Ni jioni ya saa 11 Jumatatu Agosti 5, 2019. Nipo ofisini. Mara napata simu, namba siifahamu. Mtu huyu ananiambia anataka kuiongezea nyama habari tunayochapisha kuhusiana na mauaji ya Naomi Marijani (36), anayedaiwa kuuawa na mumewe, Hamis (Meshack) Said Luwongo (38).
Mtu huyu ananieleza taarifa zinazofanana na alizonipatia awali Mchungaji Said Luwongo (76), ambaye ni baba wa Hamis, tulipozungumza naye nyumbani kwake Kigamboni, Dar es Salaam. Mtoa taarifa huyu, ananiambia Hamis mbali na kwamba baba yake anazaliwa Mtwara, hivyo ni Mmakonde, mama yake anazaliwa Bukoba.
“Nimekwambia suala hili, nikitamani ufunge safari uende Bukoba, Kijiji cha Muyaba, ukazungumze na mama wa Hamis, ambaye ni Rukia. Mazungumzo haya yatakuwa fundisho kwa familia nyingine jinsi ya kulea watoto. Sisemi, ndivyo ilivyo, ila Gazeti la JAMHURI nawapongeza jinsi mlivyoshughulikia suala la mauaji ya Naomi, nawaomba muingie gharama kidogo mlikamilishe,” amesema mtoa habari wetu.
Siku hiyo hiyo, nikaamua kukata tiketi ya kwenda Bukoba. Jumatano Agosti 7, 2019 niliamka saa 9 usiku kusali Rozali ya Matendo ya Mungu. Sikulala tena. Nikaoga na kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Saa 12:45 asubuhi, na kwa kupitia Mwanza, tukafika Bukoba saa 03:30 asubuhi.
Nilipokewa na rafiki yangu Godwin Tegamaisho, maarufu kama Tenende. Aliponipokea Uwanja wa Ndege Bukoba, tukamtafuta rafiki mwingine Wilbard, maarufu kama Muyaba. Tukaanza safari ya kwenda Kijiji cha Muyaba, kilichopo yapata kilomita 20 kutoka Bukoba Mjini. Tulifika Muyaba kama saa 06:00 mchana.
Kwa bahati mbaya, wenyeji waliotupokea Kijiji cha Muyaba wakatwambia hakuna mtu anayeitwa Rukia au Victoria. Baada ya kusugua vichwa, akatokea mtu mmoja akasema yupo mama alipata kuishi Dar es Salaam, ila anaitwa Bitoria Emmanuel. Na kwamba huyu ni mkazi wa Kijiji cha Rwome. Nilimpigia simu Mchungaji Luwongo, baba wa Hamis kuhoji tena ni kijiji kipi anatokea aliyekuwa mke wake, akanijibu kuwa ni Rwome.
Baada ya jibu hilo, nilianza tena safari ya kwenda Rwome, yapata kilomita 2 kutoka Muyaba, karibu na vijiji vya Kangoma na Ntao. Rwome ni kijiji nilichoambiwa wakazi wake wanaishi kwenye familia 32 tu kijiji chote. Nilipata kijana mwenyeji aliyetupeleka hadi nyumbani kwa mama Victoria Emmanuel. Tulifika kwake yapata saa 08:27 mchana.
Mama Victoria, maarufu kama Bitoria, alitupokea kwa uchangamfu wa hali ya juu. Tulimweleza nia ya ujio wetu, na tukamweleza juu ya kisa cha mauaji anayodaiwa kufanya mtoto wake Hamis. Nilianza kwa kumhoji iwapo anafahamu na iwapo ana taarifa za kifo cha Naomi. Mama huyu alianza kwa kusema:
“Hamis alinipigia akaniambia mke wangu [Naomi] hayupo amepotea. Baadaye nikaulizia ameishaonekana, akaniambia bado, mara akanipigia simu kwamba naitwa polisi. Mimi navisikia tu kwa mdomo, sijapata ndugu wa kunieleza nini kilitokea hasa, hata mume wangu hajanieleza. Baba mzazi hajanieleza chochote, nasikia kwa watu, mume wangu hajanieleza chochote.”
Victoria, mama mzazi wa Hamis, alitengana na mume wake mwaka 1983, ikiwa ni miaka miwili baada ya Hamis anayetuhumiwa kumuua mkewe azaliwe. Anasema yeye na mumewe kwa muda mrefu hawana mawasiliano ya karibu. “Nilikwenda kudai mali yangu, aliniacha Abdiel akiwa na miaka miwili, nimemlea hadi miaka 10. Nilifika baada ya hapo kudai haki yangu ya mashamba ya Kibugumo. Nashukuru serikali ilinitetea nikapata haki yangu,” amesema.
