“Natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi ambayo ni maskini…Nimeongoza nchi maskini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri” yalikuwa ni maneno ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa Agosti 5, 2014 alipozungumza kwenye Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo mjini Washington, D.C., Marekani.

Rais Kikwete alisema maneno hayo akiwa kwenye ziara ya siku tisa nchini Marekani alipozungumzia hali ya baadaye ya Tanzania kufuatia ugunduzi wa gesi asili. Tanzania inatarajiwa kuanza kupokea mapato yake ya kwanza kutokana na rasilimali ya gesi asili katika miaka sita ijayo, kuanzia mwaka 2020.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete pia alipata fursa ya kuhudhuria mkutano wa kwanza wa viongozi wa Marekani na Afrika ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani, mapema mwezi uliopita.

Matumaini ya Rais Kikwete yanatokana na ugunduzi mkubwa wa gesi asili uliofanyika kwenye eneo la kina kirefu baharini, kuanzia mwaka 2010, ugunduzi ambao hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa za Serikali, umefikia futi za ujazo trilioni 51.

Utajiri wa Taifa letu kwa sasa unakisiwa kuwa dola za Marekani bilioni 28. Hivyo, kwa vile thamani ya gesi asili iliyogunduliwa hadi sasa (tcf 51) inakisiwa kuwa dola za Marekani bilioni 700, kiasi hiki ni kikubwa zaidi ya mara 15 hadi 25 ya uchumi wetu wa sasa.

Hii ni neema kubwa sana kwa Taifa letu na ni mwarobaini kwa umaskini wa Tanzania endapo tutaendelea kuwa na uongozi bora, imara, mipango madhubuti na usimamizi mzuri wa neema hiyo. Baadhi ya faida za gesi asili ni pamoja na zifuatazo: kwanza, ni chanzo cha umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

Inasadikika kwamba mara mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar utakapokamilika mwaka kesho, gharama za watumiaji wa umeme zitashuka kwa takribani asilimia 50 ya gharama za sasa. Pili, upatikanaji wa gesi asili kwa wingi utavutia wawekezaji katika viwanda mbalimbali ikiwamo viwanda vya mbolea. Viwanda vya mbolea vitawahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea ya uhakika na kwa bei nafuu kuliko ilivyo sasa, jambo  litakalosaidia sana kuboresha sekta ya kilimo hapa nchini.

Kuimarika kwa sekta ya kilimo nchini kutaleta matokeo chanya kwa uchumi wa Taifa kwa sababu sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu hasa ikizingatiwa kwamba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea sekta hii ya kilimo kwa sasa.

Tatu, upatikanaji wa gesi asili utasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ugunduzi wa gesi nyingi umesababisha mipango ya ujenzi wa zaidi ya viwanda 50 mbalimbali vilivyoibuliwa hivi karibuni katika mikoa ya Lindi na Mtwara kufuatia ugunduzi huo mkubwa wa gesi asili. Viwanda hivyo vitatoa ajira kwa maelfu ya Watanzania.

Nne, upatikanaji wa gesi asili ya uhakika utaongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Tanesco na wadau mbalimbali wa maendeleo. Tano, gesi asili ikichakatwa itasaidia kupatikana kwa gesi ya kupikia, tena kwa bei nafuu, hivyo kuokoa kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti inayotumika kama nishati ya kupikia (kuni).

Sita, ugunduzi wa gesi asili kwa wingi umevutia zaidi wawekezaji katika sekta ndogo ya uzalishaji saruji. Kwa mfano, hivi sasa kampuni ya Dangote Group inayomilikiwa na tajiri namba moja barani Afrika, Alhaj Aliko Dangote, inaendelea na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha saruji huko Mtwara.

Kiwanda hiki kinatarajiwa kuanza kuzalisha saruji ifikapo Juni 2015. Saruji hiyo inatarajiwa kuuzwa kwa bei nafuu sana kwa sababu malighafi yote itapatikana hapa nchini. Upatikanaji wa saruji nyingi nchini tena kwa bei nafuu ni fursa kwa Watanzania wengi, hususani wa kipato cha chini, kumudu gharama za ujenzi wa nyumba bora na za kisasa, hivyo kuimarisha maisha yao.

