Imeelezwa kuwa Tanzania imeshika nafasi ya kwanza katika nchi zinazovutia uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki. Kadhalika Tanzania inashika nafasi ya tisa barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Australia kwa nchi za Afrika Mashariki, Geoff Tooth, wakati akihitimisha Maonesho ya Kimataifa ya Madini yaliyofanyika Perth, Australia.
Maonesho hayo yanafahamika kwa jina la Africa Down Under (ADUC) ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa fursa kwa nchi za Kiafrika zenye utajiri wa madini ikiwamo Tanzania, kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini ili kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Balozi Tooth alitumia fursa hiyo kuiasa Tanzania kuendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji nchini, kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwamo kuwa na miundombinu madhubuti ya barabara, bandari, reli, kuboresha upatikanaji wa umeme na kuwa na sera na sheria zisizobadilika mara kwa mara.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo ya siku tatu yaliyoshirikisha nchi mbalimbali duniani, Kamishna wa Madini, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja, ameeleza kuwa Tanzania ilipata upendeleo wa kipekee katika Maonesho hayo kwani Septemba 4, mwaka huu, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, alipata nafasi ya kutoa mada mahsusi kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini hapa nchini.
Aliongeza kuwa Septemba 5, mwaka huu, Tanzania ilipangiwa muda maalum wa kueleza kwa undani kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini (Tanzania Investment Forum), pamoja na kukutana ana kwa ana na wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini.
“Kupitia fursa hiyo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, ulipata fursa ya kueleza masuala mbalimbali ikiwamo historia ya Tanzania, maendeleo ya sekta ya madini, vivutio mbalimbali vya uwekezaji, pamoja na miradi ambayo inaweza kuendelezwa kwa ubia kati ya wawekezaji hao na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),” alisema Kamishna.
Mbali na kupata muda maalum wa kutoa mada katika mikutano iliyokuwa ikienda sambamba na Maonesho hayo, Kamishna wa Madini ameeleza kuwa wataalamu katika banda la Tanzania, walikuwa wakitoa elimu na taarifa mbalimbali ikiwamo sera ya madini ya mwaka 2009, sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo, madini yapatikanayo Tanzania, tafiti za kijiolojia na mashapo yaliyopo Tanzania, pamoja na huduma za kijiolojia zinazotolewa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
“Wataalamu wetu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, GST, Stamico, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) pia walikuwa wakitangaza miradi ambayo Stamico inahitaji wawekezaji wenza, walitangaza shughuli za maabara ya kisasa ya TMAA, taarifa mpya za kijiolojia zilizokusanywa na GST, walikutana ana kwa ana na wawekezaji kwa maana ya kupata ufahamu zaidi kuhusu masoko na mitaji. Vilevile walipata fursa ya kujifunza jinsi nchi nyingine za Kiafrika zinavyosimamia sekta ya madini,” alisisitiza Mhandisi Masanja.
Maonesho hayo ya Kimataifa ya ADUC yaliyoanzishwa rasmi mwaka 2003 yalikutanisha washiriki zaidi ya 2,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri wa Madini kutoka baadhi ya nchi za Kiafrika na Australia, maafisa waandamizi wa madini wa nchi hizo, wataalamu kutoka taasisi za fedha duniani, wawekezaji, na watoa huduma kwenye sekta ya madini.
Pamoja na Tanzania, nchi nyingine zilizoshiriki Maonesho hayo ni pamoja na Angola, Botswana, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Uganda, Comoro na Ivory Coast.
Nchi nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea-Conakry, Kenya, Lesotho, Malawi, Madagascar, Msumbiji, Namibia, Niger, Nigeria, Rwanda, Jamhuri ya Afrika Kusini, na Zimbabwe.