Naanza na salamu kama Mtanzania mwenye uzalendo.  Watu wengi hawaelewi maana halisi ya uzalendo. Inawezekana hata mimi nikawa miongoni mwao, kwa maana ya leo ambayo inazungumzwa na wanasiasa wengi vijana na walioibuka katika uwanja wa siasa kama sehemu ya ajira.

Kwa ufupi sisi watu wa zamani tulitafsiri uzalendo kama upendo baina yetu kama taifa na upendo kwa taifa letu.

Kuna mambo mengi sana yanayokera ukiwasikiliza watu kuhusu maana ya uzalendo. Kuna watu wanakufuru hadi kufananisha upendo wa mtu na mtu kuwa ni uzalendo. Unakuta mtu shingo imekaza kabisa anafura kuwa huo ndio uzalendo, sijui tunakwenda wapi. Ninahofia miaka hamsini ijayo inawezekana tukapoteza kabisa maana ya uzalendo.

Leo nimeamka nikitaka kujua mamlaka za wakala wa serikali katika mambo mengine, naona kila mtu anaiangalia serikali hata katika mambo ambayo serikali yenyewe imekasimisha kwa baadhi ya wakala wake.

Wiki jana nimeandika juu ya matangazo ya waganga wa kienyeji, ni nani mwenye dhamana ya uwakala kutoka serikalini? Au ndiyo tusubiri waziri mwenye dhamana atoe tamko katika suala la utapeli?

Sisi watu wa zamani bado tunaamini kupata taarifa katika magazeti, redio, televisheni na hata katika soga huku mitaani baada ya kazi za kutwa nzima. Hatuna muda wa kukaa baa au kufanya siasa, ule muda tunaopumzika tunajadili mambo mengi yenye mustakabali wa taifa letu, katika kupiga soga tunakutana na mambo mseto mengi ambayo yanatuvuruga akili.

Sasa hivi nchi imekumbwa na biashara huria na matukio huria. Kwa kisingizio cha uhuria, imefika mahali mpaka jambo makini linafanyiwa masihara, jambo la afya, siasa, diplomasia, maendeleo, kilimo na mengine mengi. Huu uhuria ndio nataka kuhoji uhalali wake iwapo utakuwa umekasimishwa kwa wakala yoyote ya serikali.

Tulianza kusikia vipodozi vya kina dada vikiangaliwa na kukaguliwa kama vina madhara, maduka kadhaa yalifungwa baada ya kubainika kuwa wanauza sumu badala ya dawa, lakini maduka ya mkononi yalibaki yakizunguka baa jioni na katika saluni kadhaa hapa mjini, lakini kibaya zaidi kuliibuka wajasiriamali wadogo wadogo waliokuwa wakifungasha mizigo kwa ajili ya wateja.

Taratibu tukasikia kuna sindano za kubadili maumbile ya binadamu, tulisikia kauli ya wakala wa serikali akitoa onyo kwa wachomaji na wachomwaji, lakini cha ajabu hatujawahi kushuhudia mtu akikamatwa na kupelekwa mbele ya sheria, sijui kwa nini, labda ushahidi utasumbua.

Vikaja vidonge maalumu kutoka ughaibuni kwa ajili ya matumizi ya binadamu kuongeza nguvu zaidi ya ile ambayo anayo, kimyakimya nayo mpaka leo sijasikia kelele za wadau kuhusu jambo hilo. Zaidi ya vidonge, kuna unga sasa ambao vijana wanatumia kama vile wameambiwa ndiyo suluhisho la matatizo yao.

Suala langu ni jinsi ambavyo uhuria huu unataka kutufikisha mahali kiasi cha kuanza kuonekana nchi yetu kuwa shimo la kutupa taka kwa kulipwa. Zipo bidhaa ambazo hatuna uhakika kama zimepita katika taasisi na wakala zetu zenye mamlaka.

Huku Kipatimo tunaletewa kila kitu, tunaletewa tochi ambazo hazitumii betri kiasi kwamba ikigoma kuwaka ni ya kutupa. Tunaletewa simu ambazo betri zake zinabinyika kama tonge la ugali, ukichaji usiku kucha unapiga simu moja tu na simu inazima kwa kukosa chaji. Huku  ni kama dampo na sijui hayo magari yanayobeba hizo taka yanapita wapi kusiko na mawakala wa kusimamia mambo hayo.

Tunaletewa vitu vidogo vidogo na hawa watu wanaojiita wa promosheni katika maeneo ya baa na tunanunua kwa nguvu ya pombe kichwani na asubuhi tunaanza kujiuliza ni kitu gani umenunua. Tunavyovinunua havina mkataba wala risiti ya EFD na hatujui vinatoka wapi, tunauziwa sabuni tatu kwa bei ya sabuni sita, hatujui madhara yake siku zijazo.

Kama kweli tunaweza kudhibiti mambo makubwa kama rushwa, mapato ya taifa, mafuta, dawa za kulevya na mengineyo, tunashindwaje kuwadhibiti hawa wachache ambao wanaua taifa la kesho kwa kuuza sumu mchana kweupe?

Ni kweli tumeshindwa kuwakamata hawa wahuni wachache wanaotaka kuharibu sura ya nchi yetu kwa kutubagaza na vitu vya kijinga?

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.