Juma lililopita, nilitoa pongezi kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa Septemba Mosi, 1964.  Ukweli Jeshi hili liliasisiwa baada ya Jeshi la Tanganyika (Tanganyika Rifles-TR)  kuasi Januari  20,1964.

Naweza kusema jeshi lile lilifanya kazi kutokana na kasoro za imani na misingi ya kuwako kwake.  Lilikuwa bado lina imani ni jeshi la mabwana na si la wananchi.  Jeshi la kulinda wakubwa na kunyanyasa wananchi.

Kwa mtazamo wa nje na utaratibu wa jeshi na kisiasa, nathubutu kusema sababu zile zilikuwa na kasoro kubwa kwa wananchi walioamua kuwa huru kiuchumi, kiutamaduni na kiulinzi.  Hivyo, uamuzi wa kujenga Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni muhimu sana.

Kama nilivyosema wiki iliyopita, Rais wa Kwanza wa Tanzania Huru, Mwalimu  Julius K. Nyerere, aliamua kujenga Jeshi Huru la Wananchi kwa kuwaelimisha wanajeshi hao nia, madhumuni na malengo ya jeshi kwa nchi na wananchi.

Madhumuni na malengo hayo hayakuishia kwa wanajeshi tu, bali yalifika hadi kwa wananchi wa Tanzania.  Kwa lugha fasaha, wananchi wamekuwa sehemu ya jeshi na wanajeshi wamekuwa sehemu ya wananchi.  Wote ni wamoja.

Jitihada kadhaa zilifanywa kuwafunda wanajeshi kutambua, kujali na kuthamini nchi yao na ndugu zao.  Kiranja Mkuu, Mwalimu Nyerere na Fumbi la nyuma, Sheikh Abeid Amani Karume, walihakikisha wanajeshi hao wamefundika.

Septemba Mosi, 1969 katika sherehe ya maonesho ya Jeshi, Mwalimu Nyerere alitoa hotuba iliyohusu chuo cha ulinzi na ujamaa.  Baadhi ya mafunzo aliyotoa kwa wanajeshi na wananchi ni juu ya uzalendo.

Alisema, “Askari wako aina mbili …. Wako askari wa fedha, ukimuuliza “Kinakuweka nini hapa? Atasema “Nalipwa, hapa kuna tija, mshahara mzuri.” Ndiyo unaomweka hapa, huyu askari fedha. Huitwa Mercenary; yuko tayari kufa, yuko tayari kuua, kwa sababu ya fedha anayolipwa.

Wa pili askari mzalendo, naye anasema lazima alipwe mshahara, ale, lazima avae, lazima atengenezewe kajumba. Lakini hayo siyo yanayomweka hapo; yeye yuko pale analinda nchi yake, anaipenda nchi yake; yeye yuko pale tayari kufa kama hapana budi; si kwa sababu ya fedha; ila kwa sababu ya nchi yake.  Huyo ni askari mzalendo; ndiye tutakayemtaka sisi.”

Maneno hayo ni fundo kubwa kwa wanajeshi wetu hata kwetu sisi tusio wanajeshi.  Ndiyo maana leo tunalipenda na kushirikiana na jeshi letu katika ulinzi na ujenzi wa Taifa kisiasa na kiuchumi.

Kabla ya kukamilisha makala ya pongezi kwa Jeshi la Wananchi,  nikumbushe hotuba mbili zilizowahi kutolewa na Amri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius K. Nyerere, alipozungumzia kuhusu moyo kabla ya silaha na kuwa kama Bwana.

Ni Februari 26, 1970 katika sherehe ya wanajeshi, Zanzibar; Mwalimu Nyerere aliwajenga imani vijana walio jeshini kuhusu imani ya moyo na matumizi ya silaha kipi kitangulie kutumika kabla mbele ya wananchi.

Mwalimu alisema,  “Tunaunda jeshi hili la wakulima na wafanyakazi; Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, jeshi la kumkabili adui wa Tanzania; lakini nitafurahishwa zaidi na moyo wa ujamaa kuliko silaha tu.

Moyo wa wananchi, wakulima na wafanyakazi, utafurahishwa zaidi wakiamini kuwa jeshi lao ni la kijamaa.  Hawawezi kufurahia silaha, bila ya kuwa na hakika ya nyoyo za wale wenye kusimamia silaha zile.

Namaliza kwa kusema Kiranja Mkuu, Mwalimu J. K. Nyerere, alipokuwa anafungua semina ya maafisa wa jeshi, Bagamoyo, Novemba 24, 1970 alisema; lazima uhuru wetu uwe uhuru wa moyoni, wa mtu kukubali na kuthamini utu wake.

Kazi yetu ya kwanza kabisa ni kukataa kabisa kuwa running dogs; sisi ni watu; Tuko tayari kufanya urafiki na watu, lakini running dogs hapana.  Kila siku tunataka uhuru wa kudumisha mila zetu, tunataka uhuru wa mambo ya siasa, na tunataka uhuru wa kuendeleza imani yetu.  Lakini hatuwezi kuwa running dog.” Je , wewe mwenzangu uko wapi?

 

0717/0787 – 113542