Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ambapo ilikuwa inasomeka: ‘hauwezi ukashinda kama hauchezi, mwanadamu anaishi mara moja tu hapa duniani. Tunaloweza kulifanya sasa, tulifanye kwa sababu hatuishi mara ya pili hapa duniani. Kubahatika kuishi duniani ni fursa.’ Endelea…
Ni fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, hatujapata fursa ya kuishi duniani kwa bahati mbaya. Mungu habahatishi. Mwanasayansi Albert anasema: “Mungu hachezi bahati nasibu.”
Dunia inawahitaji watafiti na wabunifu wa kila nyanja inayomhusu binadamu, tusifurahie kuwa taifa la watu wanaoshindwa kwa kila nyanja. Mafanikio yenye matunda mazuri yanahitaji uvumilivu.
Ukiona njia ambayo haina vikwazo huenda haielekei mahali popote. Katika barabara ya mafanikio kuna kila aina ya ukinzani, daima alama ya mafanikio ni maumivu kwanza. Bidii ni mama wa bahati njema.
Walioyafikia mafanikio ya kiuchumi, kiroho, kimaadili na kielimu wanayo alama ya maumivu. Walijituma kufanya kazi. Hawakukata tamaa, katika maisha unahitaji watu watakaokuzomea ili umkimbilie Mungu.
Unahitaji watu watakaojaribu kukutakia hofu ili uwe na ujasiri. Unahitaji watu watakaosema ‘hapana’ ili ujifunze mbinu mpya ya mafanikio. Unahitaji watu watakaokukatisha tamaa ili uweke matumaini yako kwa Mungu.
Unahitaji watu watakaokufanya upoteze kazi yako ili uanzishe biashara yako. Hayo yanaitwa ‘mapito’ ya kueleka njia ya mafanikio. Swami Sivanda anasema: “Maisha ni shule ambamo kila majonzi, kila maumivu, kila jambo la kuvunja moyo huleta fundisho kubwa.”
Watu hawampigi teke mbwa aliyekufa bali aliye hai. Watu hawautupii mawe mwembe usio na matunda bali ulio na matunda. Watu wengi wameshindwa kuyafikia mafanikio waliyonuia katika maisha yao kwa sababu wameruhusu maneno yawakatishe tamaa.
Kwa mfano, mtu akiwa mkarimu wanasema anajitangaza, asipokuwa mkarimu wanasema ana gundi kwenye vidole. Mtu akitoa hotuba fupi sana wanasema hakujiandaa, akitoa hotuba ndefu wanasema hatunzi muda.
Akiwa mtoto mchanga wanasema ni malaika, akiwa mtu mzima wanasema achana na yule shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni Mkatoliki zaidi ya Papa. Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni.
Akiaga dunia katika umri wa ujana wanasema angefanya mengi mazuri. Akifikia umri wa uzeeni wanasema miaka yake aliiharibu tu bila kufanya chochote. Watu watakusema tu lakini usiwachukie.
Mwanafalsafa Athisthenes anasema: “Wasikilize maadui wako, kwa sababu ni wa kwanza kugundua makosa yako.” David Brnkley anasema: “Mtu aliyefanikiwa ni yule ambaye anaweza kujenga msingi imara akitumia matofali waliyomrushia.”
Kupata pancha si mwisho wa safari. Safari inaendelea baada ya kuziba pancha, pancha ni vikwazo unavyokutana navyo katika harakati za kuyafikia yale mafanikio uliyonuia.
“Nimejifunza kuwa mafanikio hayapimwi sana na nafasi aliyoifikia mtu katika maisha bali vikwazo alivyoweza kushinda huku akijaribu kufaulu.’’ Aliandika Booker T. Washington.
Kupanga ni kuchagua, mwanafalsafa Benjamin Franklin anasema: “Ukishindwa kujiandaa, umejiandaa kushindwaa.” Hakuna anayepanga kushindwa ila wengi wanashindwa kupanga.
Mwandishi Vincent Lombardi anasema: “Kila mtu anapenda kufanikiwa, ila ni wachache wanaopenda kujiandaa kufanikiwa.” Mafanikio yanahitaji maandalizi, mtu anayeweza kukuokoa wewe ni wewe.
Ni wewe unayeweza kujiandikia historia nzuri au mbaya. Ni wewe unayeweza kuwa chachu ya mabadiliko au mhanga. Unaishi maisha yako, hauishi maisha ya mtu mwingine.
Maisha ni kuanguka na kuinuka. Ukianguka – inuka. Ukianguka amini unaweza bado kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Virgil anasema: “Wanashinda wale wanaoamini wanashinda.”
Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi. Napoleon Bonaparte anaandika: “Haiwezekani ni neno linalokutwa katika kamusi ya wapumbavu.”
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela anaandika: “Neno haiwezekani halimo katika kamusi yangu.”
Marcus Aurelius anaandika: “Kwa sababu jambo linaonekana ni gumu kwako, usifikiri kwa wengine haliwezekani.” Hauwezi ukashinda kama hauchezi.