Baadhi ya watu inawezekana wakawa wamekwisha kusahau kwamba kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika zilikuwepo bendi nyingi lakini mara baada ya Uhuru kuliundwa bendi iliyopewa jina la NUTA Jazz.
Mwaka huu inatimiza miaka 55 tangu ianzishwe mwaka 1964 katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa chini ya umiliki wa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (National Union of Tanzania) kwa kifupi NUTA.
Mwaka huohuo wa 1964 Muhidini Gurumo (sasa marehemu) aliitwa kujiunga na bendi hiyo ya NUTA Jazz akitokea katika bendi ya Rufiji Jazz, na kuwa mmoja wa waasisi wa bendi hiyo.
Gurumo aliungana na wanamuziki wengine kina Hamis Sama, Mnenge Ramadhani na Wilfred Boniface. Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa ‘Baba Nyerere’ – wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine zilikuwa ‘Kilimo ni Kazi Yetu’ na ‘Mwengele.’
Mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri, John Simon, alijiunga na bendi hiyo ya NUTA Jazz. Mpiga gitaa la solo, Ahmed Omar, alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi, pia ndiye aliyetamba mno katika wimbo wa ‘Mwangele.’
Jumuiya hiyo ilipobadili majina kuwa ‘Organization of Tanzania Trade Unions’ kwa kifupi OTTU, bendi nayo ikawa OTTU Jazz.
Baada ya kipindi kingine kupita, jumuiya hiyo ikabadili majina kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania, kwa kifupi JUWATA.
Wakati wa uhai wake marehemu Gurumo aliwahi kusema kuwa mpiga solo, Ahmed Omar, ndiye aliyechaguliwa kuwa kiongozi wa NUTA Jazz wakati huo.
Mzee Gurumo ambaye ndiye aliasisi mtindo wa ‘Msondo’, ukiwa ni wa asili ya kabila la Kizaramo, aliweza kutamba katika nyimbo mbalimbali.
Baadhi ya nyimbo zilizorekodiwa wakati huo zilikuwa ni ‘Aziza’, ‘Tukiwa Monica Shuleni’, ‘Sakina’, ‘Maneno ya Nyerere’, ‘Mipacha Ngui’ na nyingine nyingi. Wakati huo huo mpiga solo, Saidi Mabera, alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo.
Baadhi ya wanamuziki waliounda Juwata Jazz ni pamoja na waimbaji Muhidini Gurumo, Hassan Bichuka na mpiga kinanda, Waziri Alli, ambaye hivi sasa ni mmoja kati ya viongozi wa bendi ya The Kilimanjaro Band (Wana Njenje).
Miaka hiyo ya 1980 hadi 1990, takriban kila bendi ilikuwa na wapiga vinanda. Ikumbukwe katika bendi ya Maquis du Zaire, alikuwa akibofya Mbuya Makonga ‘Adios’, alikuwepo mwanamama pekee, Asia Darwesh, aliyekuwa akikipapasa kinanda hususan katika bendi ya MK Group, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Bandari Grill, kwenye Hoteli ya New Africa, ya jijini Dar es Salaam.
Ushindani kati ya bendi za muziki wa dansi ulipoongezeka, mwaka 1978, Muhidini Gurumo na Hassan Rehani Bichuka walihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra.
Gurumo alipofika katika bendi hiyo akawa kiongozi wa bendi sambamba na kuasisi mtindo wa ‘Sikinde Ngoma ya Ukae.’ Mtindo huo ni wa asili ya ngoma za Kizaramo.