Ukiwa na ndoto usipige kelele, kaa kimya

 

Mtu anapokuwa na ndoto mara ya kwanza huwa haipo katika uhalisia, bado inakuwa haijatimilika. Kwa msingi huo, unapokuwa na ndoto, kaa kimya usipige kelele.

Mojawapo ya kosa kubwa alilolifanya Yusufu ni kuwaambia ndugu zake ndoto yake kuwa baadaye atakuwa kiongozi wao. Huu ukawa mwanzo wa ndugu zake kuamsha chuki zao juu Yake.

“Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, “Tafadhalini sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya wangu.”

Ndugu zake wakamwambia, “Je, kweli wewe utatumiliki sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na maneno yake.” (Mwanzo 37: 5-8).

Haikuishia hapo tu, alipoota ndoto ya pili akarudi kuwaambia tena ndugu zake, “Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tukusujudie hata nchi?” (Mwanzo 37: 9-10).

Tunaambiwa baada ya Yusufu kuweka ndoto zake hadharani ndugu zake wakaanza kmchukia, wakaanza kumpa majina ya ajabu ajabu kama lile la “Bwana ndoto.” Unapowaambia watu ndoto zako, jiandae kukatishwa tamaa, jiandae kupambana na maadui ambao hata ulikuwa hujui kama ni maadui zako. Jiandae kutukanwa na kusemwa maneno ambayo hujawahi kuyasikia.

Hayo ndiyo huwa matokeo ya kutangaza ndoto zako ukiwa unaonekana huna kitu. Wewe unachokuwa umekibeba wakati huo ni wazo tu. Nakubaliana na Stephen Hough aliyesema, “Ukimya ni udongo muhimu utakaofanya wazo lolote liweze kumea.”

Siku moja wakati naandika kitabu changu cha kwanza kinachoitwa Barabara Ya Mafanikio kuna rafiki yangu aliyekuta nimeketi mezani nikichapa maneno kwenye kompyuta yangu. Akaniuliza “Unafanya nini?” Nikamjibu, “Naandika kitabu” akanijibu akisema, “Wewe uandike kitabu! Dogo utakuwa umekuwa kichaa.”

Maneno kama hayo yanakatisha tamaa sana na kama una moyo mdogo wa kuvumilia lazima utaacha. Jambo la kumshukuru Mungu sikuacha, lakini nilitaka kukuonesha jinsi ambavyo ukiwa na ndoto na kuanza kuisemasema kwa watu unaweza kuishia njiani na hata siku mojausione ndoto yako ikitimia.

Kukosa ukimya kulikaribia kumfanya Yusufu auliwe na ndugu zake. Huruma ya kaka yake Reubeni ndiyo ilimwokoa asiuawe. Hawakuishia hapo tu, wakaamua kumuuza kama mtumwa.

“Unapokwenda na kutangaza ndoto zako hadharani, unawakaribisha maadui ambao watakuja kukuponda kabla hujaona ndoto yako ikitimia.” Ni maneno ya mchungaji Mensa Otabil toka nchini Ghana.

Kuna msemo ambao huwa naupenda sana, ulisemwa na Frank Ocean. Anabainisha, “Fanya kazi kwa bidiï katika ukimya, yaache mafanikio yapige kelele.” Hii ni kaulimbiu muhimu kwa kila mtu mwenye ndoto.

Kuna aliyeboresha zaidi msemo huo akasema, “Fanya kazi kwa bidii katika ukimya, iache Lamborghini (aina ya gari) ipige kelele.”

Unapokuwa na ndoto kaa kimya, ndoto yako ni yako peke yako na si ya wengine. Endelea kufanyia kazi mawazo uliyonayo ili ndoto yako itimie.

Nakubalina na Plutarch aliyesema, “Ukimya katika kipindi sahihi ni hekima, na ni bora kuliko kutoa neno.”

Ndoto yoyote inahitaji ukimya. Unaweza kuwaambia wale tu ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuwa msaada wa wewe kutimiza ndoto yako, lakini si kila mtu anahitaji kusikia kile unachotaka kukifanya.

Mwanafalsafa Confucius anasema, “Ukimya ni rafiki wa kweli, hajawahi kusaliti.” Ukitaka watu wasikusaliti katika ndoto yako kaa kimya.

Ukimya hauishii tu katika ndoto zetu, hata maisha yetu ya kila siku yanahitaji ukimya. Mwanao amefaulu kidato cha sita na anaingia chuo, kaa kimya watu waone anafanya kazi baadaye. Mkeo amepata mimba, kaa kimya wataona mtoto. Unataka kununua gari, kaa kimya wataona unapakimbele ya nyumba yako.

Umenunua kiwanja na kuanza kujenga, acha kutangaza. Waache watu waone unawaaga kwamba unatoka katika nyumba ya kupanga na unahamia kwako. Umepandishwa cheo kazini, kaa kimya watasikia ukiitwa bosi. Maisha ya ukimya ndiyo yamewafanya watu wenye ndoto kubwa wazilete duniani zionekane. Simba mwenda kimya ndiye mla nyama.