Kudhani kwamba Lazaro Nyalandu hayumo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kujidanganya. Bado yumo. Mtandao wake upo, na unafanya kazi kweli kweli. Baadhi ya waliokuwa wasaidizi wake leo ndio wenye uamuzi wa nani anyang’anywe, au nani apewe kitalu.

Kudhani kwamba ugawaji wa vitalu kwa mnada/mtandao kunasaidia mambo, ni kujidanganya. Mfumo ndiyo mbaya kuliko hata ule wa kamati. Hili nitalieleza kwa vielelezo mbele ya safari.

Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Dk. Hamisi Kigwangalla, anayofanya mengi yanaonyesha tofauti yake na Nyalandu, lakini mahali pekee wanapopatanishwa na kuwa ‘marafiki’ ni kwenye kuzibeba kampuni za Friedkin Group (FG) – yaani Wengert Windrose Safaris Ltd (WWS), Tanzania Game Trackes Safaris Ltd (TGTS) na Mwiba Holding.

Waziri ametangaza kuifuta Kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Green Mile Safaris (GMS) kwa makosa ya kuunda. Kifungu cha sheria alichonukuu kuhalalisha alichofanya kwa kampuni hii kinaeleza makosa yanayoweza kumfanya waziri akafuta leseni; na pia taratibu za kufuata kufikia hatua hiyo. Kifungu 38(13) cha Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kinasema: “No decision to cancel the allocation of a hunting block shall be made until the person concerned has been given an opportunity to be heard.” Nina shaka kama Dk. Kigwangalla amezingatia kifungu hiki muhimu kinachomtaka ampe nafasi hiyo mlalamikiwa ya kujitetea. Hapa pekee waziri ameshakwama, na haya ndiyo matokeo ya uonevu. Uonevu husababisha upofu hata kwa lililo la wazi.

Je, upofu huu wa kisheria ni wa bahati mbaya? Jibu ni hapana. Waziri anajua anachofanya. Wasaidizi wake walioko TAWA wanajua nini wanakitaka hata kama ni kwa kumpa uongo waziri.

Nini kimeandaliwa?

Hii sinema yooote ni geresha tu. Mpango ni kuhakikisha kitalu cha Lake Natron East wanapewa Wamarekani hawa wa Friedkin kwa maana ya Kampuni ya WWS. Waziri alipotoa barua ya kuwafutia leseni GMS, WWS walikunywa mvinyo. Wakashangilia kweli kweli.

Hawa hawa wanaopewa kitalu hiki wameshaisumbua sana serikali na wadau wengine. Taarifa za usumbufu wao zimeainishwa na mawaziri wengi waliopita. Lakini si kitalu hiki pekee kilicho kwenye rada za Wengert.

Kitalu kingine wanachokitaka kwa udi na uvumba ni cha Maswa, ambako kuna kampuni nyingine ya Mtanzania. Huu ndiyo ukweli ambao watu wanapaswa kuupata. Hawa wanaonyang’anywa vitalu ni Watanzania. Tumelogwa na nani? Kwanini Watanzania sisi wenyewe kwa wenyewe tunamalizana kwa fitina?

Zinatumika hoja nyepesi kuwanyanyasa Watanzania hawa. Kwa mfano, GMS ananyanyaswa kwa sababu ya rekodi ya baadhi ya wageni wake waliowinda miaka mingi iliyopita. Wanatumia hoja nyingine kwamba amekataa kuvilipa vijiji fedha za maendeleo. Hivi kweli yupo mtu mwenye akili timamu katika zama hizi za Rais John Magufuli anayeweza kutunisha msuli akakataa kulipa stahiki zilizopo kisheria? Nani ana ubavu huo? Hawa ‘wachovu’ GMS ndio wa kuigomea serikali kuilipa inachokitaka kama ni cha kisheria?

Mtandao wa kuwang’oa GMS ni mpana. Mrisho Gambo akaaminisha umma kuwa GMS wanashiriki ujangili wa twiga. Taarifa ya serikali ikatoka na majibu kuwa twiga hawafi kwa ujangili, bali kwa kimeta!

Upotoshaji wote unatungwa kuhalalisha Watanzania wafukuzwe ili Wamarekani wapewe vitalu. Shida hapa ni kitalu cha Lake Natron East ambacho Wamarekani wanakililia usiku na mchana; na kifuatacho ni kitalu cha Maswa Mbono.

