Siku chache baada ya Jeshi la Polisi nchini kukutana na wadau wa habari na kuwataka waripoti habari zinazozingatia amani na usalama wa nchi pamoja na kuwafanya raia wawe na imani na jeshi hilo, baadhi ya polisi wamekuwa vinara wa kuendeleza vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa raia, huku mara kwa mara wakitumia nguvu kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Moja ya matukio ya kustaajabisha ya jeshi hilo ni kwa ofisa wa polisi kunyanyasa, kudhalilisha na kumshushia kipigo, Salma Juma, mkazi wa Kinondoni kwa kile kinachodaiwa kuegesha gari karibu na Kituo Kidogo cha Polisi Hananasif bila idhini ya jeshi hilo.
Akizungumza na JAMHURI, Salma alisema: “Siku ya Jumanne (Septemba 16) usiku nikiwa na mgeni wangu tukitoka kwenye mizunguko yetu, tuliegesha gari karibu na kituo hicho tukiamini kuwa ni salama kwetu.
“Hatua chache baada ya kuondoka katika eneo hilo tuliona askari aliyevaa sare za Jeshi la Polisi akitufuata huku akifoka na kutuamuru tutoe gari katika eneo hilo,” alisema Salma.
“Tulijieleza kuwa sisi ni wenyeji wa eneo hilo na zaidi ni kwamba kwetu gari hazifiki. Hata hivyo, askari hakutuelewa na kuanza kutuamuru kuondoa gari katika eneo lile. Mwenzangu alirejea garini na kuondoka katika eneo hilo,” alieleza Salima.
“Mimi niliyebaki katika eneo hilo akanishushia kipigo. Kipigo hicho kimenisababishia maumivu, vidonda, uvimbe na kuharibikiwa kwa simu yangu ya mkononi. Nilijaribu kupiga kelele ili nipate msaada lakini hakuna aliyejitokeza kunisaidia,” anasema Salima.
Salma alisema kuwa ametoa taarifa Kituo cha Polisi Oysterbay na kufungua jalada la uchunguzi namba DSM/KIN/CID/PE/171/2014 na kupatiwa PF3 ambapo amepatiwa matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala.
Gazeti hili limeshuhudiwa PF3, vidonda na uvimbe mwilini mwa dada huyo, vilivyotokana na kipigo kilichotoka kwa polisi.
Gazeti hili lililazimika kufika katika Kituo Kidogo cha Polisi Hananasif. Askari waliokuwapo kituoni hapo walikiri kufahamu kutokea kwa tukio hilo, lakini hata hivyo, hawakukubali kutoa namba wala jina la askari huyo zaidi ya kukubali simu ya mmoja wao itumike kuzungumza na askari huyo aliyetenda tukio hilo.
Askari huyo alipohojiwa na JAMHURI, alisema “Hata yeye amenipiga, ameniuma na kunikunja. Na siku hiyo nilikuwa na askari wa ulinzi shirikishi.
“Waliegesha gari bila ya hata salamu na kuondoka. Achana na kutokuomba uangalizi wa gari lao. Nilipowafuata na kuwaamuru waondoe gari, mwanaume alitii amri na kuondoa gari karibu na kituo. Mwanamke alinitolea neno chafu la mauzi (limehifadhiwa),” anasema askari huyo.
Gazeti hili lilipomhoji kuhusiana na kuchukua hatua mikononi kwa kumpa kipigo kilichomuathiri, kumdhalilisha na kusababisha dada huyo kufungua jalada kituo cha polisi Oysterbay, askari huyo alisema; “Hata mimi amenikunja, amenipiga na kuning’ata. Nimefungua jalada, ukitaka kuthibitisha nenda kwa Mkuu wa Kituo Oysterbay atakuthibitishia.”
JAMHURI limeelezwa na baadhi ya watu waishio karibu na kituo hicho kuwa hata mwezi uliopita kuna mtu alipigwa na askari hao na kusukumwa mtaroni.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya kusikitisha yanayofanywa na askari polisi nchini yanayonyanyasa raia huku yakiwaacha baadhi ya wananchi kutokuwa na imani na jeshi hilo.
Baadhi ya matukio ni pamoja na utekelezaji wa majukumu ya askari wa Usalama Barabarani ambao umegubikwa na uonevu na rushwa. Askari wa Usalama wa Raia nao wanadaiwa kutumia nguvu nyingi hata pale zisipohitajika na kusababisha athari kwa raia na mali zao.
Moja ya matukio hayo ni tukio la hivi karibuni ambalo askari polisi waliwapiga waandishi wa habari waliofika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kutafuta habari, siku ambayo uongozi wa jeshi hilo ulipokutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kwa mahojiano.