribia kupata uhuru, iliutangazia ulimwengu kwamba ipo tayari kuchelewesha uhuru wake ili nchi zote za Afrika Mashariki zipate uhuru wakati mmoja kisha ziunde Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa bahati nzuri Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 ikiwa nchi ya kwanza kupata uhuru Afrika Mashariki, nayo Uganda ikapata uhuru mwaka 1962.

Japokuwa Tanganyika na Uganda zilikuwa zimepata uhuru, Rais Julius Nyerere wa Tanganyika na Waziri Mkuu Milton Obote wa Uganda, waliendeleza mazungumzo ya shirikisho na Jomo Kenyatta wa Kenya. Tanganyika na Uganda zikafanya juhudi kubwa kuhimiza Uingereza itoe uhuru wa Kenya ili shirikisho liweze kuanzishwa. Lakini Kenya ilipopata uhuru mwaka 1963 haikuwa na haja tena na shirikisho.

Julius Nyerere aliyekuwa na nia njema kabisa katika kuanzisha shirikisho akajihisi kuwa amegeuzwa mjinga. Ndipo akaamua kuanzisha muungano na Zanzibar na Abeid Karume. Shirikisho lilishindikana kuanzishwa na badala yake ilianzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967 ikavunjika mwaka 1977. Japokuwa kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kulisababishwa na uhusiano wa Tanzania na Uganda. Kenya ilichukua nafasi hiyo kuleta hali mbaya zaidi kati yake na Tanzania.

Chukua, kwa mfano, tukio baya la 1977 Tanzania ilikuwa inajiandaa kwa sherehe za kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 5, 1977. Sherehe hizo zilipangwa kufanyika Zanzibar. Lakini wageni wengi walialikwa kwenye sherehe hizo walikwamishwa Kenya kwa makusudi kabisa baada ya Kenya kuzuia ndege za Jumuiya kutumiwa na abiria waliokuwa wakienda katika sherehe hizo. Ilitokea wakati ule nikiwa Nairobi.

Nilikuwa nimejiandaa kurejea nyumbani kwa ndege lakini nilikwama. Nikasafiri baadaye kwa gari. Lakini wageni waliokuwa wakienda Zanzibar walikwamishwa kabisa na Kenya. Hawakufika kabisa Zanzibar. Je, jirani anayevuruga shughuli zako utasema ni jirani mzuri? Tukirudi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuanzishwa upya mwaka 2000 kukaja wazo la kuanzishwa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Japokuwa huko nyuma katika miaka  ile ya 1960 Kenya haikutaka shirikisho, leo inataka shirikisho lianzishwe moja kwa moja bila kupoteza wakati. Na inafanya kila kitu katika kuilazimisha Tanzania ikubali shirikisho. Kwa nini?

Hilo ni suala ambalo viongozi wa Tanzania na wala si wananchi tu wanaopaswa kulitafutia jibu tena kwa umakini na wanalijua. Kenya haipiganii lianzishe shirikisho sasa kwa sababu eti inataka ushirikiano wa kweli na Tanzania. Inataka ardhi ya Tanzania.

Si kweli kwamba Kenya inaipenda Tanzania au inawapenda Watanzania ambao wakati wote inawaona ni wajinga. Kenya inanyemelea ardhi ya Tanzania. Kwamba Kenya inataka ardhi ya Tanzania si jambo geni. Ni suala lenye historia ndefu. Mwaka 1926 magavana wa Kenya, Uganda na Tanzania walianzisha mikutano ya kila mwaka Nairobi, Kenya. Tanganyika iliwakilishwa na Donald Cameron, Gavana wa pili wa Tanganyika.

Wakati mikutano hiyo ya Kenya mkoloni alikuwa na wazo la kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Wakati ule sehemu kubwa ya ardhi ya Kenya ilikuwa imechukuliwa na Wazungu tangu enzi za Lord Delamere. Kwa hiyo, Wazungu wa Kenya walitaka kujipanua mpaka Tanganyika ili wachukue ardhi ya Tanganyika. Donald Cameron aliliona hilo. Akapinga kwa nguvu zake zote wazo hilo la kuanzishwa kwa shirikisho hilo. Akaiepusha Tanganyika kuporwa ardhi yake.

Desemba 20, 1956, Rais wa TANU, Julius Nyerere, alipohutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, alimsifu sana Donald Cameron. Alimtaja Cameron kuwa gavana pekee wa Tanganyika aliyewafikiria sana Waafrika wa Tanganyika hata akawaepusha katika matatizo ambayo yangewapata kama lingeanzishwa Shirikisho la Afrika Mashariki ambalo Tanzania leo inataka kushiriki katika kulianzisha. Ole wake Tanzania ikiwa sehemu ya Shirikisho la Afrika Mashariki.

Makala hii itaendelea katika toleo lijalo. Usikose nakala yako ili kujua sababu zinazohalalisha Tanzania kuondokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.