Ukiomba mvua usilalamike kuhusu matope
Kulalamika ni mtihani. Unaweza kulalamika kuwa maua aina ya waridi yana miiba au kusifu kuwa miiba ina maua. Kuna mtoto aliyewalalamikia wazazi kuwa hawamnunulii viatu.
Aliacha kulalamika alipoona mtu ambaye hana miguu, kuna makundi ya watu yanayolalamika kila mara: wale wasiopata wanachokistahili na wanaopata wanachokistahili.
“Baadhi ya watu wanalalamika kila mara; kama wangezaliwa kwenye Bustani ya Edeni, wangetafuta mambo mengi ya kulalamikia,” alisema John Lubbock.
Jambo la kufahamu ni kuwa huwezi kuwa na tamu bila jasho, huwezi kuwa na furaha bila huzuni, huwezi kuwa na maisha bila kifo, huwezi kuwa na maisha bila maumivu na huwezi kuwa na mvua bila matope.
Kwa baadhi ya watu ninakubaliana na maneno ya William Arthur Ward, “Ulimi unaolalamika unadhihirisha moyo usio na shukrani.”
Mwanasaikolojia alipewa kibarua cha kujua mtazamo wa mapacha wa kiume; Esau na Yakobo. Aliwaambia wazazi wao wawanunulie zawadi siku ya kuzaliwa kwao.
Esau alinunuliwa kompyuta kubwa ya mezani, alilalamika na kusema: “Mngeninunulia kompyuta ndogo ya kiganjani -palmtop.” Yakobo alipewa gunia la samadi, alifurahi sana na kusema: “Nafurahi sana maua yetu nitayawekea mbolea. Hii ina maana kuna ng’ombe mahali fulani huenda tutakunywa na maziwa kila mara.”
Yakobo alikuwa na mtazamo chanya, Esau alikuwa na mtazamo hasi. Wakati mwingine mtazamo hasi husababisha kulalamika.
Wafanyakazi kwenye Shirika la Posta la Marekani walipokea barua iliyokuwa imeandikwa juu, ‘Barua kwa Mungu’. Baada ya kuifungua walikuta ombi kwa Mungu la dola mia tano. Wafanyakazi waliamua kutomkatisha tamaa muombaji, walichanga na kumtumia dola mia nne hamsini.
Baadaye mtu huyo alituma barua nyingine kwenye posta, mlengwa akiwa Mungu. Wafanyakazi wa Shirika la Posta waliifungua. Ilikuwa imeandikwa hivi: “Mwenyezi Mungu nipitishie pesa kwa shirika jingine. Shirika la Posta wamechukua dola hamsini zangu.” Muombaji huyo ukisoma katikati ya mistari alikuwa mlalamikaji tu.
“Ulimi unaolalamika unadhihirisha moyo usio na shukrani,” alisema William Arthur Ward. Kuna methali isemayo: “Ukishibisha sana tumbo linakukaba koo.” Watu unaowatendea mema ndio watalipa mema kwa mabaya.
Kila mara tazama jambo zuri ambalo uwepo wake unakufanya utoe shukrani. Badala ya kulalamikia msongamano wa magari, shukuru kwamba una gari. Badala ya kulalamika kuwa vyombo vya kuosha baada ya mlo ni vingi, shukuru kwamba kuna aina nyingi za vyakula, mapochopocho ni mengi na kuna watu wa kula chakula.
John alikuwa na mbwa aliyemuita ‘mjomba Joe’. Alipoulizwa kwanini alimpa mbwa jina kama hilo, alijibu: “Ni kwa sababu ni kama mjomba wangu, anaguna kwa aina ya chakula chochote anacholetewa na anataka kugombana na mtu yeyote anayekutana naye.”
Kuna hadithi ya mchota maji, alikuwa akichota maji na kuyapeleka kwa mfalme, alitumia mitungi miwili. Mtungi mmoja ulikuwa na nyufa, hivyo maji yalimwagika njiani. Mtungi huo ulilalamika kwa maana ulifikishwa nyumbani bila chochote.
Mtungi mwingine ulifikishwa nyumbani umejaa maji, mchota maji aliuambia mtungi uliokuwa unalalamika, tazama nyuma yako maua yanavyopendeza. Nilipanda mbegu za maua njiani baada ya kuona kuwa una nyufa na umekuwa ukizimwagilia, Mungu anaweza kutumia nyufa zetu kutoa jambo zuri.
Tutafakari maneno haya ya busara ya mtu fulani. “Leo kwenye basi niliona msichana mzuri sana akiwa na nywele za dhahabu. Nilimwonea wivu, alionekana mzuri sana nami nilifikiri kama ningekuwa mzuri kama yeye. Ghafla aliposimama kuteremka alikuwa na mguu mmoja na gongo la kutembelea, aliponipita alitabasamu. Ee Mungu, nisamehe ninapolalamika. Nina miguu miwili.