Kwa wiki tatu mfululizo tumekuwa tukiandika habari juu ya mkataba wa kununua matrekta na kujenga kiwanda cha kuunganisha matrekta cha URSUS kilichopo wilayani Kibaha.

Kiwanda cha kuunganisha matrekta kwa mujibu wa mkataba ilibidi kiwe kimekamilika Juni, mwaka jana. Hadi leo kazi iliyofanyika ni ndogo kwa kiwango kisichoridhisha.

Kampuni ya URSUS iliingia mkataba na SUMA JKT, ambayo baadaye imehamishia mkataba huu kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Hadi sasa mkataba huo ulioingiwa Oktoba 22, 2015, yaani siku nane kabla ya Uchaguzi Mkuu, umetekelezwa kwa kusuasua. Kampuni ya URSUS imeshindwa kuleta matrekta kwa wakati, lakini hata hayo machache 825 iliyoleta yana matatizo mengi.

Tumesema kupitia habari tulizochapisha kuwa matairi ya mbele ya matrekta hayo rimu zinavunjika, matairi yanatobolewa na ‘mbigiri’, jembe linakatika, kifua cha trekta kinakatika, mfumo wa umeme si mzuri, honi hazilii, betri ni mbovu kwa matrekta yote na matatizo mengine mengi. Yameainishwa matatizo 20 yanayoyakumba matrekta hayo.

Matrekta yaliyoletwa hayana vipuri hadi NDC wamechukua uamuzi wa kufungua, wenyewe wanasema kuchinja matrekta 26 kwa ajili ya kupata vipuri (spare) za matrekta hayo.

Katika hali ya sintofahamu, NDC imeamua kuwaelekeza wakulima kununua vipuri vya trekta aina ya Massey Ferguson. URSUS waliingia mkataba wa kuleta vipuri kabla ya kuleta matrekta yote 2,400 nchini.

Mkataba unawataka wazabuni hawa wanaolipwa kwa mkopo wa masharti nafuu kujenga vituo vinane vya kukarabati matrekta na kuwa na magari ya kwenda vijijini kuhudumia matrekta ya wakulima.

Kampuni hii ya URSUS zipo taarifa kuwa iko chini ya mufilisi. Tunapata hofu kuwa dalili zilizopo serikali isipochukua hatua za haraka, wakulima badala ya kukombolewa watajikuta wanauziwa vyuma chakavu visivyo na faida. Pia kuna taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, kuwa tayari Tanzania imelipa asilimia 60 ya malipo. Tunataka uchunguzi ufanyike ili kubaini kama malipo haya ni kwa mujibu wa mkataba.

Tumefurahishwa na hatua ya Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuwaita Waziri wa Viwanda na Biashara na Katibu Mkuu wake wakawahoji na kuwataka wachukue hatua kudhibiti hali. Tumepata moyo zaidi baada ya kuona waziri na katibu mkuu wamekutana na Balozi wa Poland nchini, Krzysztof Buzalski, nchi iliyotukopesha kwa ajili ya kununua matrekta hayo.

Upungufu ulioainishwa na wabunge wa matrekta haya kutokuwa na hakikisho (warranty), ubovu wote ulioainishwa na hatua ya kukagua matrekta haya kabla ya kuletwa nchini, tunapenda iwe sehemu ya mabadiliko ya msingi ya mkataba kati ya Tanzania na Kampuni ya URSUS, ambayo kwa jinsi mkataba wao ulivyokaa, unapingana na mkataba mama ulioingiwa kuchukua mkopo kati ya Tanzania na Poland. Tuwasaidie wakulima wetu kwa kuzuia wasiuziwe matrekta mabovu. Mungu ibariki Tanzania.