Baada ya gazeti hili la uchunguzi, JAMHURI, kuandika kuhusu ubovu wa matrekta wanayouziwa wakulima nchini wiki iliyopita, Bunge kupitia Kamati ya Viwanda na Biashara limeingilia kati kunusuru nchi kuingia katika madeni yasiyo na faida, hivyo kumwita Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ajieleze.

Habari za uhakika kutoka bungeni zinaeleza kuwa Jumatano iliyopita uongozi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) uliitwa bungeni, lakini mara tu baada ya kuwasilisha taarifa yake ulibanwa kila kona ukakosa majibu na kufukuzwa mbele ya kamati. Walipewa maswali 10 wanayopaswa kuwa na majibu yasiyo ya ‘kubabaisha’ ambayo walipaswa kuyawasilisha mbele ya kamati jana.

Hadi JAMHURI linakwenda mitamboni kikao cha Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara kilikuwa kinaendelea. Katika kikao cha Jumatano iliyopita, Kamati ya Bunge ilitaka maelezo kwa nini mradi wa kuleta matrekta umechelewa kukamilika, matrekta mengi yaliyoletwa ni mabovu na kwa nini NDC pamoja na kubaini ubovu wa matreka hayo imeendelea kuyauza kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ameliambia JAMHURI hivi karibuni kwamba serikali imekwishalipa asilimia 60 ya malipo ambayo ni dola milioni 33, sawa na Sh bilioni 75.9, na kwamba URSUS wamekwishaleta matrekta 825 na kwamba matrekta 1,575 yaliyosalia Kampuni hii ya URSUS ambayo taarifa zinaonyesha kuwa imewekwa chini ya Mufilisi kwa kukosa fedha imeahidi kuwa itayaleta kwa wakati ifikapo Oktoba mwaka huu bila wasiwasi.

Mradi wote gharama yake ni dola milioni 55, sawa na Sh bilioni 126.5, ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Poland. Mkopo huu unaopaswa kulipwa ndani ya miaka 30, ulisainiwa kati ya Tanzania na Poland Septemba 28, mwaka 2015 ukiwa ni mwezi mmoja kabla ya uchaguzi na mkataba wa kununua matreka ya URSUS kwa kutumia mkopo huu ukasainiwa Oktoba 22, mwaka 2015, yaani siku 8 kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Pamoja na kupokea asilimia 60 ya malipo, matrekta iliyoleta URSUS ni sawa na asilimia 34 ya mradi wote wa matrekta 2,400. Kwa wastani Tanzania ilikuwa inaingiza matrekta 200 kwa mwaka. Matrekta huwa yanafanya kazi hadi miaka 50 bila kuharibika. Idadi hii ya matrekta 2,400 ingechukua wastani wa miaka 12 kuingizwa nchini chini ya utaratibu wa kawaida, ila bahati mbaya matrekta haya yanayoingizwa mengine yanaharibika kabla ya kufikishwa shambani.

 

Wabunge wahoji mkataba

Wabunge waliwaweka kitimoto maofisa wa NDC kufahamu ilikuwaje mkataba haujatekelezwa kwa wakati na kwa nini Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) cha jijini Arusha hakikutoa cheti cha ubora wa matreka ya URSUS. Majibu waliyopewa ni kuwa awali CAMARTEC ilikagua matreka na kubaini kuwa yana ubovu URSUS ikaurekebisha.

NDC iliwaambia wajumbe wa Kamati ya Bunge kuwa serikakali iliipatia CAMARTEC jukumu la ukaguzi wa matrekta haya na kufanya majaribio yote ya msingi kwa CAMARTEC, ambayo ilibaini upungufu wa kiufundi kwa matrekta hayo – kama kufunguka kwa jembe na kuvunjika kwa ‘rims’ za matairi. Kwa kubaini hayo na baada ya kutaarifiwa Kampuni ya URSUS, ilifanya marekebisho na awamu ya kwanza ya matrekta ikaletwa nchini.

Baada ya matrekta kuingia nchini na kuanza kutumika, matrekta yalibainika kuwa na matatizo mengine mengi. NDC iliiomba CAMARTEC kufanya ukaguzi kwa mara ya pili. Ukaguzi ulibaini aina 19 za ubovu kwa matrekta hayo, ikiwamo rimu kuendelea kuvunjika, kifua cha trekta kuvunjika, tairi kupata pancha kila mara, taa na mfumo wa umeme kuwa na matatizo na mengine mengi.