Aidha, kiwanda cha saruji cha Dangote Group kinatarajiwa kuajiri wafanyakazi wa kudumu takribani 1,000, lakini pia kutakuwa na wafanyakazi wengine wa mikataba (wa kuja na kuondoka) wapatao 9,000. Kimsingi, kiwango cha gesi asili kilichogunduliwa (tcf 51) hadi sasa kinaihakikishia nchi yetu kuingia kwenye uchumi wa gesi asili, ambao ukisimamiwa vizuri utaihakikishia Tanzania kufikia Dira yake ya Maendeleo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ngeleja injini ya mafanikio ya Rais JK

Katikati ya mafanikio haya ya ugunduzi wa gesi asili kwa kiwango kikubwa kuanzia mwaka 2010 pamoja na ujenzi wa miundombinu itakayoliwezesha Taifa kunufaika vilivyo na neema ya gesi asili, tunamkuta mchapakazi William Mganga Ngeleja.

Huyu ni Mbunge wa Sengerema tangu mwaka 2005 hadi sasa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na aliyewahi kuwa Naibu baadaye Waziri wa Nishati na Madini kwa takribani miaka mitano na nusu kuanzia Januari 2007 hadi Mei, 2012 alipojiuzulu uwaziri, kufuatia kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa kulikoanzia bungeni.

Ni ukweli usiopingika kwamba mafanikio makubwa tunayoyaona sasa kwenye sekta za nishati na madini ni matokeo ya maono, mipango mizuri, na ubunifu mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kipindi ambacho Ngeleja alikuwa Waziri wa Nishati na Madini (2007-2012). Kwa mfano, utafutaji wa gesi asili na mafuta ulianza kushika kasi zaidi wakati Ngeleja akiwa waziri.

Ujenzi wa bomba la gesi Mtwara-Dar es Salaam

Jambo moja kubwa na muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu lililofanywa na Serikali ya Rais Kikwete wakati Ngeleja akiwa waziri, ni ubunifu wa mradi wa bomba la gesi asili linalojengwa kutoka Mtwara hadi Dar lenye urefu wa zaidi ya Km 500.

Ngeleja, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) mwaka 2009, walibuni mradi huu wa bomba la kusafirishia gesi asili na kuanza kuutekeleza kabla hajajiuzulu uwaziri Mei, 2012. Tunawakumbuka Ngeleja na TPDC kwa ubunifu huu kwa sababu mradi huu haukuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010, hivyo bila maono na ubunifu wao mradi huu leo usingekuwa hapa ulipofikia.

Walichofanya Ngeleja na TPDC kinafananishwa na maono na ubunifu aliofanya Rais Kikwete mara tu baada ya kuingia madarakani kwa kubuni na kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2006. Kama ilivyo kwa mradi wa bomba la gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar, ujenzi wa UDOM haukuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010.

Ujenzi wa mradi wa bomba la gesi utakapokamilika mwaka 2015, utakuwa ni mwarobaini kwa kero ya umeme ambayo imekuwa ikiligharimu Taifa trilioni za fedha za Kitanzania kila mwaka. Kama nilivyotangulia kusema, bomba la gesi litasaidia kusafirisha gesi asili yenye uwezo wa kufua umeme usiopungua megawati 3,000 kwa siku, ilhali mahitaji na matumizi ya umeme kwa siku kwa sasa hayazidi megawati 1,000. Mradi huu wa bomba la gesi asili utagharimu takribani dola za Marekani bilioni 1.23 na unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Mchuchuma-Liganga yapata mwekezaji

Mambo mengine makubwa aliyofanya Rais Kikwete na ambayo ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya Taifa letu ni pamoja na kumpata mwendelezaji wa mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Mchuchuma-Liganga, ulioko Ludewa, mkoani Njombe.