Kampuni za WWS, TGTS na Mwiba Holding ambazo ni mali za Friedkin Conservation Fund (FCF) zina rekodi mbaya. Nitaeleza kwa ufupi.

Miaka kadhaa iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitaka uchunguzi ufanywe na apewe ripoti kutokana na malalamiko ya wanakijiji kuhusiana na vitendo vya unyanyasaji vilivyokuwa vinafanywa na Kampuni ya Mwiba Holdings iliyojimilikisha kinyemela eneo la Mwiba mkoani Simiyu na kuliita Mwiba Ranchi, huku likiwa halikidhi kabisa vigezo vya kuwa ranchi ya wanyamapori.

Matakwa ya kampuni hiyo kupewa haki ya matumizi ya eneo hilo kama ranchi yalikataliwa kwa msingi wa kukosa vigezo na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, huku aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyalandu, akiwashinikiza wakurugenzi wa wanyamapori wakiuke amri ya waziri wake na kutoa haki hiyo ya matumizi kwa rafiki zake hawa.

 Baada ya kufanikiwa kurithi mikoba ya Balozi Kagasheki, Nyalandu alihakikisha kuwa kila walichokitaka Wamarekani hawa wababe wanakipata ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuilazimisha Kampuni ya Fereck Safaris iliyoshinda zabuni ya kitalu cha uwindaji cha Makao WMA wakiachie ili awazawadie rafiki zake hawa. Japo kitalu hicho alikigawa kwa Kampuni ya Mwiba Holdings, kampuni hiyo haikuwa imeandikishwa kama kampuni ya uwindaji.

Aidha, Nyalandu alihakikisha kuwa anabariki matumizi ya eneo la Mwiba kama ranchi kinyume cha kanuni za uanzishwaji wa ranchi ya wanyamapori. Ujasiri wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alex Songorwa na msaidizi wake, Profesa Japhary Kideshesho, kumkatalia Nyalandu kuvunja sheria za wanyamapori uliwagharimu, kwani Nyalandu aliwafukuza kazi mara tu baada ya kupata uwaziri.

Hata hivyo, amri ya Nyalandu kunyang’anya kitalu kilichokuwa kinatakiwa na Wamarekani hawa kupitia Kampuni ya Wengert Windrose Safaris ilikwama na ndipo Nyalandu akishirikiana na Wamarekani hao na Peter Msigwa walipounda njama ya kunyang’anya kitalu hicho kutoka kwa mmiliki halali ambaye ni Green Mile Safaris. Walidai kuwa GMS imekiuka sheria za uwindaji na kumfutia leseni zote za uwindaji. Hata hivyo, si Mwindaji Bingwa (PH) au msimamizi wa idara aliyechukuliwa hatua kutokana na kosa hilo. Kimsingi, PH na msimamizi wa idara ndio waliotakiwa kuhakikisha kuwa sheria zote za uwindaji zinafuatwa vilivyo.

Baada ya kuifutia Kampuni ya GMS leseni ya uwindaji, Nyalandu aliamua kukigawa kitalu kilichokuwa kinamilikiwa na GMS kwa Kampuni ya WWS [Wamarekani]. Ni kipindi hiki hiki ambacho Nyalandu aliamuru kutoa Leseni ya Rais kwa Wamarekani hawa kinyume cha sheria akiruhusu marafiki zake waue wanyamapori 708 wakiwemo tembo na simba. Leseni ya siku 21 ikatolewa Agosti 01, 2014. Familia ya watu wanane wakiwamo watoto ikaruhusiwa kuua wanyama wetu bila kulipa hata senti moja serikalini. Waliokuja ni Thomas Dan Friedkin, Thomas Hoyt Friedkin, Susan Fridkin, Debra Friedkin, Thomas Dan Friedkin Jr, Ryan Friedkin, Corbin Friedkin; na Savannah Friedkin.

Hapakuwapo maelekezo ya rais ya kutoa kibali hicho. Tena basi, mwaka huo hapakuwapo Leseni ya Rais, bali Leseni Maalumu! Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 lilihusu uwindaji kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 1974 ambayo iliruhusu uwepo wa Leseni ya Rais. Sheria Na. 12 ya mwaka 1974 ilifutwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2009. Katika Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 hakuna Leseni ya Rais, bali kuna Leseni Maalumu na malengo yake ni tofauti. Hawa Friedkin walioshiriki udanganyifu huu, leo ndiyo wanabarikiwa wapewe Lake Natron East.