Inaelezwa wabunge wamehoji imekuwaje baada ya CAMARTEC kukagua na kubaini upungufu huo bado matrekta yameendelea kuingia nchini? CAMARTEC ndiyo taasisi yenye wajibu wa kutoa cheti cha ubora kwa matrekta yanayoingizwa nchini, lakini NDC haikuomba cheti hiki cha ubora na ikaendelea kuuza matrekta mabovu kwa wakulima.

Hata hivyo, NDC walifahamu fika kuwa hata kama CAMARTEC wakikagua na kubaini ubovu wa aina yoyote, hawawezi kusaidia kitu, kwani mkataba umeitia serikali kitanzi. Kifungu cha 8 cha Masharti Mahususi ya Mkataba (SCC), kikirejea kifungu cha 10 cha masharti ya jumla ya mkataba kati ya URSUS na SUMA JKT uliorithiwa na NDC, kinasema bayana kuwa URSUS atajikagua mwenyewe kwa kutumia viwango vyake vya ubora na kujipa cheti cha ithibati.

“Mzabuni anapaswa kuwasilisha cheti cha ukaguzi alichokitoa yeye mwenyewe, ambacho kitaambatanishwa na vyeti ya mtengenezaji kwa mnunuzi (Serikali ya Tanzania) ili kuthibitisha kuwa bidhaa zimetengenezwa kwa viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa mkataba,” inasema sehemu ya mkataba huo ambao URSUS ndiye mzabuni na mtengenezaji wa matrekta hayo.

Kifungu cha 10 cha masharti mahususi ya mkataba (SCC) yanayochukua mkondo katika mkataba huu, kikirejea kifungu cha 12(1)(e) cha masharti ya jumla ya mkataba (GCC), kinatoa mamlaka makubwa mno kwa URSUS.

Kwanza kifungu kidogo kinachotangulia cha (d) kinaipa URSUS mamlaka ya kuifahamisha NDC kuwa sasa imeanza kufungasha mzigo wa matreka kuletwa Tanzania. Baada ya NDC kupokea taarifa hiyo, ndani ya siku 5 za kazi inapaswa kupeleka wakaguzi nchini Poland kukagua matrekta hayo.

Wakaguzi hao wanapaswa kulipiwa gharama za usafiri wa ndege na Serikali ya Tanzania na URSUS wenyewe wanalipa gharama za watu watatu kulala hotelini kwao kwa muda usiozidi siku 5. “Kushindwa kutuma wakaguzi, kutamaanisha kuwa mnunuzi (Serikali ya Tanzania) amejiondolea haki ya kukagua mzigo (matrekta) yakiwa kiwandani,” inasema sehemu ya mkataba huo ambao JAMHURI limeuona.

Mbaya zaidi, matreka yakifika bandarini Dar es Salaam, mkataba unairuhusu serikali kukagua matrekta hayo kwa viwango vyake na taratibu kama yanapungua, bidhaa iliyoletwa ni yenyewe na ubovu wa mwonekano. “Serikali inapaswa ndani ya siku 7 za kazi tangu URSUS imefikisha matreka hayo, kuwasilisha madai husika.

“Kushindwa kutoa taarifa kwa URSUS ndani ya siku 7 kunamaanisha mnununzi (Serikali) amejiondolea fursa ya kuwasilisha madai dhidi ya ubovu utakaobainika na URSUS haitawajibika kwa lolote,” inasema sehemu ya mkataba huo.

Inaongeza kuwa ikiwa matreka yamebainika kuwa na ubovu, basi URSUS kwa uamuzi wake inaweza kutengeneza ubovu huo kwa gharama zake au kuleta mengine kufidia yaliyoharibika.

Kwa maana hiyo, kwa kuwa matreka yalikaa bandarini zaidi ya miezi 6 yalipoingizwa nchini hadi NDC ikalazimika kuilipa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) dola 272,586.5 sawa na Sh milioni 626.94 kutokana na URSUS kuchelewesha nyaraka za kutolea matrekta 825 yaliyowasili mwanzo, basi siku 7 za kukagua matreka hayo ziliishapita na wala NDC haikuwasilisha madai, hivyo hakuna chochote wanachowadai URSUS kimkataba.

 

Matrekta hayana waranti

Kifungu cha 13 cha Masharti Mahususi, kinaporejea kifungu cha 17 cha Masharti ya Jumla ya Mkataba, kinasema: “Hakikisho la URSUS linadumu kwa kipindi cha miezi 12 ya trekta kufanya kazi au saa 1,000 za magari, kulingana na kitakachowahi. Kipindi hiki kwa vyovyote iwavyo, kinapaswa kuwa ndani ya muda wa meizi 18 tangu siku ‘bill of lading’ inapotolewa baada ya mzigo kusafirishwa kwenda kwa mnunuzi.”