Mradi huu ambao umekuwapo kwenye makabrasha ya Serikali kwa miongo kadhaa bila kuendelezwa, hatimaye mwaka 2011 ulipata mwendelezaji — Kampuni ya Kichina iitwayo Hongda Group — kwa kushirikiana na mbia wake Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Baadhi ya manufaa ya mradi huu ni pamoja na uzalishaji wa umeme megawati 600, ajira na fedha za kigeni kutokana na mauzo ya chuma na makaa ya mawe. Uwekezaji katika mradi huu ni takribani dola za kimarekani bilioni 3.

Mpango kabambe wa umeme vijijini kupitia REA

Mpango kabambe wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ulibuniwa mwaka 2009/2010 ingawa utekelezaji wake ulianza kushika kasi mwaka 2010/2011. Mpango huu ni mojawapo ya mambo mengi makubwa na mazuri ambayo Rais Kikwete amefanya katika utawala wake. Hii ni muhimu sana kwa sababu hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea bila kuwa na nishati ya umeme ya uhakika kwa wananchi wake.

Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huu imeiwezesha Serikali kuwafikishia umeme asilimia 36 ya wananchi hadi sasa. Hii ni zaidi ya lengo lililokuwa limepangwa na Serikali la kuwafikishia umeme asilimia 30 ya wananchi ifikapo mwaka 2015, hivyo Serikali imevunja rekodi kwa kuvuka lengo ililokuwa imejiwekea kupitia REA, Tanesco na washirika wa maendeleo.

Usimamizi katika sekta ya madini waimarishwa

Itakumbukwa wakati Rais Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, Taifa lilikuwa limegubikwa na malalamiko kutoka kila kona ya nchi kwamba nchi yetu ilikuwa hainufaiki vya kutosha kutoka kwenye rasilimali zetu za madini (hususani dhahabu, almasi na tanzanite), kutokana na sera na sheria mbovu za madini pamoja na mikataba mibovu iliyokuwa inawanufaisha zaidi wawekezaji, wengi wao kutoka nje ya nchi.

Rais Kikwete alisikia kilio cha Watanzania wenzake na hivyo akaamua kuwajibu kwa kuchukua hatua zifuatazo:

Moja, mwaka 2006 Rais aliagiza mikataba yote ya madini ipitiwe upya ili kurekebisha kasoro zilizokuwa zinalalamikiwa.

Pili, mwishoni mwa mwaka 2007 Rais Kikwete aliunda Tume Maalum iliyoongozwa na Jaji Bomani ili kumshauri na kupendekeza namna bora ya kusimamia sekta ya madini. Tume hii ilikamilisha kazi na kukabidhi taarifa yake kwa Rais mwezi Mei, 2008.

Tatu, Mwaka 2008 Serikali, kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ililifufua Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). Nne, mwaka 2009 Sera mpya ya Madini ilitungwa. Tano, mwaka 2010 sheria mpya madini ilitungwa. Sita,  Novemba 2009 Serikali ilianzisha Wakala wa Ukaguzi wa Migodi ya Madini nchini (TMAA).

Pamoja na mambo mengine, hatua hizi kwa pamoja ndizo zilizoboresha usimamizi na manufaa ya sekta ya madini nchini. Baadhi ya matunda ya hatua hizi zilizochukuliwa ni kuongezeka kwa mrabaha wa dhahabu kutoka asilimia 3 hadi asilimia 4; kampuni za madini zilianza kulipa kodi ya mapato (30%) mfano Resolute (Nzega), Tulawaka (Biharamulo) na GGM (Geita).

Manufaa mengine ni ule utaratibu ambao sera na sheria mpya za madini ziliuweka unaoiruhusu Serikali kumiliki asilimia fulani ya hisa kwenye mgodi wa madini. Matokeo ya masharti hayo ya sera na sheria mpya za madini ni kwamba kwa sasa Watanzania wanamiliki asilimia 50 ya hisa za mgodi wa tanzanite ulioko Mirereni, mkoani Manyara.

