Miradi mbalimbali inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika bandari za Ziwa Nyasa, inatazamiwa kuongeza ufanisi maradufu katika uhudumiaji na usafirishaji mizigo.

Hatua hiyo inaelezwa kwamba itazinufaisha pia nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zinazopakana au kuwa karibu na ziwa hilo la tatu kwa ukubwa Afrika.

Katika mazungumzo rasmi na gazeti hili, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abed Gallus, anasema Ziwa Nyasa linaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Njombe na Ruvuma kwa upande wa Tanzania sambamba na nchi jirani za Malawi na Msumbiji. Hali kadhalika pia ni rahisi kutokea ziwa hilo kwenda Zambia hadi Zimbabwe.

“Kuna maeneo ambayo hayafikiki kabisa kwa njia nyingine isipokuwa kwa njia ya maji tu. Au mengine yanaweza kufikika kwa njia ya barabara, lakini ni umbali mrefu, hivyo kuyafikia pia ni gharama kubwa kuliko kutumia njia ya maji. Hii si tu kwa Tanzania, bali hata kwa majirani zetu wa Malawi na Msumbiji,” anasema.

Anasema huduma za usafiri na usafirishaji katika ziwa hilo zinazidi kuboreka, hatua ambayo anasema likitumiwa vema linaweza kutoa mchango mkubwa katika kuboresha uchumi wa wakazi wa mwambao wa ziwa hilo katika mataifa haya matatu; Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Ujenzi wa meli

“Kwa kuzingatia umuhimu wa Ziwa Nyasa katika uendeshaji uchumi sambamba na kuwepo kwa changamoto za kiusafirishaji ziwani, Januari 2015 Serikali ya Tanzania kupitia TPA ilisaini mikataba miwili kwa ajili ya ujenzi wa meli tatu; mbili zikiwa za mizigo na moja ya abiria na mizigo,” anasema Gallus.

Meneja huyo anasema ujenzi wa meli mbili za mizigo za Mv Njombe na Mv Ruvuma ambazo ujenzi wake ulianza Januari 2015 ulishakamilika na zinafanya kazi tangu mwaka 2017, hivyo zipo kwa ajili ya kukodiwa na wafanyabiashara wa nchi hizi tatu. Meli hizo mbili za mizigo, kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000.

“Hizi meli zinafanya kazi, hivyo kwa niaba ya TPA napenda kuwakaribisha wateja wote (wa nchi zote tatu au nyingine za jirani) kutumia meli hizi mpya na za kisasa. Wataokoa muda na pesa kusafirisha kwa meli kuliko kutumia njia ya barabara ambayo ni ghali,” anasema Gallus.

Kwa sasa anasema ujenzi wa meli ya abiria na mizigo ya Mv Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 unaelekea kukamilika.

Meli hiyo pia inatazamiwa kutumiwa na wananchi na wafanyabiashara wenye mizigo midogo midogo katika ukanda huo wa SADC.

Kwa mujibu wa Gallus, TPA pia inaboresha na kupanua Bandari ya Kiwira ambayo ni lango kuu la usafirisaji wa mizigo katika Ziwa Nyasa.

Mradi mwingine wa TPA unaoendelea Ziwa Nyasa, Gallus anasema ni ujenzi wa Bandari ya Ndumbi mkoani Ruvuma.

Hii ni bandari ya muda mrefu ya upitishaji wa shehena mbalimbali, hususan makaa ya mawe.

Anasema shehena za nchi za Malawi, Msumbuji na hata Zambia, zinaweza kusafirishwa hadi Bandari ya Mtwara, kisha zikasafirishwa kwa magari au reli hadi katika bandari za Ziwa Nyasa na kisha kusafirishwa kwa usafiri rahisi wa meli hadi katika nchi hizo jirani.

Kwa mujibu wa Meneja Gallus, ujenzi katika Bandari hiyo ya Ndumbi unahusisha pia sehemu ya kuhifadhia mizigo, gati la kisasa, ofisi na nyumba ya wafanyakazi.

Changamkieni fursa

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta, anapongeza hatua ya serikali ya Rais John Magufuli kupitia TPA kuamua kuboresha usafiri wa maji katika ziwa hilo kwa kuunda meli mbili za mizigo na moja ya abiria, sambamba na upanuzi wa Bandari ya Kiwira.