Hii maana yake ni kuwa muda wa hakikisho unahusisha hata muda wa kusafirisha matrekta haya, ambapo kwa yaliyoingia nchini mwaka 2017 hayana tena hakikisho (warranty), hivyo maelezo kuwa yakiharibika URSUS watayatengeneza hayana nguvu yoyote ya kisheria.

 

Hoja za wabunge

Wabunge wanataka kufahamu Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia NDC kwa nini haijasimamisha mkopo huu baada ya mzabuni kuwasilisha matrekta yaliyo mabovu na kushindwa kutekeleza mkataba kwa wakati. Kifungu cha 17.5 cha mkataba kinamruhusu mnunuzi kuvunja mkataba anapobaini kuwa mzabuni amekiuka masharti.

Walisema inakuwaje NDC inatumia gharama za walipakodi kufanya marekebisho ya matrekta na kutumia vipuri vya matrekta ya Massay Ferguson kwa maelezo kuwa ndivyo imara. “Kwanza hakuna makubaliano kati ya URSUS na NDC kutumia vipuri vya Massey Ferguson. Lakini hii peke yake kuwa hakuna vipuri vya URSUS unatumia vya Massey inasema bayana kuwa URSUS wameshindwa mkataba. Matrekta 825 waliyoleta ina maana hayana pa kupata vipuri.

“Kwa kukosa spea imefika mahala wakatwambia hao NDC kuwa wameamua ‘kuchinja’ matrekta 26 yawe spea. Hivi hii ni akili gani? Kwamba serikali inachukua mkopo, matreka haya yalipaswa kuuzwa au kukopesha kwa wakulima halafu eti yanakatwakatwa kuwa spea za kutengeneza matreka mabovu ya URSUS, mtu tuliyekubaliana atutengenezee matrekta mapya? Hii haikubaliki.

“Kuna watu wanamhujumu Mheshimiwa Rais [John] Magufuli. Ukiangalia siku ulipoingiwa mkataba, kwamba siku 8 kabla ya uchaguzi wanaingia mkataba huu wenye matatizo, yanaletwa matrekta mabovu, wanaendelea kuyatetea… hatuwaelewi kabisa watu hawa. Tunajua katibu mkuu na waziri ni wageni katika wizara hii, ila wanawajibika kishera. Wakishindwa kuwabana watendaji, sisi tunageuzia kibao kwao, maana hawa tunawamudu. Acha kwanza tuunde Kamati Teule ya Bunge, halafu tutajua mbivu na mbichi. Waziri akae mguu sawa,” amesema mmoja wa wabunge.

Mbunge mwingine akaongeza: “Hizi ni trekta mpya kabisa ‘brand new’. Hakuna namna trekta brand new inavunja kifua (central beam). Hata trekta za miaka 20 hazivunji vifua. Kwa shida kama hizi trekta ilitakiwa kurudishwa kwao mara moja ili zikarekebishwa na si kusambazia wakulima.”

 

Uongozi mbovu

Wabunge wamebaini pia kuwa NDC wanafanya mzaha katika masuala mazito ya nchi. Mbunge mwingine ameliabia JAMHURI kuwa kitengo cha matreka haya yanayoingizwa nchini ya URSUS kinaongozwa na mtu aliyesomea masuala ya rasilimali watu.

“Hapa alipaswa kuwapo mtaalamu, injinia. Hivi kweli NDC wako serious kweli? Wanachukua mtu wa HR ndiye anakiongoza kitengo hiki badala ya Mechanical Engineer au Agro Engineer?

“Huyu mtu wa HR hata akiulizwa nati inafananaje hajui. Hivi kweli tuko serious kukuza kilimo chetu kwa utaratibu huu kweli? Hapana. Mambo mengine lazima tuchukue hatua. Hatuwezi kuacha fedha za walipakodi zikaharibika kiasi hiki,” amesema.

Mbunge mwingine akaongeza: “Kwa mfano hapa tukiuliza mlioko humu ‘spindle’ ni nini? Mnajua? Gear box na engine zinaharibika, trekta mpya na sisi tunatafuta njia ya kutengeneza badala ya kurudisha kwa mtengenezaji ajue mwenyewe…

“Hizi gharama za mafundi na fidia kwa wakulima walioweka hela zao hapo huku yanaharibika anabeba nani? Kwa matatizo yote haya na bado mkaendelea kuyauza? Ni kuwatia umaskini wakulima wetu na kwa hili MD wa NDC hakwepi kuwajibika.”

