Agosti ya mwaka huu 2019 ni ya kipekee kwa taifa letu. Tumepokea wageni wengi wanaohudhuria Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Fursa za aina hii hujitokeza mara chache, kwa hiyo kila Mtanzania ana haki na wajibu wa kuchangamkia fursa zinazotokana na ugeni huu.

SADC ni matokeo ya historia ya ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika. Ulikuwa ukombozi wa uhuru, na baada ya mataifa yote kuwa huru, sasa ni mapambano ya kiuchumi.

Tangu kipindi cha kuasisiwa kwa chombo cha kuongoza mapambano ya kujitawala, dhima kuu ya waasisi wetu ilikuwa kuhakikisha kuwa Mwafrika anajikomboa kisiasa na kiuchumi. Sote tunatambua kuwa wakoloni na walowezi walilenga kujinufaisha wao na mataifa yao ya asili. Kwao, Afrika ilikuwa chimbo lao la kuchota rasilimali; na Waafrika walikuwa mitambo yao ya kufanikisha uporaji huo wa utajiri.

SADC ni kielelezo halisi cha namna umoja wa Waafrika unavyopaswa kuimarishwa. Wakoloni walifanikiwa kutuaminisha kuwa mipaka ya kufikirika waliyotuwekea ilikuwa ni mipaka ya ‘Mungu’. Imani hiyo ikatufanya tujiwekee vikwazo vingi vya sisi wenyewe kwa wenyewe kufanya biashara. Tukajiwekea sheria kali zinazomzuia Mwafrika wa taifa moja kuvuka na kuingia katika taifa jingine la Waafrika wenzake kufanya biashara. Muda wa kuondoa vikwazo au vizuizi hivyo umeshawadia. Mipaka iendelee kuwapo kwa sababu za kihistoria, lakini kamwe isiwe kikwazo cha kumzuia Mwafrika wa taifa moja kuingia katika taifa jingine kufanya biashara.

Hatuna budi sisi wenyewe kuanza kuuziana bidhaa mbalimbali kabla ya kwenda ughaibuni kutafuta bidhaa hizo. Soko la kimataifa sharti lianzie kwenye mataifa yetu kabla ya kwenda Ulaya, Marekani au Asia.

Tumeanza na Jumuiya ya Afrika Mashariki, tupo kwenye SADC na sasa tuangalie namna ya kuvunja minyororo yote iliyotutenga ili tuweze kushiriki kwa pamoja mataifa yote ya Afrika katika kufanya biashara.

Lakini hilo halitawezekana kama Afrika itaendelea kukubali kugawanywa kwa misingi ya kikabila, ukanda, rangi, lugha au jiografia ya nchi. Tunatambua kuwa muungano wa Afrika ni jambo gumu kwa sababu mabeberu mara zote wamehakikisha wanatugawa na hata kutuanzishia vita ili tupoteze mwelekeo.

Kwa miaka yote inajulikana wazi kuwa Tanzania ndiyo kinara wa kuisemea Afrika katika masuala yote ya kiuchumi, usawa, amani na kadhalika. Hatuna budi kuendelea kuibeba dhima hiyo kwa sababu ni ndoto na matamanio ya waasisi wa taifa letu.

Ni kwa sababu hiyo tunawasihi viongozi wetu kuwa mfano mwema kwa wenzao wa mataifa mengine, na kamwe tusiwe nyuma pale kunapo onekana kuwa mchango wetu kwa jambo fulani unatakiwa. Afrika itajengwa na Waafrika. Uwezo huo tunao. SADC ni mfano halisi.