Tangu watengane na mumewe, Mchungaji Luwongo, ilimchukua hadi mwaka 2015 kupata haki yake. “Mwaka 2015 serikali ilinitetea nikapata haki yangu. [Mchungaji Luwongo] aliponipa haki yangu nikawagawia watoto hapo hapo Kibugumo na Kitongoji cha Mwela,” amesema.
Amesema baada ya kuwa ameachana na Mchungaji Luwongo, alirejea kijijini Rwome, ambako maisha yalikuwa magumu. Ilimbidi aachane na Uislamu na kurejea kwenye dini yake ya awali ya Ukristo. Pia alipata msaada wa kujengewa nyumba na walokole.
Anakumbuka mwaka 2015 siku alizoishi kwa mwanae Hamis, hakuona dalili za ugomvi na mkewe Naomi. “Sikuona ugomvi siku nilizomaliza. Walikuwa huyu anakwenda kazini, hakuwa na mfanyakazi mke… nilikuwa naosha vyombo, tunaishi, hakuwa na mfanyakazi, sikuona ugomvi wa aina yoyote,” amesema.
Mama Victoria amesema tangu Hamis akumbwe na matatizo ya tuhuma za mauaji, mdogo wake Hamis (Abdiel) anayeishi Dar es Salaam hajazungumza na mama yake. “Sofia [mtoto wangu mwingine] naye tulizungumza siku moja. Tunasikia kutoka redioni na magazetini. Gazeti hili [la JAMHURI] ndilo limenipa taarifa sahihi za mauaji haya. Gazeti nalitunza, naangalia, gazeti lililetwa na Mlokozi.
“Mzazi mwenzangu hataki kunijulisha, mtoto mdogo wake hataki kunijulisha,” amelalamika.
Huku akibubujikwa machozi, Mama Victoria akazungumzia wema wa Naomi: “Mikoba yote ninayoishika kwenda kanisani nimepewa na Naoni. Sikukuu ya Krismasi amenitumia Sh 20,000, na baadaye akanitumia Sh 20,000 ninunue vitenge nishindie, nikanunua dawa za sukari inayonisumbua.
“Sijui kama nitakanyaga Dar es Salaam tena. Yeye (Naomi) ndiye alikuwa mama, anasema mama, amefika. Mume mwenzangu alinijibu akasema usikanyage hapa tena. Sitarudi tena Dar es Salaam… Kwa upande wangu mimi, Naomi alikuwa msaada. Mikoba niliyonayo, ya Naomi, magauni. Kama amefariki nimepoteza. Alikuwa ananihudumia kama mama yake.”
Nilimuuliza tena, katika simu aliyopigiwa na Hamis juu ya kifo cha Naomi alimwambiaje, Mama Victoria akasisitiza: “Aliniambia hivi, mke wangu amepotea mama, sasa hivi anachukua wiki. Nikamuuliza je, mtoto? Akasema amechukuliwa na shangazi yake. Kazi? Akasema kazini hayupo. Nikamuuliza kwa mama yake? Akasema huko kote nimeishafika. Nikamwambia wanawake tuna mengi, anaweza kuwa kwa mwanaume mwingine. Akasema nampigia simu hapokei… baadaye [Hamis] akanipigia simu akasema wananiita polisi Jumatatu. Mpaka leo sijazungumza naye.”
Alipododoswa kama kweli familia ilikuwa shwari bila tatizo, akasema: “Miaka 3 iliyopita nilisikia ugomvi kwa watu, kwa dada zake kwamba waliwahi kugombana na mwanaume alitaka kumchoma kisu, sijui kufanyaje. Kuja kuyapata hayo nanung’unika… nikajiuliza vitu walivyo navyo, wanakosa mfanyakazi wa ndani? Hili lilinishitua. Nikawauliza kwa nini wakose mfanyakzi wa ndani? Hamis akasema mama mkorofi huyu (mwanamke), mfanyakazi hawezi kukaa humu ndani na hela zote walizonazo, zote…”
Kuhusu malezi ya watoto, alipohojiwa kama anaamini aliwapa watoto wake malezi mazuri, Mama Victoria akasema: “Mmmmh, tulipotengana nilikuja nao huku wote. Mchungaji Luwongo akatuma mwanae na mwanangu (Julius – alifariki). Nilikuwa nimelima michele, viazi… aliwachukua mwaka 1984 akawachukua. Sofia, nilimzaa 1978. Na kwa kweli wamekosea, mwaka wa kuzaliwa kwa Hamis ni 1980. Naona tulipotengana watoto hawakupata malezi mazuri.”
Mama Victoria, Mungu alimjalia watoto 10, ila kwa kuolewa na wanaume wanne tofauti. Anao watoto aliowazaa na mwanaume wa kwanza aliyefahamika kwa jina la Bartazer. Hawa ni Burchard, Julius, Shukuru (Sospeter) na Zelida. Mume wake wa kwanza alikuwa wa Kijiji cha Igombe, Kitongoji cha Bulamula.
