Baadhi ya ndugu hulazimika kutelekeza miili ya wapendwa wao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana hali ngumu ya uchumi, JAMHURI limeelezwa.
Ndugu hao huchukukua hatua hiyo baada ya kushindwa kulipia gharama za matibabu za mpendwa wao alipokuwa akiendelea na matibabu.
Ofisa Ustawi wa hospitali hiyo, Emmanuel Mwasota, amesema idara yake imekuwa ikibeba mzigo huo kwa ajili kusaidia wanandugu wasio na uwezo wa kulipia gharama za matibabu kila mwezi na kwamba wamekuwa wakitumia kati ya Sh milioni 500 hadi Sh milioni 600 kila mwezi.
Mwasota amesema kuwa wagonjwa wenye gharama kubwa kwa sasa ni walioko kwenye uangalizi maalumu, ambao hugharimu wastani wa Sh 50,000 kwa mgonjwa mmoja wakiwa wanapatiwa dawa na huduma nyingine hospitalini hapo.
Amesema kuwa kuanzia kipindi cha mwaka 2018 na 2019 zaidi ya wagonjwa 1,500 wametelekezwa, zaidi ya hapo miili 62 ilitelekezwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya ndugu zao kukosa pesa za kulipia ‘bili’ japokuwa walikuwa wakitambuliwa na ndugu zao.
Mwasota amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2018 na 2019 idara yake imepitia na kusikiliza shida za wagonjwa zaidi ya 15,000; kati ya hao 1,284 ni wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni wagonjwa walio wengi kufikishwa hospitalini hapo wakiwa hawana ndugu na kwa wale wenye ndugu baadhi hufika siku moja tu na baada ya hapo hawaonekani tena.
“Mimi nawashangaa baadhi ya wanandugu hasa wakati wanapoleta wagonjwa kutibiwa hapa hospitalini, wakifika tu wanasema wao wana undugu na mgonjwa na baada ya mgonjwa kupokelewa na kutibiwa inapofikia hatua ya kupona au akifariki dunia wakitakiwa kulipa ‘bili’ utasikia, ‘hapana, sisi si ndugu wa mgonjwa au marehemu, ni majirani tu’, hivyo kuiachia idara majukumu ya kuhakikisha malipo yanafanyika ili kumtoa mgonjwa au mwili ukazikwe,” amesema Mwasota.
Mwasota amesema wamekuwa wakitoa matangazo na elimu sehemu zote za hospitali ili wananchi wajue umuhimu wa kuchangia huduma za afya na majukumu yao pindi mgonjwa anapofikishwa hospitalini. Hata hivyo amesema juhudi hizo hazijafanikiwa kwa kiwango cha juu.
Mwasota amesema mwaka 2016 na 2017 kulikuwa na wagonjwa 100 ambao hawakuwa na ndugu wala nauli, mwaka 2018 na mwaka huu kulikuwa na wagonjwa 129 wote hawana ndugu, lakini kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii wakapatiwa msaada wa kurudishwa katika vijiji vyao kwa usimamizi wa idara.
“Changamoto kubwa hapa na imeota mizizi ni baadhi ya maiti za Kiislamu zinakuwa na changamoto kuliko zile za Wakristo, kwani inapofikia mgonjwa ni Mwislamu amefariki dunia na ndugu wanakuja kwenye idara na kudai wameshaandaa kila kitu wanataka mwili tu wakazike, hasa unapohoji suala la kulipia bili wengi wao wanakwambia hawana, ila uwape mwili maandalizi tayari wakazike, na kwa upande wa Wakristo wanachukua muda hata ukiwaelekeza kufuata sheria wanafuata kulingana na mazingira yao,” amesema Mwasota.
Amesema pamoja na kazi kubwa wanayoifanya ya utoaji elimu, wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali zikiwemo za wanandugu kutoa miili kinyume cha sheria.
Amesisitiza kuwa suala la wanandugu kulalamika miili ya wapendwa kuhifadhiwa hospitalini hapo kwa wiki mbili hadi mwezi, hilo ni suala la kitaalamu, kwa kuwa kwa upande wao wamekuwa na utaratibu mgonjwa anapofika hospitalini lazima wamchukue vipimo, hatua hii huhitaji muda.