Aidha, Serikali inamiliki asilimia 20 kwenye mgodi wa Mchuchuma-Liganga, nk. Ni wazi kwamba kwa hatua hizi zilizochukuliwa mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa Taifa umezidi kuimarika.

Serikali ya Rais Kikwete ilichukua hatua hizi za kuimarisha usimamizi na manufaa ya sekta ya madini wakati Wizara ya Nishati na Madini ikiongozwa na William Ngeleja, akisaidiwa na Adam Malima, Mbunge wa Mkuranga, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Fedha.

Uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Fuel bulk procurement)

Zawadi nyingine nzuri ambayo Rais Kikwete amewaletea Watanzania ni kuanzisha utaratibu wa kuagiza bidhaa ya petroli (mafuta) kwa pamoja (Fuel bulk procurement). Utaratibu huu umeisaidia sana nchi kudhibiti, kwa kiasi kikubwa, uchakachuaji wa mafuta, ukwepaji kodi na uhaba wa mafuta uliokuwa unafanywa au kusababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Fuel bulk procurement ilianzishwa mwishoni mwa mwaka 2011. Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa mapema mwaka huu kupitia Wizara ya Nishati na Madini, utaratibu huu umeisaidia nchi kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 500 za Tanzania tangu uanze kutumika. Mwanzilishi wa utaratibu huu wa fuel bulk procurement ni Ngeleja alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini, kwa kushirikiana na EWURA.

Yote kwa yote, kwa muhtasari huu huna budi kukubaliana na matumaini na ndoto za Rais Jakaya Kikwete kwamba kwa mambo ambayo ameyasimamia ni kweli kabisa kuwa yeye Rais Kikwete atakuwa Rais wa mwisho kuongoza Tanzania maskini.

Na ni kweli kwamba muhtasari wa baadhi ya mambo makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa yatakayopaisha uchumi wa nchi yetu kama vile ugunduzi wa gesi asili yenye takribani futi za ujazo trilioni 51, zenye thamani ya takribani dola za 700 bilioni za Marekani, kiasi ambacho ni kikubwa kwa zaidi ya mara 15 au 25 ya uchumi wetu kwa sasa ambao unakadiriwa kuwa dola 28 za Marekani.

Kadhalika, ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam; Uendelezaji wa mgodi wa Mchuchuma-Liganga; Mpango kabambe wa usambazaji umeme vijijini kupitia REA; Sera (2009) na sheria (2010) mpya za madini; Uagizaji wa mafuta kwa pamoja (fuel bulk procurement); Uanzishaji wa Wakala wa Ukaguzi wa Migodi ya Madini nchini (TMAA), 2009 na ufufuaji wa STAMICO mwaka 2008 — haya yatapaisha uchumi.

Watanzania wanakumbuka kwamba mambo haya makubwa na muhimu kwa Taifa letu yaliasisiwa na kuanza kutekelezwa ndani ya kipindi ambacho Ngeleja alikuwa Waziri wa Nishati na Madini. Hii ndiyo sababu iliyonishawishi nianze na kuhitimisha makala hii kwamba katikati ya mafanikio ambayo Serikali ya Rais Kikwete imefanya anasimama Mtanzania aitwaye William Ngeleja, aliyekuwa Naibu na Waziri wa Nishati na Madini (2007-2012).

Mafanikio niliyoyataja pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali, hususan iliyomo katika sekta sita zilizopewa kipaumbele, na usimamizi unaofanywa kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) unaihakikishia nchi yetu kuondokana na umaskini ifikapo mwaka 2025.

Wakati tunamshuru Mungu kwa neema ya rasilimali aliyotuletea, kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na kupiga vita rushwa na vitendo vyote viovu vinavyodhoofisha kasi ya maendeleo ya Taifa letu.

Mwandishi wa makala, amejitambulisha kuwa ni msomaji mahiri wa gazeti hili. Anapatikana Kinondoni, Dar es Salaam.