WIKI hii tumeshuhudia michango mbalimbali ikitoka kwa wabunge kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma. Yametokea malumbano kati ya wabunge kadhaa na kiti cha Spika. Binafsi nilishuhudia tukio hili, hadi Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa amekalia kati cha Spika akaamuru mbunge mmoja kuondolewa ukumbini. Mabaunsa sita, walikwishajongea kwa nia ya kumtoa ukumbini, lakini yeye akajitoa mwenyewe.

 

Wabunge hawa walianzisha tafrani baada ya kuwa wameomba mwongozo wa Spika, wakitaka kumjibu Stella Manyanya, ambaye inaaminika alikipakazia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kudai kuwa kinashiriki kuhamasisha madaktari nchini waendelee kugoma.

 

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alikuwa wa kwanza kuomba mwongozo wa Spika akaeleza alichokiona kuwa ni uongo. Kabla hajakaa sawa, Mweka Hazina wa CCM, Mwiguru Nchemba, akatumia taarifa ya Wapinzani kuthibitisha alichokiita mpango wa wapinzani kuendelea kuchochea wafanyakazi wagome nchini.

 

Mwenyekiti wa Kikao hicho, alionekana kuelemewa na wabunge na kuishia kuendelea kusema: “Kaa chini, kaa chini, nasema kaaa chini… msitafute umaarufu hapa.” Huku wakati Mwenyekiti akisema hivyo kutoka kwenye kiti cha Spika, nilisikia maneno yaliyonipa shida. Sikumfahamu ni nani, ila kutoka kwenye ukumbi wa Bunge mmoja akasema hivi: “Oyaaaaa, tuondoleee kiwingu.”

 

Kwa kweli waheshimiwa wabunge binafsi nataka niwambie msiyoambiwa. Najua mnayo kinga ya kusema au kufanya lolote muwapo bungeni pasi kushitakiwa au kuchukuliwa hatua yoyote kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, napata wasiwasi uhuru huu sasa mmeanza kuutumia vibaya.

 

Mmeutumia vibaya kwa kiwango ambacho heshima ya bunge iko mashakani. Bunge sasa limegeuka kijiwe cha kufanyia uhuni kwa baadhi ya wabunge. Kauli na matendo yenu hata kama yanalindwa na sheria, yataifikisha mahala nchi idharauliwe mbele ya mataifa mengine. Mkumbuke kuwa televisheni zinaonekana ndani na nje ya nchi.

 

Heshima mliyopewa kisheria inawezekana baadhi yenu hamuitambui. Heshima hii inapaswa kuwafanya muwe mfano wa matendo mema. Inawapasa nyie kama wabunge muwe chimbuko la mijadala yanye afya katika jamii. Leo katika vijiwe, watu wanajadili lugha za wabunge na si hoja za msingi mnazowasilisha. Hii si kwa sababu hamuwasilishi hoja za msingi, bali kwa sababu baadhi yenu mnaziwasilisha kwa lugha ya kihuni.

 

Tunalikumbuka na kulitamani Bunge la enzi za akina Sebastiani Rukiza Kinyondo. Mnatufanya tulitamani bunge la akina Dk. Chrisant Mzindakaya. Hawa walikuwa wakitofautiana mara kadhaa na Serikali au Chama tawala, lakini staha ilikuwa sehemu ya lugha waliyotumia kufikisha ujumbe kusudiwa.

 

Nafahamu kuwa watu wanakerwa na dhana ya kuwa na chuo cha siasa. Inawezekana baadhi yetu tunaona kilichokuwa Chuo cha Siasa Kivukoni ni mali ya CCM hivyo hakina maana tena kwa Watanzania. Mimi nasema utaratibu wa sasa wa kuokota watu mitaani ambao wakati mwingine hawajathibitika kama wana mwenendo mzuri, lakini ama kwa fedha zao au kwa umaarufu chama tawala na wapinzani mkawakumbatia, mnaipeleka nchi hii kusiko.

 

Narudia, haiwezekani tukawa na viongozi wanaotamka lugha za kihuni katika sehemu muhimu kama hii ya Bunge. Watanzania tumechoshwa na michezo ya kitoto inayofanywa bungeni kwa sasa. Tunasema ifike mahala kanuni za Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Haki, Wajibu na Kinga za Bunge zirekebishwe na kuchukulia hatua kali zaidi wabunge wenye kupotoka.

 

Lakini pia hii ni fursa kwa Watanzania. Kwa hali ilivyo hatuwezi kuacha nchi yetu ikaendelea kuangukia mikononi mwa viongozi wasio na maadili. Iwe ni wa chama tawala au wa vyama vya upinzani, tuutumie mchakato wa Katiba Mpya kuingiza Ibara yenye kutaja sifa za mtu kuwa kiongozi. Katiba mpya ivilazimu vyama vya siasa au kiwepo chuko cha kitaifa ambacho yeyote anayetaka uongozi katika nchi hii atawajibika kupata mafunzo.

 

Wakati tukisubiri chuo hicho, turejee katika misingi ya ustaarabu. Demokrasia ni sehemu ya kustaarabika. Inapotokea mwenzako akatoa hoja usiyokubaliana nayo, jibu si kupiga kelele, kuguna au kumrushia ngumi, bali ni kusubiri akamaliza kueleza utumbo wake nawe ukasimama kwa njia ya taarifa au mwongozo wa Spika ukamshushua kwa hoja.

 

Na hapa naomba nieleweke. Nidhamu imeshuka si kwa wapinzani tu, hata kwa wabunge wa CCM. Utaratibu unaotumika kuwasilisha hoja za kuwajibu wapinzani wanapotoa hoja unathibitisha ama utovu wa nidhamu au kupungukiwa kwa maarifa. Nasema hapa tulipofikia sasa basi. Nchi hii haiwezi kuendelea na utaratibu wa viongozi kutojiheshimu.

 

Heshima ya wabunge itadumu tu kwa wao kujihesimu kwanza. Hatuwezi kuendelea na utaratibu huu ambao kimsingi unaharibu heshima ya taifa na kuwajenga vijana na watoto kuhisi kwamba kiongozi bora mtu mwenye uwezo wa kufanya fujo na vurugu. Hapana. Hatuwezi kwenda hivyo. Wabunge jiheshimu na mjirekebishe.