Anasema hatua hiyo si tu inaimarisha usafiri, bali pia inaboresha ujirani mwema kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa katika nchi zote zinazopakana na ziwa hilo.

Anasema anaamini uchumi wa Kyela na wilaya za jirani; za Tanzania na za nchi nyingine zinazopakana na ziwa hilo watakaochangamkia fursa ya biashara, uchumi wao utakua maradufu, kwani ni rahisi sasa kubadilishana bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.

“Kwa mfano, Tanzania tunazalisha makaa ya mawe na pia hapa Kyela tunavuna mpunga, hivyo ni vema wafanyabiashara wachangamkie fursa ya kupeleka bidhaa hizi katika nchi za jirani na huko wakaja na kitu kingine ambacho kina mahitaji makubwa Tanzania,” anasema.

Gerson Charles, Msimamizi wa Kituo cha Mamlaka ya Mapato (TRA) kilichoko Ipyana, akisimamia mizigo inayopita katika bandari za Itungi na Kiwira wilayani Kyela, anapongeza hatua zinazochukuliwa na TPA kuboresha bandari na usafirishaji wa njia ya majini katika Ziwa Nyasa kwa ujumla.

Pamoja na kuwahimiza wananchi na wafanyabiashara kutumia usafiri wa majini ambao si ghali kulinganisha na aina nyingine za usafiri, Charles anawashauri pia kufika TRA kupata maelekezo ya namna nzuri ya kusafirisha shehena zao ndani na nje ya nchi pamoja na elimu ya kodi.

Naye Richard Mahundi, mchimbaji mdogo wa makaa ya mawe Liweta, jirani na Bandari ya Ndumbi mkoani Ruvuma anapongeza hatua ya ujenzi wa bandari hiyo kwamba ndio umesababisha wao kuanza uzalishaji wa madini hayo.

“Shida kubwa iliyokuwa inatukwaza kuanza mradi huu ni namna ya kuwafikishia wateja wetu makaa ya mawe, lakini ujenzi wa meli za mizigo na uboreshaji wa Bandari ya Ndumbi, umeondoa kabisa hicho kikwazo,” anasema na kuongeza kwamba wanatazamia kuwa na wateja nchini Malawi.

Ziwa Nyasa kwa ufupi

Nyasa ni kati ya maziwa makubwa ya Afrika Mashariki, likishika nafasi ya tatu kwa ukubwa baada ya Ziwa Victoria linaloongoza na Ziwa Tanganyika linalofuatia.

Ziwa hili lenye visiwa kadhaa vikiwemo vya Likoma na Chizumulu lina urefu wa kilometa kati ya 560 na 580 na ukubwa wa kikometa 50 hadi 80.

Kusini mwa ziwa hili kuna Mto Shire unaotoa maji Ziwa Nyasa kwenda Zambezi na hatimaye Bahari ya Hindi, likipata maji yake mengi kupitia Mto Ruhuhu na mingine midogomidogo. Kijiolojia, Ziwa Nyasa ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.

Bandari za Ziwa Nyasa

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Gallus, anasema kuna bandari 15 upande wa Tanzania zinazohudumiwa na TPA katika ziwa hilo, hivyo kutambuliwa kisheria. Bandari hizo ni pamoja na Bandari ya Itungi iliyoko Kyela, mkoani Mbeya, yaliko pia makao makuu ya Bandari za Ziwa Nyasa. Bandari nyingine zilizomo katika wilaya hiyo ya Kyela ni Kiwira na Matema.

Kwa upande wa wilayani Ludewa, mkoani Njombe, Gallus anasema kuna bandari rasmi sita za Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde, Lupingu na Manda.

Katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, Gallus anataja bandari zinazosimamiwa na TPA kuwa ni Ndumbi, Lundu, Nkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay na kuongeza kwamba kisheria, kila bandari lazima isimamiwe na TPA.

Kwa upande wa Malawi, bandari kubwa taarifa zinaonyesha kwamba ni ile ya Chipoka, katika Wilaya ya Salima. Pia kuna bandari ndogo ndogo za Monkey Bay, Nsanje, Nkhata Bay, Nkhotakota na Chilumba. Kwa upande wa Msumbiji kuna bandari za Niassa na moja katika Mto Shire.