Wabunge hawa walisema baada ya kuona matreka ni mabovu, NDC ilipaswa kuyarudisha kiwandani kwa URSUS kama ambavyo Toyota walirudisha magari 5,000 Japan walipobaini kuwa yalikuwa na tatizo la mfumo wa breki hivi karibuni.

NDC wamelijulisha Bunge kuwa URSUS wanapaswa kuingiza nchini matrekta 2,400 na zana zake kutoka Poland vikiwa katika vipande vipande vikubwa (Semi Knocked Down – SKD) na baadaye vikiwa katika mfumo wa vipuri (Completely Knocked Down – CKD).

Mpaka sasa yameingia matrekta 825, yaliyouzwa ni 586 na yaliyoko kiwandani bado ni 236 na ambayo yametumika kama ‘spare’ ni 26. Baada ya kuwa matrekta kadhaa yaliyouzwa kuwa yameharibika na hakuna ‘spare’ zake kwa sasa NDC imeamua kutoa ‘spare’ kwenye matrekta  mapya na kuwafungia wakulima.

Ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha matrekta – mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 40. Kimsingi kimechelewa kwa kuwa kwa mujibu wa mkataba kilipaswa kuwa kimekamilika kuanzia mwezi Juni, 2018.

URSUS walipaswa kuanzisha vituo 8 vya kuhudumia matrekta sehemu mbalimbali nchini kwa kutumia ‘Mobile Service Car’ 8 ambazo zilitakiwa kuletwa nchini mwanzoni mwa mwaka 2017, lakini mpaka sasa hakuna kituo kilichoanzishwa. Kwa mujibu wa mkataba mpaka sasa kulipaswa kuwa kumeshaletwa Mobile Service Cars/Vans na kuanza kuwahudumia wateja sehemu mbalimbali za nchi.

Kati ya matrekta hayo yaliyoletwa, matrekta 37 yameuzwa kwa fedha taslimu kwa thamani ya Sh 667,280,000. Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetoa mkopo kwa wakulima walionunua matrekta 33 yenye thamani ya Sh 417,670,000 na benki ikalipa hela yote kwa NDC kwa niaba ya mkulima ambaye ana mkataba wa mkopo na benki. Hata hivyo, wakulima wengi hawalipi wakidai matrekta yameharibika.

Matrekta mengi yameuzwa kwa njia ya kukodisha – ambapo mkulima anatumia trekta kukodisha wakulima wenzake na kutumia fedha anazokusanya kurudisha mkopo wa trekta. Njia hii imerahisisha, kwani wakulima waliokuwa hawana dhamana ya mikopo benki na wenye kipato cha chini wamepata fursa hiyo.

Jumla ya matrekta 516 yenye thamani ya Sh 26,193,994,030 yameuzwa kwa njia hii baada ya kuwa yamelipiwa kianzio cha Sh 5,155,170,555, hivyo deni linalobakia kwa wakopaji ni Sh 21,038,823,475 ambazo zinapaswa kulipwa ndani ya miezi 36.

 NDC baada ya kufanya mbinu za kuwasiliana na URSUS bila mafanikio, waliamua kwenda Poland kukutana na uongozi wa kiwanda hicho, ambapo uongozi ulibainisha kuwa hali ya fedha ya URSUS haikuwa ya kuridhisha. Kiwanda kimewekwa chini ya usimamizi wa menejimenti mpya katika jaribio la kuzuia kisifilisike.

“NDC imedhamiria kuzuia kuingizwa kwa trekta mpya kwa mujibu wa mkataba mpaka itakapojiridhisha kuwa trekta hizi hazina mapungufu yalioonekana kwenye awamu ya kwanza na zoezi hili litawahusisha pia BICO kama wataalamu wachunguzi wa NDC,” NDC imeieleza Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara.

 

Prof. Gabagambi NDC alonga

Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ameliambia JAMHURI katika uchunguzi wa habari hizi  hivi karibuni kuwa suala la rimu kuvunjika ni tatizo na akaongeza kuwa wamepata ufumbuzi:

“Yale matatizo yote yanarekebishika. Kwa sasa tunatumia KMCC Moshi, Kilimanjaro Machine Tools, tunabadilisha rims kabla hatujauza katika ku-arrest situation (kunusuru hali). Tunajitahidi kuyahudumia. Kuhusiana na yale ambayo hayajaja 1,575, hayo hatutakubali yaje bila kurebishwa kabla hayajaja.

“Defects hizi ni za kawaida, hata ukienda katika hizo akina Massey Ferguson ukiangalia kuna tatizo fulani wakati wanaanza.”

