Wiki iliyopita katika sehemu ya 10 hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Nilitembea kidogo kisha nikajikuta niko kwenye himaya ya watu wa ajabu. Sielewi sawa sawa kama hawa walikuwa ni watu au la. Nilipelekwa kwenye ghorofa moja na huko nikakuta nimeandaliwa chakula. Kilikuwa eti damu ya kichwa cha mtu. Sikula na waliponibembeleza ikashindikana hatimaye waliondoka. Nikaachwa peke yangu.” Endelea…
Baadaye alikuja bibi kizee mmoja akanisalimia na kuniamrisha kuwa nikiwa huko kazi yangu itakuwa ni kuchunga ng’ombe wake. Kama kazi hiyo nitaifanya vema, aliniahidi eti watanirudisha nyumbani. Alinisisitiza yule bibi kwamba utii ni kitu muhimu, la sivyo wataniacha huko huko.
Siku moja nikiwa machungani niliona mambo ya ajabu sana. Kwa mbali nilisikia mlio wa gari linakuja upande wangu. Punde si punde nikaliona linakuja. Eneo hilo halikuwa na barabara, ila lile gari lilikuwa linapita tu popote. Liligonga miti na lilipopita ile miti ikarudia tena hali yake. Looo! Jamani! Hii ni ndoto au kweli?
Siku moja nilikwenda kuchunga nikiwa na kijana mdogo. Tulipokuwa huko machungani alinieleza kuwa karibu siku zangu za kurudi kwetu zinakaribia ila alitaka kunionyesha jinsi watu wa dunia hii wanavyohangaikia wafu wao. Tarehe ya kifo changu ilikuwa inakaribia. Wanandugu wa upande wa baba na wa mama walikusanyika ili wafanye ibada ya kuniombea.
Zilichangwa pesa kutoka kwa ndugu hawa na ikaandaliwa sherehe ya kunikumbuka. Pesa zingine zilipelekwa kanisani ili nisomewe misa ya kumbukumbu. Zingine zikatengwa kwa ajili ya kununulia mapochopocho. Niliwapenda sana ndugu zangu walivyokuwa wakinienzi. Pia ilikubalika kuwa kaburi langu liwekewe marumaru ili lipendeze na liendane na hadhi yangu.
Mimi nilikwenda mpaka nyumbani kwetu. Nikawasikia ndugu wakizungumza kwa nguvu na kwa furaha. Hawakuwa na huzuni kama walivyokuwa nayo ile siku walipokuwa wananizika. Hata wewe rafiki yangu Bugulugulu hiyo siku ulipita nyumbani. Mama yangu akakukaribisha kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kifo changu.
Hivi ni kweli ulikuwa hunioni au ndiyo ukorofi wako tu wewe mpendwa wangu! Nakumbuka fika baada ya kuongea na mama uliaga ukaanza kuondoka. Bahati nzuri ukawa unaelekea upande tuliokuwa mimi na yule kijana mdogo. Nilikutegeshea mguu nione kama kweli hunioni. Ulijikwaa ukataka kuanguka.
Nilikuona unaangalia kwa makini uone ni kitu gani kimekinzana. Hali hiyo aliiona pia mama yangu na akataka kujua kulikoni! Ulidai eti hata wewe hujui! Hivi ni kweli ulikuwa huoni mguu wangu? Au umeoteshwa macho kwa ajili ya urembo? Mimi na yule kijana tulirudi kwenye dunia yetu na nikaendelea na shughuli yangu ya kuchunga wale mifugo wa yule bibi.
Siku moja nikiwa katika shughuli zangu za uchungaji, alipita binti mmoja na kunisalimia kwa heshima kubwa: “Bugulugulu ndugu yangu, ninakusalimia salamu za kutoka chini kabisa ya roho yangu. Najua umeteseka sana, lakini hayo ndiyo maisha ya huku! Utazoea tu! Ninavyokuona wewe utakuja kuwa bingwa na unaweza hata ukapata cheo kikubwa cha huku.” Sasa moyoni nikawa ninasema niwe mchawi?
Nililazimika kumwangalia binti huyu kwa makini zaidi. Kwa hakika sikukumbuka kumwona popote katika maisha yangu. Angalizo zaidi lilinifanya nibaini kuwa msichana huyu alikuwa na macho ya nguruwe na mikono yake imefananafanana na mikono ya mamba, moyo ulienda mbio. Nikaogopa kwa hakika mwili ulikufa ganzi nikahangaika kwenye nafsi yangu. Sikujua la kufanya. Yule binti aligundua tatizo langu akawa kama anasimama kidogo na punde mdomo wake ukawa dhahiri kabisa ni wa mamba. Alinibadilikia mikononi mwangu!
Nilipokuwa nikitafakari la kufanya, ile hali ya upole wa yule binti ikawa inabadilika hatua kwa hatua na kuwa nduli akitaka kunimeza. Sasa alikuwa amekamilika, amekuwa mamba kabisa. Aliachama tayari kuning’ata na kunikata vipande vitatu; kimoja huku na kingine huko na kimoja kibaki kinywani mwake. Lilikuwa tukio la balaa kweli kweli. Nilitulia nikangojea bahati yangu, kwani Waswahili husema: “Bahati haivutwi kwa kamba.”
Mara akatokea babu mmoja alikuwa mgeni machoni pangu. Alionekana kuwa na nguvu sana. Mishipa ya shingo ililingana na kidole cha mkono kile cha mwisho. Mwili mzima ulionekana mkakamavu. Yule babu akamuuliza yule mamba alikuwa anataka kunifanya nini! Loooo! Yule mamba akanywea na kubadilika na kuwa binadamu tena, ila tu ile mikono yake na yale macho yake ya nguruwe yakabaki hivyo hivyo. Akaomba msamaha na kuahidi tena kuwa hatanidhuru.
