Wiki iliyopita zilichapishwa habari nyingi, ila nimejikuta na shindwa kujizuia nashawishika kuandika jambo juu ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mheshimiwa sana, Samuel Sitta, ‘Mzee wa Kasi na Viwango.’ Mheshimiwa huyu ametoa kauli kuwa Bunge Maalum la Katiba lazima liendelee na kura zipigwe.
Si hilo tu, amekwenda mbali zaidi na kusema kura hizo watapiga hata ambao hawatakuwapo kwenye ukumbi wa Bunge kwa maana ya kuwa safarini nje ya nchi au kama ni wagonjwa hospitalini. Anasema wanalenga kubadili kanuni utumike utaratibu wa kuwapigia simu waridhie wanakubali au kukataa nini kisha kazi ikamilishwe.
Sitanii, hakika kauli hii ya Sitta imenishtua. Imenishtua na kunifikirisha juu ya Mheshimiwa huyu. Nikiri Watanzania wengi miaka mitatu tu iliyopita walikuwa wakimwona Sitta kama shujaa wa nchi hii. Wapo walioshikilia msimamo wakawa mara zote wakisema kuwa Sitta katika sifa za uongozi, bado kuna punje inampungukia.
Wengi wamekuwa wakisema Sitta anasukumwa na matarajio, matakwa na matamanio binafsi katika kila uamuzi anaofanya. Mimi sijasema hivyo. Wanasema Sitta hata wakati anapambana na Edward Lowassa alikuwa na lake jambo. Sasa hili kwa kuwa linasemwa sana na si maneno yangu ila nimelisikia katika vijiwe vingi, acha niliseme tu.
Sitanii, huko ‘saiti’ wanasema hata Richmond, Sitta alishirikiana na baadhi ya ‘wataalam’ kumchongea Lowassa ‘yai viza.’ Wanasema Richmond yalikuwa madai hewa kwani Sitta ndiye aliyeikaribisha nchini kampuni hiyo mwaka 2002 akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Na kweli, nilivyofuatilia pale TIC nikaona kumbukumbu zenye kuonyesha ushiriki wa Sitta katika kuileta Richmond nchini mwaka huo akiwa ameikabidhi kampuni hii mradi wa kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza. Mradi huu haujawahi kutekelezeka. Nimesoma baadhi ya kumbukumbu Sitta anakiri kuileta nchini Richmond.
Hata hivyo, Sitta anasema wakati anaipa Richmond kibali cha kuja nchini ilikuwa haijawa kampuni ya kitapeli. Napata shida kidogo. Sitta alifanya utaratibu aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye akapelekwa nyumbani kwa Mohamed Gile nchini Marekani na kumtambulisha kuwa ni mfanyabiashara makini.
Huyo mmiliki wa Richmond ambaye Sitta alimtambulisha kwa Sumaye akimtaja kama mfanyabiashara makini, akampa mradi wa kujenga bomba la mafuta kati ya Dar es Salaam na Mwanza, lakini hadi leo bomba hilo halijawahi kujengwa. Wala mimi sitaki kwenda huko, maana wengi wataanza kukumbuka siasa za Richmond na Dowans.
Nilisema tena kwa sauti kubwa, kuwa kesi za Dowans Serikali inapoteza muda na fedha kwa sababu ya ushabiki wa kisiasa haiwezi kushinda hata kesi moja. Ningetumia maneno ya uswahilini ningesema ‘kiko wapi?’ Serikali imeshindwa Uingereza, ikashindwa na katika Mahakama yetu katika kesi hii ya Richmond.
Sitanii, shinda ninayopata ni moja tu. Sitta ni Mwanasheria. Amesoma sheria hizi hizi nilizosoma mimi. Mitaala aliyotumia ndiyo hiyo hiyo tuliyoitumia sisi shuleni. Sheria ya Mikataba (the Law of Contract) tunayoitumia haijabadilika tangu mwaka 1912 Uingereza iliporasimisha mfumo wa sheria tunaotumia sasa.
Najiuliza, Mzee Sitta ameanza kusahau sheria ya mikataba inasema nini? Suala la Richmond na Dowans alilitumia kisiasa kama wanavyosema huko ‘saiti’ kuwa alitaka kuua nguvu za Lowassa katika harakati zake za kugombea urais na wananchi wamfikirie yeye na kumuona ni jasiri?
Najua kwa kutaja jina Lowassa, kwa baadhi ya watu demokrasia inaweza kukoma mara tu unaposoma jina hili. Ukachukua kila chembe ya uvumi uliotamalaki hapa nchini dhidi ya Lowassa na kuacha kusoma maudhui ya makala hii ukaangukia kwenye pepo la kumfikiria Lowassa kwa yale yasemwayo dhidi yake bali si kwa yale atendayo.