Mwasota amesema hospitali inajitahidi kutoa elimu kwa wagonjwa na wananchi, hivyo jitihada hizo zinatakiwa zidumishwe katika hospitali zote ili kabla ya mgonjwa kuandikiwa rufaa ya kufika Muhimbili awe na uelewa wa kutosha.
Amesema baadhi ya wajawazito wamekuwa wakilalamika dhidi ya gharama za matibabu lakini anafafanua kuwa kiwango cha kujifungua huanzia Sh 125,000 kwa mama atakayejifungua kwa njia ya kawaida, lakini wakati mwingine gharama hufikia Sh 250,000 kwa wajawazito wenye changamoto za mifumo ya uzazi.
“Kwa upande wa wajawazito wanaojifungua kwa operesheni gharama ni kuanzia Sh 250,000 hadi Sh 500,000, kama mama hana uwezo wa kulipa pesa hiyo, akilipa tu Sh 250,000 anaruhusiwa kutoka. Tatizo linakuja kwa wajawazito ambao hawajapatiwa rufaa na wanakuja kama binafsi, hawa wanalipa kuanzia Sh 500,000 na kuendelea kama atakuwa na matatizo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwasota amesema: “Kuna ndugu wanaolalamika kukosa huduma ya chakula na mambo mengine. Hao mimi nimewachoka, kuna kipindi walianzisha hata maandamano kudai kwamba wananyanyaswa, kwani hawana sehemu za kulala na hawapewi chakula wanapokuwa wakiwauguza wagonjwa wao hasa wale wa mikoani.”
Amesema utaratibu wa hospitali, mgonjwa akishapokewa na kulazwa, jukumu lote la kumpatia matibabu, vifaa na chakula ni juu ya hospitali, ndugu anapigiwa simu tu ya kuambiwa maendeleo ya mgonjwa wake.
Katika hatua nyingine, Aida Mwaisenye, Mkuu wa Kitengo cha ‘Mwochwari’ amesema kitengo hicho kimekuwa na uwezo wa kuhifadhi miili 56 kwa siku na kuitoa kwa ndugu na jamaa kwa ajili ya taratibu zinazostahili.
Mwaisenye amesema katika kipindi cha mwaka 2018 na 2019 kitengo chake kimepokea miili 140 iliyookotwa na polisi, kati ya hiyo, 20 ni jinsia ya kike, wengi wao wakiwa watoto wachanga waliotupwa vichakani na wazazi wao.
Amesema miili inayoletwa katika kitengo chake wengi ni wenye umri kati ya miaka 21 hadi 30 na wamekuwa na utaratibu wa kuhifadhi miili hiyo kwa takriban siku 21.
Salma Ali, ni mmoja wa ndugu walioleta mgonjwa kutibiwa katika hospitali hiyo, anadai mgonjwa wake ameletwa katika hospitali hiyo tangu Juni 3, mwaka huu akiwa na shida ya kutokwa damu sehemu za siri baada ya kugongwa na trekta huko Morogoro. Anadai waliambatana na watu watatu wasio na ndugu, na pesa zimewaishia.
Amesema kuwa tangu kipindi hicho mgonjwa wao amekuwa akitibiwa lakini changamoto inayowakabili ni kwamba wanahitaji kulala, kula na kufua.
“Yaani pesa tulikuja nazo kama milioni mbili lakini kutokana na changamoto za kula, kufua na mahitaji mengine pesa hiyo imetuishia kabisa, tunafikia hata kula sahani moja watu watatu kwa mlo mmoja, kwa kweli watusaidie serikali kuangalia hili,” amesema.
Naye, Sijawa Jafari, mkazi wa Songea, amesema mgonjwa wake ametimiza miezi kadhaa tangu afikishwe Muhimbili, Juni 27, mwaka huu, akiwa anakabiliwa na changamoto katika mfumo wa ulaji chakula.
Amesema kuwa mgonjwa huyo ni mume wake, alipata ajali ya pikipiki na kuvunjika uti wa mgongo, akatakiwa kulipa Sh 200,000, na baada ya hapo alitakiwa kulipa Sh 3,200,000 ili kumfanya mgonjwa huo awekewe vyuma.
“Mimi nataka wagonjwa wote wanaopewa rufaa ya kuja hapa Muhimbili kutibiwa, akija na muuguzi wake tutengewe sehemu ya kulala, kula, kujisaidia na kufua na gharama kama zimekuwa kubwa wasaidiwe ili iwe rahisi kwetu sisi wauguzaji,” amesema.