Wakachagua maeneo/vitalu vya kuua hao wanyama. Hayo maeneo waliyopendekeza wanayopigania hadi sasa yawe yao. Miongoni mwayo ni Maswa Mbono na Lake Natron East. Maeneo waliyoomba na kukubaliwa ni Maswa Mbono GR, Maswa Kimali GR, Makao WMA, Makao Open Area (waliyoigeuza kuwa ranchi), Lake Natron GCA East; na Lake Natron GCA North.

Walipokuja, watoto wadogo wakawinda kinyume cha sheria. Ikumbukwe moja ya sababu iliyotumika kuinyang’anya leseni Kampuni ya GMS ni watoto wadogo kuwinda. Je, hawa Wamarekani wao kwanini hawahukumiwi kwa hilo licha ya ushahidi wote kuwapo?

JAMHURI tulifanya kazi kubwa kwa kuandika ‘ujangili’ wa WWS/TGTS kupitia Leseni ya Rais. Baada ya kuandika habari hiyo wakaondoka nchini mara moja. Wanyama wetu wakapona.

Mbinu hizi chafu za Nyalandu hazikuishia hapo. Alijitahidi kwa kadiri alivyoweza ili WWS wapate Hadhi ya Uwekezaji Mahiri (SIS) kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutumia nyaraka za uongo. WWS walidanganya kuwa kitalu (Lake Natron East) ni chao. Mtu makini atajiuliza, wamepata hiyo hadhi kwa kigezo kipi? Je, ni kwa ile hundi hewa ya dola za Marekani milioni mbili ambazo mmoja wa wakurugenzi wa Friedkin Group alipiga picha akimkabidhi Nyalandu ili kuuzuga umma kuwa wanachangia maendeleo ya uhifadhi?

Hizo fedha walizitoa lini? Au ni zawadi kutokana na magari yao kukamatwa na bangi yakipeleka Kenya? Au ni ubabe ambao wamekuwa wanaufanya dhidi ya kampuni nyingine? Au ni kuwa tayari kutoa ndege kwa matumizi binafsi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii?

Nirudi nyuma kidogo. La kushangaza ni pale inapokuwa Strategic Investment Status imetolewa na TIC kwa Friedkin siku moja [Agosti 20, 2015] na kuridhiwa siku hiyo hiyo na Nyalandu [Agosti 20,2015]; huku maofisa wa Idara ya Wanyamapori wakiwa hawana habari.

Mbaya zaidi, Friedkin wametumia vitalu ambavyo si vyao kuomba hadhi hiyo ya uwekezaji, ikiwemo Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba ambayo ilitolewa kwao kinyemela na kwa kuvunja kanuni zinazotaka ranchi iwe kilometa 20 kutoka kwenye maeneo kiini yaliyohifadhiwa.

Ranchi hiyo inapakana (yaani iko umbali wa kilometa 0) na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Eneo la Hifadhi la Serengeti, Pori la Akiba la Maswa na Jumuiya ya Hifadhi ya Makao. Eneo hili ni ushoroba kati ya hifadhi hizi.

Hivyo, Kampuni hii ya Mwiba haizalishi wanyamapori kama inavyotakiwa kisheria, bali wanachofanya ni kutegea wanyama kutoka kwenye eneo hilo ili wawinde. Huu ni uhuni usiovumilika. Kwa ujambazi huu, nani atagoma kuamini kuwa kuna michezo hatari ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii?

Tabia ya kampuni za FCF katika tasnia ya uwindaji

Kimsingi, kampuni za FCF (WWS, TGTS na Mwiba Holdings) zimekuwa na tabia ya ubabe na usumbufu katika tasnia ya uwindaji wa kitalii. Tabia hizi zimeonekana katika sehemu mbalimbali ambako kampuni hizi zimekuwa zinawinda.

Pamoja na mgogoro wa Lake Natron East, mgogoro mwingine unaohusiana na kampuni hizi ulikuwa kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii (WMA) ya Makao ambako TGTS ikishirikiana na Kampuni ya Mwiba Holdings walijenga kambi kwa ubabe kwenye kitalu ambacho kilimilikishwa kihalali kwa Kampuni ya Fereck Safaris Ltd.

Kampuni ya TGTS ilishindwa kwenye mchakato wa maombi ya kitalu cha Makao ambako ilipata alama 50 wakati washindani wao, Fereck Safaris walipata alama 86.