Funga kazi ya safari yangu iliishia pale ambapo mlinikamata kule kwenye Kijiji cha Bukondamoyo. Siku hiyo sitaisahau kabisa. Ilikuwa kwamba, katika safari yangu nilikuwa nimesahau yale maneno ya yule bibi wa mwanzoni kuwa nitakutana na ng’ombe mpole.
Kumbe ilikuwa balaa, ni kinyume kabisa na maelezo ya yule bibi. Kwenye kichaka kikubwa kilichokuwa mbele yangu nilishtukia amekurupuka kifaru anakuja kunimaliza. Nikaanza kumkimbia. Naye akaja kasi zaidi akipiga kelele za kuogofya. Nilipiga kona na kuzunguka kichaka hiki, na yeye akawa anakuja tu kasi kwelikweli. Niliogopa! Jamani niliogopa mno! Nikakata tamaa ya maisha. Yule mnyama akawa ananisogelea karibu kila dakika, yuko kasi kabisa.
Nikapiga kelele. Nikapiga kelele kuomba msaada sijui kutoka wapi! Kifaru alikuwa amenibakiza hatua chache tu anichote kwa pembe zake na anisambaratishe. Akafumba macho yake bila shaka alijua kuwa lengo lake sasa limefika kwenye ‘point of no return’.
Na alikuwa na uhakika atakapoibuka, atakuwa amenidunga kwenye pembe zake na aanze kunigaragaza. Aliponigusa tu! Mara akageuka kuwa ng’ombe! Akawa ananiangalia na kunirambaramba. Ndipo nikakumbuka maneno ya yule bibi: “Utakuta kamba njiani” – kumbe nyoka. “…utakuta ng’ombe mpole…” – kumbe kifaru mkali.
Bulongo, kifaru mwone kwenye sinema tu na usijaliwe kukutana naye mubashara. Kwanza, ni mkubwa zaidi ya ng’ombe. Halafu yeye na binadamu ni maadui. Kwa hiyo kukutana naye ni vita na huwa na lengo la kukumaliza tu basi.
Sina maelezo ya kilichotokea rafiki yangu baada ya kifaru huyu kugeuka na kuwa ng’ombe mpole. Inasemekana eti mimi nilikuwa ninakimbia na nguo zangu zilikuwa zimebaki marapurapu kwa vile nilikuwa sijabadilisha muda mrefu.
Watu walianza kunifukuza. Wakapiga yowe baadaye mkanikamata. Mimi nilikuwa ninawafahamu wengi wenu. Ila tu wachache ambao sikuweza kuwatambua. Kwa vile walikuja baada ya mimi kufa. Nywele zangu zilikuwa ndefu na zilikuwa zimechafuka kwa vile tangu nilipokufa sikupata muda wa kuziosha vizuri, kucha zangu pia zilikuwa ndefu, kwani dunia ya huko nilikokuwa haina utamaduni wa kukata kucha! Nilikuwa kituko!
Watu wote walikuja kunishuhudia na wewe rafiki yangu ukaja nikakutambua. Alipokuja mama na baba yangu, nilizinduka nikaenda kuwakumbatia na wao wakaduwaa wasiamini walichokiona. Mkaamua kunipeleka hospitali muone kama mnachokiona ni hakika.
Jamani, teknolojia ya nilikokuwa ilikuwa ni kubwa mno. Ni mimi kabisa wala msiwe na wasiwasi. Nilimwonyesha mama kovu langu la zamani akalitambua. Waganga wakanipima akili yangu! Hawakuona dosari yoyote. Basi nikapewa ruhusa nirudi kwetu.
Bwana, urafiki una nguvu za ajabu zilizopea na kuvuka mipaka, nguvu hizi ndizo zilizonituma nikuandikie hii barua ndefu yenye mambo ya siri. Samahani kwa kukupotezea muda na labda pengine hata inaweza kuingilia mambo yako ya imani, ila kwa hakika Gamboshi kuna watu walioendelea sana kiteknolojia.
Wakigundua kuwa kuna watu wanawadodosa dodosa kuhusu maisha yao, wana tabia ya kuja na kuwachukua watu kadhaa kwenye ukoo wa mhalifu. Kwa hiyo chunga sana wasije wakakuteka nyara wewe pamoja na nduguzo kadhaa wa karibu. Nyamaza kimya kabisa. Tena wanapenda sana kuwateka wale wenye akili na tegemeo kwenye ukoo husika.
Bwana na yule bibi kizee nilikuja kugundua hapo baadaye kuwa anaishi Tindabuligi. Huwa tunakutana mara kwa mara na eti ananiogopa kwa vile huwa anashangaa jinsi nilivyochoropoka kutoka katika himaya yake. Eti huwa anadhani labda na mimi ni ngangari kwa shughuli hizo.
Hapana bwana, mimi niliponea kwenye tundu la sindano na kwa kudra za Mwenyezi Mungu tu. Hiyo miaka mitatu mliyokuwa mnadhani nimekufa, nilikuwa hai, ila tu katika mazingira tofauti na ya hapa duniani. Rafiki huo ndio uhalisia wa mambo na kama nilivyokutahadharisha hapo awali, usimwambie mtu yeyote. Nyamaza! Sana sana mpe tu hii barua aisome mwenyewe, basi kwa hilo hakuna ubaya.
Sina zaidi ya hayo. Nisalimie mama, ndugu na marafiki zako.
Wasalaam,
Rafiki yako mpendwa,
Bugulugulu Duu.
Hapa ndipo mwisho wa hadithi hii iliyochapishwa katika matoleo 11 ya Gazeti la JAMHURI. Hapana shaka kuna jambo umejifunza ndugu msomaji. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu namba 0755629650.