Nchi hii inasikitisha. Nguvu iliyotumika kushambulia jina la Lowassa, nikipita kwenye vilinge naiona ikitumika sasa kummaliza Bernard Membe. Walewale waliokuwa wanampeleka Membe majungu dhidi ya Lowassa na kumwita Lowassa fisadi, leo wamehamia kwa ‘Mtoto wa Mkulima’, Mizengwe, ahaa samahani, Mizengo Pinda.
Nasikia na nashuhudia sasa mzee wa kuwambia wenzake wanafikiri kwa kutumia makalio ndiye Kamanda Mkuu wa Vita ya Mtoto wa Mkulima kuelekea Ikulu. Umbea sawa na waliokuwa wakimsambazia Lowassa umehamishiwa kwa Membe sasa wakidhani ndiye tishio la kufikia matakwa yao.
Sitanii, nchi hii viongozi vurugu, wapigakura vurugu. Haikuwa nia yangu kueleza harakati la urais 2015 katika makala hii, bali kioja cha Sitta kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wasiokuwapo watapigiwa simu kupiga kura. Maswali niliyopata ni haya yafuatayo kati ya machache.
Je, huo ndio uwezo wa Sitta kufikiri? Je, kwa nini Sitta avunje kanuni ya msingi kuwa huwezi kutolea uamuzi kesi ambayo hukuisikiliza? Je, hao wajumbe watakaopiga kura kwa njia ya simu watajua nini kimejadiliwa na wanapigia nini? Je, Sitta maneno haya amekubaliana na Mwenyekiti wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete?
Binafsi namheshimu mno Mzee Sitta. Tulikwenda ofisini kweke, tukazungumza hoja ya kuwa na Baraza la Habari la kisheria, ambalo alituelewa akatuunga mkono na naomba kumwambia nadhani jinsi alivyotupokea wiki tatu zilizopita kwa maslahi ya tasnia ya habari na nchi hii, lakini katika suala la Katiba Mpya naomba kumshauri hadharani.
Kwamba inawezekana Mzee Sitta husomi alama za nyakati. Kwamba, inawezekana Mzee Sitta una matamanio ya kupata posho za ziada kujihami kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kwamba inawezekana Mzee Sitta una matamanio ya kugombea tena ubunge au urais kwa mara ya kwanza, na mengine, na mengine.
Ulipofika sasa nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa ufunge breki. Ngoma za masikio ya Watanzania zimepenywa kwa unyenyenyekevu na makubaliano yayofikiwa kwenye TCD kati ya Rais Kikwete na TCD a.k.a UKAWA. Kwamba sasa watu wanataka Tume Huru ya Uchaguzi na si kura za walioko nje ya Bunge Maalum la Katiba.
Kwamba watu wanaona kama CCM haina nia ya kuiba kura inahofia nini kuruhusu Tume Huru ya Uchaguzi ambayo hata wapinzani watakuwa na uwakilishi kwa nia ya kuangalia kura zinahesabiwaje na ngapi zinapatikana, si wao kuhesabu kura? Kikwete anaweza kutofautiana naye, lakini katika hili nasema heko.
Kwamba Kikwete amekubali Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba Kikwete amekubali hoja ya mgombea binafsi, na kwamba Kikwete amekubali matokeo ya Urais kupingwa mahakamani, na kwamba Kikwete yuko njiani kukubali uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata habari, tusipompongeza katika hili tunataka tumpongeze wapi?
Sitanii, tuelewane lugha, pongezi hizo hapo juu haziondoi kauli yangu kuwa Kikwete amevunja sheria kwa kukubali wazo la Katiba mpya katikati ya mwaka wa fedha wa Serikali pasipo kupitia bungeni akidhani anawapiga bao Chadema au mpango wa Big Results Now, ambao nao haujapitia bungeni. Namshauri arejee kwenye utawala wa sheria.
Watanzania wenzangu nasema na narudia kusema. Mzee Sitta kama anatunisha msuli na kusema anaendelea na Bunge la Katiba, basi napata shaka iwapo kuna mawasiliano ya dhati na Mwenyekiti wake aliyezungumza na UKAWA kupitia TCD. Kama nilivyosema namshauri Sitta hadharani, naomba sasa wawili hawa wawasiliane.
Sitanii, lipo jingine lililonipa shida kidogo wiki hii, ila kutokana na ufinyu wa nafasi nitaligusia bila kulizungumzia kwa kina. Hili nitaendelea kulitafakari, na naomba tushirikiane wewe msomaji kulifanyia kazi, kisha tupate jibu la pamoja. Hili si jingine, bali ni habari kwamba Mheshimiwa sana Freeman Mbowe amevunja Katiba ya Chadema.
Kwamba Mbowe alipaswa kuondoka madarakani baada ya kuwa Mwenyekiti wa Chadema kwa miaka 10 mfululizo limezungumzwa. Kwamba hili ndilo liliwaponza Zitto Kabwe, Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo limezungumzwa. Sasa hili bado nalifanyia kazi. Naangalia ikiwa baadhi yetu hatuheshimu sheria za vyama, tutawezaje kuheshimu Katiba? Tukutane wiki ijayo.