Kampuni ya TGTS kupitia Mwiba Holdings ikawa inaendesha utalii wa picha katika kitalu hicho na kujihusisha na uwindaji ingawa hawakuwa na kibali cha kufanya shughuli hizo. Kampuni ya Fereck Safaris ililalamika kuwa inapoteza safari mbili na hivyo kudaiwa kulipa fidia. Aidha, idara ikapokea malalamiko kuwa wananyimwa haki ya kutumia eneo lao na Kampuni hii ya Mwiba.  Baada ya Nyalandu kuupata uwaziri akashinikiza kuwa Fereck waachie kitalu chao ili rafiki zake wakichukue. Ikawa hivyo.

Barua ya Baraza la Congress kwa Rais Obama

 Kampuni hizi za Friedkin kwa kutambua kuwa hazina haki kwa waliyodai, zikapanua mgogoro kwa kuandika barua kwa wabunge wa Marekani.

Baraza la Congress la Marekani lilimwandikia Rais wa Marekani, Barack Obama, barua likiituhumu Idara ya Wanyamapori kwa kuinyanga’anya Kampuni ya Friedkin kitalu na eti kukitoa isivyo halali kwa kampuni nyingine ya kigeni, jambo ambalo halikuwa kweli, kwani GMS si ya kigeni, bali ni ya Kitanzania.

Walilipotosha kwa makusudi Baraza la Congress ili kuendeleza ubabe na mbinu chafu kulinda masilahi yake. Uongo na tuhuma hizo viliwasilishwa kwenye Baraza la Congress baada ya Friedkin na WWS kushindwa mahakamani. Hata hivyo, tuhuma hizo hazikueleza kuwa wameshindwa kesi. Hawa watu wameshashindwa na GMS mara saba mahakamani katika kesi walizofungua wao na walizofunguliwa.

Ushawishi (lobbying) uliofanywa na Friedkin kwenye Baraza la Congress ni moja ya mbinu chafu zilizokuwa na lengo la kuhakikisha kuwa kampuni zake zinaendelea kupata haki ambayo si stahiki yao kisheria.

Kampuni za Friedkin zimegeuza nchi hii kuwa koloni lao. Hili linathibitishwa na dharau zao dhidi ya serikali huko nyuma na hata sasa.

Nashauri vyombo vya uchunguzi vipate ukweli kuhusu uanzishwaji wa Ranchi ya Mwiba – je, nani aliiruhusu wakati haikidhi vigezo? Tujue ukweli juu ya unyanyasaji wa wananchi kule Meatu. Watanzania waelezwe kwa nini walipewa hadhi ya kutumia Leseni ya Rais kuua wanyama 708; watu waelezwe kwa nini watoto wadogo waliruhusiwa kuwinda kinyume cha sheria za nchi? Je, Wamarekani wana kinga kuvunja sheria za Tanzania na wakaachwa hivi hivi?

Wananchi waelezwe ukweli juu ya magari ya kampuni hii kukamatwa yakiwa yamepakiwa magunia ya bangi yakisafirisha kwenda Kenya – nani anafanya biashara hii? Inawezekana kweli dereva kuiba gari kutoka Arusha kwenda Nairobi bila wakubwa wa kampuni kujua?

Ndugu zangu, kama nilivyopata kusema, inawezekana GMS akawa na makosa yake, lakini katika hili anaonewa. Wachache wanaofahamu mchezo huu mchafu watajua nilichoeleza hapa ni ukweli kwa asilimia 100.

Wamarekani hawa wanatumia maguvu yao ya fedha na ubabe wa taifa lao kuwasumbua Watanzania wanyonge. Kampuni iliyoshiriki michezo michafu kama hiyo haiwezi kuwa na uhalali wa kupewa vitalu wanavyopokwa wazalendo wa nchi hii.

Waziri Kigwangalla pengine hajui mengi nyuma ya sakata hili, na kama anayajua, basi kuna kinachompa upofu. Amfukuze GMS kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria. Asitumie maguvu ya uwaziri kumwonea mtu ambaye anajua hawezi hata kubisha hodi Ikulu kuomba msaada. Tujenge taifa la haki. Rais amesema hataki kutawala taifa la watu wanaonung’unika, basi iwe hivyo pia kwa wanaomsaidia. Tuishi kwenye ukweli; na wenye sauti wawe sauti ya wasio na sauti – kwa watu aina ya GMS.