Ndugu Rais, Watanzania wa leo wengi wana fikra nzito kuliko baadhi ya waheshimiwa. Nimetumiwa meseji mbili. Ya kwanza mwandishi anasema amesukumwa na makala yangu niliyoiandika miaka tisa iliyopita ikiwa na kichwa cha habari, “Rais wangu Kikwete kwaheri ya kuonana wapambanaji wetu.” Akaandika, “Kama ningalikuwa na uwezo wa kumfikia Mheshimiwa Rais ningemwambia neno moja. Nalo ni hili -wakati wenzako watakuwa na kazi moja tu katika muhula huu wa kujitengenezea mitandao kwa ajili ya urais wa mwaka 2015, wewe mtandao wako uwe ni barabara. Jenga barabara kwa kasi kubwa, Watanzania wa 2015 watakuwa tofauti na wa leo. Barabara hizi zitakuja kukusemea na zitakuwa ndio mtandao wako.”

Baba Mayega hayo siyo maneno yangu, ni andiko lako mwenyewe katika gazeti la Jumatano Desemba 1, 2010. Sasa mbona uliyemtabiria urais, leo hajali maono yako? Barikiwa zaidi mbarikiwa.’’

Huyu kanikumbusha mwaka 2005 nilipokufuata ofisini kukutaka ukachukue fomu ya kugombea urais, ushindane na wana mtandao. Ndiyo kusema mapenzi yetu kwako ni ya ukweli tangu zamani, siyo kwa sababu ya urais wako.

Ndugu Rais, Katibu Mkuu wa chama chako aliyepita alipokuja nyumbani kwangu, aliniambia, “Bwana Mayega nimetumwa na Rais nije nikuulize ungependa uwe nani katika nchi hii?’’ Nilimwomba akamshukuru Rais kwa heshima kubwa aliyonipa. Nikamwomba akaniombee Rais aniache hivi hivi niliyo. Vivyo hivyo baba ninakuja kwako. Nitaendelea kukulilia siyo kwa chochote unipatie mimi, bali wasikilize masikini wa nchi hii! Wananchi wameteseka vya kutosha.

Ujumbe mwingine ulisomeka, “Baba ni nani? Ni hao waliomwambia Mfalme Utukufu wake ni asubuhi hadi jioni njia nzima hadi alipotokeza mtoto anayeshangaa sherehe na kusema, jamani eehhh mfalme yuko uuu…’’ Wazungu waliamini kuwa Mwafrika ni mtu wa machakani. Unaweza kumtoa kutoka katika kichaka, lakini huwezi kutoa kichaka kilichomo ndani ya kichwa cha Mwafrika.

Tulichekelea kuwatoa wapinzani kutoka upinzani bila kuelewa kuwa huwezi kutoa dhana ya upinzani kutoka katika kichwa cha mpinzani. Tuliwachukua wengine tukawafanya naibu waziri, wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa. Hata wengine tukawatuma katika mataifa wakawe mabalozi. Nilikuandikia baba kuwa haya tunayoyafanya ni kwa hasara yetu wenyewe, lakini yaonekana sikusomeka vizuri. Nafurahi leo Dk. Slaa amenifanya nisomeke vizuri. Mpinzani aliyebobea, padri, daktari na balozi Willbrod Slaa ameiletea nchi hii ufunuo wa kutetemesha! Anasema kule, yeye ndio Tanzania. Amesema kweli. Anatushtakia eti Bunge la Ulaya limeihukumu Tanzania bila kuipa nafasi ya kujitetea.

