Wananchi Manispaa ya Songea wameelezea wasiwasi wao kuhusu kukumbwa na milipuko wa magonjwa mbalimbali, kutokana na kukidhiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali yakiwamo soko kuu la mji buo.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wamesema miundombinu ya maji taka Soko Kuu la Songea ni mibovu. Mitaro ya mji huo imefurika na kutiririsha maji hovyo yanayosambaa kwenye maeneo ya wauza nyanya, vitunguu, samaki na dagaa.
Kitendo cha kutiririka kwa maji katika mji huo ni kutokana na maji yanayotumika kuoshea utumbo na kumwagwa hovyo bila kufuata utaratibu.
Saidi Ally, mfanyabiashara wa Soko Kuu la Songea, amesema chemba ya maji machafu hujaa na maji kutiririka hovyo. Hali hiyo inatishia maisha yao huku wahusika wakijua kwamba maji hayo ni mkusanyiko wa uchafu kutoka vyooni na maeneo mengine na wauza nyama kwenye mabucha. Chemba za maji machafu zinaziba na maji kusambaa ovyo.
“Kwa kweli hapa chemba hii unayoiona maji yakijaa linafumuka na hapa pote panajaa maji, huwezi kukaa, pananuka vibaya na haya maji ni ya vyooni na mengine yanayotoka kwenye mabucha, hata wewe mwenyewe ulivyokaa hapa kwa muda mfupi unaona panavyonuka, hii ni hatari sana kwa afya zetu,’’ amesema Saidi.
Katika Soko la Manzese, wafanyabiashara wa maeneo hayo wameiambia JAMHURI kuwa uchafu unatupwa kila mahali hadi njia inajifunga na kwa kuwa hakuna eneo la kutupa taka, hivyo wameiomba halmashauri kuondoa taka zilizosahaulika kipindi kirefu bila kuzolewa.
Mikidadi Kanduru, mfanyabiashara wa machungwa sokoni hapo, amesema wanashangazwa na manispaa, miezi mingi inapita hakuna hatua zozote zinazochukuliwa za kuondoa taka hadi hali inakuwa mbaya, harufu kali hasa wakati wa mvua.
Kutokana na mlundikano wa taka, wateja wao hawasogei kwenye biashara zao kwa kuogopa harufu ya jalala na kwamba Maafisa Afya wanapotembelea sokoni hapo na kujionea shehena ya uchafu, wanawaahidi kuzoa wakiondoka hawarudi tena.
“Hali ni mbaya wateja hawakai, wanapoona nzi wamejaa wanadhani machungwa yameoza, sisi wenyewe tunaumwa mara kwa mara kila wiki lazima tunywe dawa, na usione tumekaa hapa tunakula chakula ni shida tu hizi, hapa hapakaliki tukikaa mbali wateja wanatupita, bora tujitese ili tupate hela ya kula, ingenyesha hata wewe mwenyewe usingeendelea kuuliza maswali,’’ amesema Kanduru.
Pamoja na manispaa kushindwa kuweka mji safi, wafanyabiashara wa maeneo yote kila mmoja hutozwa ushuru wa Sh 400, kwa siku manispaa hukusanya Sh 100,000 kwa Soko la Manzese wakati Soko Kuu la Songea hukusanya Sh 150,000 kwa siku.
Manispaa ya Songea kwa siku inazalisha taka ngumu tani 15,000 na magari yanayozoa taka ni matatu na vikundi kazi vilivyopewa kazi ya kufagia na kuzoa taka havina uwezo wa kumaliza taka.
Mbali na uchafu katika masoko, Stendi Kuu nayo imelalamikiwa kukithiri kwa uchafu unaotokana na ukosefu wa vifaa vya kuhifadhia taka na wakati mwingine watu hujaza mikojo kwenye makopo ya maji na kuyatupa ovyo.
Emanuel Haule, mfanyabiashara katika Stendi Kuu Songea, ameiambia JAMHURI kuwa stendi hiyo haifanani na hadhi ya manispaa hiyo hasa wakati wa masika, hutapakaa matope na kuleta mwonekano mbaya kwa wageni wanaokuja mkoani kwa mara ya kwanza.
Mbali na Stendi Kuu katika mtaa wa Delux hawana choo na hujisaidia kwenye vichochoro, sehemu ambazo mama lishe hufanya biashara katika maeneo ya vichohoro hivyo.
“Stendi haina ubora hilo la kwanza, halafu chafu, wageni wote wanaokuja kwa mara ya kwanza wanafikia stendi sasa unadhani wakija tu wanapokewa na tope, uchafu umezagaa utadhani hii stendi haina mwenyewe, hata vyombo vya kuwekea taka hakuna, kinachosikitisha hapa yupo bibi mmoja anayefanya kazi ya usafi hana hata vifaa vya kujikinga hasa glovu, na kibaya zaidi kuna watu wanaweka mikojo kwenye makopo na kuyatupa ovyo,” ’amesema Haule.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Zakaria Nachoa, alipoulizwa kuhusu uchafu unaolalamikiwa, amesema hilo si jukumu lake bali ni la maafisa wa afya, na kuongeza kuwa yeye hana taarifa kama mji ni mchafu na kama kuna malalamiko hayo atasubiri taarifa ya Afisa Afya wa Manispaa au mkuu wa masoko.
“Mimi nina mambo mengi, siwezi kujua kama kuna uchafu stendi na sokoni, mtafute Afisa Afya atakwambia, kama maji machafu yanatiririka ovyo ni suala lake kuwakamata mama lishe wanaotupa mifupa kwenye makaro ndiyo maana yanaziba,’’ amesema Nachoa.
Alipotafutwa Afisa Afya wa Manispaa aliyejulikana kwa jina moja la Mahundi, kwa njia ya simu, alisema yuko nje ya ofisi kikazi. Hata hivyo, gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na wasaidizi wake lakini walikataa kuzungumzia hilo ingawa walikiri kukithiri kwa uchafu katika viunga vya Manispaa ya Songea.
Naye Mkuu wa Masoko, Salumu Homela, amesema tatizo la uchafu linasababishwa na maafisa afya kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo, huku akitoa lawama kwa Afisa Afya wa Manispaa.
“Hili wa kulaumiwa ni Mahundi, anawaondoa watu wanaosimamia vizuri na kuwaweka watu anaowataka yeye, alimtoa Mchata ambaye alikuwa anamudu, matokeo yake ndiyo haya malalamiko kibao,” amesema Homela.
Katika hali isiyo ya kawaida, JAMHURI ilishuhudia chemba ya maji taka Mtaa wa Magengeni Mfaranyaki limefumka na kutiririsha maji ovyo na watoto wakionekana kucheza kwenye madimbwi, jambo ambalo ni la hatari kwa afya.