Jifunze‌ ‌kuamka‌ ‌mapema‌

“Kama una ndoto ya kuajiriwa, usilale hadi saa moja.”  alisema Ruge Mutahaba akiwa mkoani Mbeya katika fursa mwaka 2017. Linaweza kusikika kama jambo geni, lakini watu waliofanikiwa kwenye sekta mbalimbali ni watu waliojijengea tabia ya kuamka mapema.

Msemo wa Ruge Mutahaba nilioanza nao hapo juu si tu maalumu kwa watu wanaotaka kuajiriwa ,  bali kila mtu anayetaka mafanikio na mwenye ndoto.

Kama kila mmoja angejua thamani ya kuamka mapema ,  basi watu wengi wangekuwa wamefika mahali pakubwa sana.

Huwa najiuliza nchi za wenzetu zinaendeleaje na sisi tunabaki nyuma? Lakini ukweli ni kwamba wenzetu wanajali mno muda. Tazama Wachina na Wajapani muda mwingine hawalali wakifanya kazi usiku kucha.

Hakuna uchawi katika mafanikio!

Siku moja wakati nimeandika makala iliyokuwa na kichwa cha ;  ‘Dalili 12 za kijana anayechelewa Kufanikiwa’ niliandika maneno haya: “Usiamke mapema. Unawahi kuamka ili ugundue nini?” Watu wengi walicheka, lakini nia yangu ilikuwa siyo kuchekesha.

Jifunze kuamka mapema na jenga tabia ya kuamka mapema kila siku iitwayo leo.  “Maisha huanza asubuhi,” anasema Joel Osteen. Na kama kweli maisha huanza asubuhi je, wale watu wanaoamka saa 6 mchana? Jibu lipo wazi ni kana kwamba wamepoteza maisha.  “Panzi anayelala sana huamka na kujikuta kwenye mdomo wa mjusi,” wanasema Waigbo wa Nigeria. “Kulala mapema na kuamka mapema hutengeneza siku njema.”  (Msemo wa Kiingereza) Ripoti iliyoandikwa kwenye jarida la Wall Street inasema muda muafaka wa kuamka ni saa 10 alfajiri. Ingawaje kuna watu wameweza kuamka hadi saa 9. Robin Sharma anasema, “Saa 11 alfajiri ni muda wa magwiji kuamka.”

  

FAIDA ZA KUAMKA MAPEMA:

Huongeza uzalishaji

  Mtu hupata saa  za ziada. Wakati wengine wanafanya kazi saa 8 wewe unaweza kufanya  hadi saa 18.

Mfano mzuri ni Aliko Dangote ambaye hufanya kazi saa 18 kila siku. Ukiamka saa moja kabla ya muda  wako wa kawaida kila siku, utakuwa na jumla ya saa saba ndani ya wiki moja, kwa mwezi ni saa 30. Muda huo unatosha kufanyia kazi ndoto na  maono yako na unaweza kufanya makubwa.

  

Huongeza ubunifu

Watu wanaoamka mapema wana sifa ya kuwa wabunifu katika kazi zao.   

  

Hupunguza msongo wa mawazo

Ukipata muda wa ziada ni rahisi kumaliza kazi zako zote kwa muda na kila siku husika. Mtoto mmoja aliwahi kumuuliza mama yake kuwa mbona baba yake hurejea nyumbani na kuendelea kufanya kazi za ofisini akiwa nyumbani wakati wa usiku? Mama yule alimjibu mwanae, “Baba yako hawezi kufanya kazi zake zote ofisini. Lakini shida kubwa baba huyo hakujua matumizi sahihi ya muda wake. ”

Usumbufu unakuwa haupo: au kama upo, basi ni kidogo sana (kwa watoto, kazi na kelele)

Hakuna anayekutumia barua pepe  (e-mail), meseji au anayewasiliana na wewe.

Kuna machache tu ya kutizama kwenye mitandao ya kijamii:

Mojawapo ya vitu vinavyotupotezea muda ni mitandao ya kijamii. Mtu anaweza kushinda Facebook, Instagram au WhatsApp,  lakini hakuna lolote la faida analolipata.

Utapata muda na wakati mzuri wa kusali :   na kumshukuru Mungu kwa kukuwezesha kuiona siku mpya na pia utapata muda mzuri wa kufanya tafakari ya maisha yako.

Utapata muda wa kusoma vitabu na kupata maarifa ambayo yatakufanya usonge mbele zaidi:  Watu wengi huwa nikiwaambia soma vitabu wanasema  hawana muda. Ukijenga tabia ya kuamka mapema huwezi tena kusema muda hakuna.   

Ukiamka mapema utapata muda wa kufanya mazoezi na kuijenga afya yako.

Kwa wanafunzi, muda wa asubuhi na mapema huwa ni muda mzuri wa kusoma kwani ubongo  unakuwa kama sponji (tabia ya kufyonza) na  kuweka katika akili kwa wepesi zaidi yale unayokuwa ukiyasoma. Hii ni kutokana na uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Chuo  Kikuu cha California, Berkeley nchini Marekani walioongozwa na Dk. Mathew Walker.

Hasara kubwa na mbaya kuliko zote ya kutoamka mapema ni kwamba ukiwa mtu wa kulala sana unaukaribisha umasikini.

“Ewe mvivu, utalala hapo mpaka lini? Utaamka lini katika usingizi wako? Wasema “Acha nilale kidogo tu, acha nisinzie kidogo! Niache nikunje mikono nipumzike kidogo!” Wakati huo umasikini utakuvamia kama mnyang’anyi, ufukara utakufuata kama jambazi.” (Methali 6: 9-11)