Kisha akaeleza kuwa baada ya tuhuma za kuichafua nchi kuwafikia hao wafadhili walimwita na kumhoji. Hiyo haikuwa nafasi ya Tanzania kujitetea? Alitaka aitwe nani ndiyo iwe imeitwa Tanzania? Anadai alichofanya katika mahojiano hayo ni kufafanua tu. Lakini hata mara moja hakusema kuwa alikanusha kuwa tuhuma hizo zinazoichafua nchi yetu si za kweli. Hakukanusha kuwa vyama vya upinzani vimezuiwa kufanya mikutano na shughuli nyingine za kisiasa nchini. Hakukanusha hata mara moja kuwa si kweli watu Tanzania wanatekwa, wanateswa, wanapigwa risasi na wengine kupotezwa. Hakukanusha kuwa baadhi ya wapinzani wanafunguliwa kesi za kughushi! Sasa alichowafafanulia ni nini? Namna watu wanavyouawa au kupigwa risasi? Alifafanua jinsi mikutano ya vyama vya siasa inavyozuiwa? Alitarajia hukumu isomeke vipi? Akitusisitizia alisema ulimwengu mzima, umetangaziwa na Bunge la Ulaya kuwa Tanzania ya leo haifai kwa uwekezaji, haifai kufanya nayo biashara yoyote na haifai kabisa kwa utalii! Na sisi bwana. Katika hali kama hii tunaagizaje ndege nyingine tatu wakati sasa hata hizi tulizonazo watalii wamekatazwa kuzipanda?

Hukumu hiyo ya Bunge la Ulaya hao wakuu wa nchi za SADC wenyewe hawajaisikia? Hao si ndiyo hao hao wafadhili wao? Wataenda kinyume cha makatazo ya wafadhili wao? Na kwanini bwana Slaa aje alisisitize hili hapa wakati huu huku akijua kuwa viongozi wakuu wa SADC wako hapa kwenye mkutano?

Msondo ngoma waliimba, ‘Kupamiapamia sasa tumepamia jabali.’ Kwa Slaa baba tulipamia mwamba. Aliposema utetezi ulikuwa mgumu zaidi kutokana taarifa zilizotoka humu ndani nikamkumbuka mzee wangu Hamis Kagasheki. Alisema alishtuka kumsikia Rais akiwaita baadhi ya mawaziri kuwa ni wapumbavu, lakini aliposikia mahojiano ya baadhi yao akasema Rais alikuwa sahihi.

Baba, kama mwenyewe unaona kuna wapumbavu, Rose Mhando wa nyimbo za Injili aliimba, ‘Epuka vikao vya wapumbavu.’ Unatarajia ushauri gani wa maana kutoka kwa mtu uliyemuweka peponi baada ya kumtoa jalalani zaidi ya kusema ‘ewala bwana kwa kila kitu?’

Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba katika maisha yangu ya kielimu, alinifikisha mpaka ngazi ya juu kabisa kuelekea upadri. Dk. Slaa ni padri aliyehitimu vizuri masomo yake ya filosofia. Kusema alivyosema na mahali aliposemea alijua analenga nini. Alilelewa katika upadri. Haiwezekani roho yake ya kipadri isiguswe na uovu uliotendeka. Ni ujumbe ambao umewakaanga kabisa wenye mamlaka baada ya kuwajulisha wananchi dhiki kuu itakayowashukia muda si mrefu kutokana na laana ya kuhukumiwa na dunia. Laiti, wangekuwa na upeo wangemrudisha akaendelee kuuza duka. Yawezekana vipi msomi huyu asijue tofauti kati ya nchi na serikali? Kuichafua serikali siyo kuichafua nchi. Serikali huja na kupita ,lakini nchi hubaki. Aliupimaje upeo wa wenye mamlaka?

Kimataifa hali hii ilianza kulalamikiwa katika Bunge la Afrika Mashariki jijini Arusha. Mbunge kutoka Kenya alidai kuwa baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika Mashariki ni madikteta. Akaahidi kuwa iwapo Mungu atawajalia uhai na wakaja kushika nafasi za uamuzi nchini mwao viongozi wa aina hiyo hawatashirikiana nao. Kama ndani ya Bunge hilo wawakilishi wetu walikuwapo na hawakusema kitu ni kwamba nao maovu haya yamewadumaza. Hatuioni sababu ya kujisahihisha? Lakini hawa wenye Bunge la Ulaya si ndio hawa hawa wenye mahakama ya ICC? Kama Bunge lao limetuhukumu, mahakama yao itatuachaje?

Dk. Slaa amewafanya wananchi wawahofie viongozi wao kuwa wanaweza kuitwa ICC. Baadhi ya viongozi wa nchi za wenzetu walipokabiliwa na hali kama hii walilazimisha utawala wa maisha.