Maisha huwa hayana maana iwapo mwanadamu anaishi tu, siku nenda, siku rudi bila ya kugundua au kujifunza japo jambo moja jipya kila siku. Uamkapo asubuhi, utembeapo barabarani, ulalapo kitandani yafaa ujiulize: ‘Unaishi na mawazo yanayoishi au yaliyokufa?’
Maisha ni kufikiri, binadamu wote tuna fursa ya kufikiri, haijalishi unafikiri nini, lakini unafikiri. Kinachotokea katika maisha yetu hakitokei nje ya kufikiri kwetu. Jemedari Napoleon Bonaparte (1769 – 1821) aliyepata kuwa mfalme wa Ufaransa, alisema: “Yupo aina moja ya jambazi ambaye sheria haipambani naye, lakini ndiye mwizi wa kilicho cha thamani kubwa kwa mwanadamu – ni muda.”
Ninaomba kuuliza swali, kama leo ndiyo ingekuwa siku yako ya mwisho ya kuishi hapa duniani ungefanya nini? Tafakari. Martin Luther kwa upande wake alisema: “Hata kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho bado ningefanya kazi ambayo ingezaa matunda kwa ajili yangu au kwa anayekuja nyuma yangu.”
Jana iliyopita hauwezi ukaifufua, wiki iliyopita hauwezi kuifufua, mwezi uliopita hauwezi ukaufufua, vivyo hivyo mwaka uliopita hauwezi ukaufufua. Ukipoteza muda, muda utakupoteza zaidi. Napoleon alizoea kuwaambia wanafunzi wake: “Kila saa unayopoteza ni fursa ya kuwa na balaa badaye.”
Alfred Montapert anasema: “Ukichagua kuchezea muda hauwezi kukwepa matokeo yake ambayo siku zote ni mabaya tu.” Waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa wote wanatumia saa 24. Wote wamo ndani ya siku 365 za mwaka.
Tofauti ya jina la tajiri na maskini inapatikana katika matumizi ya muda. Wakati wote muda ni rafiki wa ‘mafanikio’, pia ni adui wa ‘mafanikio’. Tuutumie muda vizuri maana muda ni mali.
Ni vizuri kuthamini muda, ukitaka kujua umuhimu wa mwaka mmoja muulize mwanafunzi ambaye amerudia darasa. Ukitaka kujua umuhimu wa mwezi mmoja muulize mwanamke ambaye amejifungua mtoto kabla ya mwezi mmoja. Ukitaka kujua umuhimu wa juma moja muulize mhariri wa gazeti linalotoka kila wiki.
Ukitaka kujua umuhimu wa siku moja muulize mtu mwenye kibarua cha kulipwa kwa siku wakati ana watoto kumi wa kulisha. Ukitaka kujua umuhimu wa saa moja waulize wachumba ambao wamepanga kukutana baada ya saa moja kufunga ndoa.
Ukitaka kujua umuhimu wa dakika moja muulize mtu ambaye ameachwa na gari stendi. Ukitaka kujua umuhimu wa sekunde moja muulize mtu ambaye ameponea chupuchupu katika ajali. Ukitaka kujua umuhimu wa milisekunde muulize mtu ambaye ameshinda medali ya fedha katika mashindano ya mbio.
Kila siku unayopata kuishi hapa duniani ina umuhimu wake. Methali ya Kifaransa inasema: “Hazina zote za duniani haziwezi kurudisha fursa moja iliyopotea.”
Ndiyo kusema, utajiri wote wa ulimwengu hauwezi kurudisha nyuma dakika moja iliyopotea. Liwezekanalo leo lisingoje kesho. Mchezaji wa mpira, Jerry Rice, anasema: “Leo nitafanya ambayo wengine hawatataka kufanya ili kesho niweze kutimiza ambayo wengine hawataweza kutimiza.”
Hauwezi ukashinda kama hauchezi, mwanadamu anaishi mara moja tu hapa duniani. Tunaloweza kulifanya sasa, tulifanye kwa sababu hatuishi mara ya pili hapa duniani. Kubahatika kuishi duniani ni fursa.