Alipoulizwa tairi kupata pancha mara kwa mara, akasema: “Ni kweli matairi yale yametengenezwa kwa ajili ya Ulaya, yamekuja Afrika, tutayarekebisha na yatatulia. Wananchi wanaomba kukopeshwa. Hadi sasa tumeleta matrekta 825, demand (mahitaji) ni kubwa sana. Na bado watu wanataka kuchukua matrekta hayo.

“Napata shaka hizi kelele za mabovu, mabovu, zisije zikawa zinatoka kwa washindani wetu ambao nina uhakika hawawezi kuuza trekta hata moja kwa sasa. Trekta kuharibika ni jambo la kawaida, maana hata barabarani tunakuta magari yameharibika.”

Alipoulizwa kama hayana shida kwa nini wameingia mkataba na KMCC ya Moshi na BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwamba gharama za matengenezo wanayofanya nani atazilipa kwani URSUS  walipaswa kuleta matrekta yasiyo na matatizo, amesema: “Tumekubaliana na URSUS kwamba watazilipa, tuendelee na marekebisho.”

JAMHURI limehoji hii URSUS kampuni iliyoko chini ya Mufilisi ikifirisiwa hizo fedha atalipa nani, Prof. Gabagambi akaongeza: “Huu ni mkataba kati ya nchi mbili, siyo mkataba kati ya URSUS na NDC. Ni jukumju la kila nchi kuhakikisha kila mtu ana-deliver (anautekeleza). Kwetu mkataba huu ulikuwa chini ya SUMA JKT, wakashindwa kuutekeleza, Serikali ya Tanzania ikauhamisha haraka sana kuja NDC ili mradi uendelee.

“Itakapodhihirika wameshindwa, ni jukumu la Serikali ya Poland kumbail-out (kumwezesha) ARSUS afufuke amalizie mradi kulingana na mkataba…”

Alipoulizwa kama Serikali ya Tanzania ameijulisha matatizo ya URSUS, akajibu: “Siyo kwamba tumekaa kimya, kuna taratibu zake za kiserikali ambazo zimeishafanywa. Zote zimeishafanywa.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Murad Saddiq, alipoulizwa na JAMHURI kabla ya kwenda mitamboni, akasema: “Kufikia saa 8 au 9 hivi nitafute. Tunaanza saa 3, naamini muda huo tutakuwa tuna kila kitu. Yote hayo unayouliza tumewataka walete majibu yake mbele ya Kamati Jumatatu (jana) asubuhi. Sasa wala usiwe na shida, nitakupatia kila kitu, nipigie muda huo.” Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni kikao kilikuwa bado kinaendelea.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ambaye awali alimsihi mwandishi kuwasiliana na Katibu Mkuu, Prof. Joseph Buchweishaija, hakukubali kujibu maswali ya JAMHURI hadi sasa. Hata Katibu Mkuu, Prof. Buchweishaija mara kadhaa alipotafutwa kuzungumzia suala hili, alitoa ahadi nzuri ya kumtafuta mwandishi atakapomaliza kikao, lakini hadi tunakwenda mitamboni ahadi hii haijatekelezwa.

 

Wakala wa URSUS

Mtanzania anayetajwa kuileta Kampuni ya URSUS nchini, Julius Zellah, hivi karibuni alipohojiwa na JAMHURI kwa nini kampuni hii imeshindwa kutekeleza wajibu wake kimkataba na kwamba imeleta matrekta mabovu nchini, amesema:

“Ule ni mradi wa Serikali ya Tanzania. Hivyo hizo habari ungewasiliana na NDC kabla hujazitoa. Mimi sikubaliani nazo kwani wakulima kadhaa wanatumia instructions (maelekezo) tofauti na manual (kitabu cha maelezo).”

Hata hivyo, Zellah amesema ni lazima URSUS walete “service van”, yaani gari la kufanya matengenezo kwa matrekta hayo ziwasaidie wakulima maeneo ya vijijini.

JAMHURI limemweleza Zellah kuwa tangu URSUS waingie kwenye msukosuko wa kufilisiwa, hawajibu barua za NDC, hawapokei simu wala kuijibu kampuni ya ulinzi inayolinda eneo la TEMCO pale Kibaha, naye akasema: “Ni kweli, juzi (wiki moja iliyopita) tulikaa na URSUS.  Wataanza kujibu kila e-mail.”

Matrekta haya yanatajwa kuwatia hasara wakulima wengi, kwani wanaingia gharama kubwa kuyakarabati kutokana na ubovu yaliyonao na wengine wameyaegesha.