Baada ya hapo alizaa watoto wawili na mwanaume aliyekuwa anafanya kazi Benki Kuu, aliyefahamika kwa jina la Tibashengwa [DB1] , ila kwa bahati mbaya aliwakataa watoto; Adelina na Novat – Tibashengwa.
Kwa Mchungaji Luwongo alizaa watoto watatu ambao ni Sofia, Hamis na Abdiel. “Nilipokuja hapa [baada ya kutalikiana na Mchungaji Luwongo] nikakutana na mwanaume mwingine, tukazaa mtoto mmoja Justa France, yuko Dar es Salaam. Niwe wenzindo. Bana 10 (Ndiye wa mwisho. Watoto 10).
Pia, lipo jambo la kushtua kidogo. Mama mkwe wa Naomi, alikuwa hafahamiani na wazazi wa Naomi pamoja na mke huyo kuishi na mtoto wake zaidi ya miaka 7. “Ukweni, nilimwambia [Naomi] unipe anwani, akasema mama yake anatokea Kihanja, Bukoba. Nikamwambia unipe anwani nimpigie simu, kuna mjukuu wangu Kasigwa, akasema mama yake alifariki. Nikamwabia nitafika nauliza nifike. Alikataa kunipa hiyo anwani.”
Mawasiliano kati ya Mama Victoria na watoto wake si mazuri pia. “Nimemwambia mjukuu afute namba ya…(jina linahifadhiwa),” amesema. Alipoulizwa iwapo ana nia ya kumsaidia mtoto wake Hamis katika kesi ya mauaji inayomkabili, akasema: “Sina jinsi ya kumpa msaada, nipo mbali, sijasikia kesi yake anavyoiendesha… siku hizi kuna matukio mengi, mke anaua mume kwa bisibisi, kwa hiyo yanayotendeka katika nchi hii yamezidi. Maombi sijaacha, naendelea nayo, sina jinsi ya kutetea mambo hayo, kwa kuwa sijaonana naye uso kwa uso. Mungu ndiye anayejua.”
JAMHURI limemuuliza nini kilimfanya Mama Victoria atengane na Mchungaji Luwongo, akasema tatizo alikuwa mama mkwe: “Akawa anasema watoto wangu wa mwanzo, kwamba nimeleta mirija. Huruma ndiyo iliyoniponza. Kumhurumia, balya bwaigoro, balya limo Lindi, mbenu inye ngila nti, olete mazaile, yampinduka (huwa wanakula jioni, wanakula mara moja Lindi, sasa mimi nikasema kwamba, amlete mzazi, mzazi akanigeuka). Nilikuwa mimepanda migomba, nilikuwa nauza ndizi, akaona mali imekuwa nyingi, akasema nimeleta mirija niiondoe. Watoto wangu anawaita mirija? Nikaondoka kweli.”
Ameongeza kuwa mama wa Mchungaji Luwongo, alikuwa “anajifanya Mpiga Ramuli, alikuwa amejenga vijumba vidogo. Kwa siku alikuwa anapigia ramuli watu 6 hadi 7, akala akanenepa na kusahau mimi niliyemleta.”
Anasema walikuwa na nyumba Keko Mwanga, lakini Mchungaji Luwongo aliiuza vikabaki vyumba viwili, havina choo ndimo watoto hao wakawa wanaishi. “Walikuwa wananiita wanakata hela ya kulipia kujisaidia chooni kwa jirani. Sikupata nafasi ya kuwafunda watoto. Walikuwa wanaangua nazi, Abdiel, alikuwa na miaka 10, ndipo nilipomwingiza shule na Hamis akalazimika naye kuingia shuleni (Kibugumo), akaanza kuuza nazi Kigamboni, na baadaye nazi Mbeya.
“Malezi yalipungua… alikuwa ameishapata mwanamke mwingine. Alimtuma mzee Madadi, Shabani akaja hadi hapa, akasema anataka watoto wake. Hamis, Sofia, waliondoka, Abdiel alibaki kwa kuwa alikuwa ananyonya. Nilikata nyasi, nikapata nauli, nikampelekea mwanae. Kumfikisha, nikakuta anachunga ng’ombe. Kama isingelikuwa mimi kuniogopa kuwa ni mkorofi, basi asingekwenda shule,”amesema.
Alipoulizwa kama ana ushauri kwa wanandoa, akasema: “Sasa kama ni kusema, niseme nini? Aliyechoma ni mwanangu, aliyechomwa ni mwanangu, lakini wasifanye hivyo, wanatuumiza sisi wazazi (analia).”
Kuhusu mwisho wa ndoa yake na Mchungaji Luwongo, akasema: “Kitendo alichonitendea mume wangu, si vyema. Niliasi nikawa Mwislamu, jina langu amelitamka kwamba ni Rukia, nilipokuja hapa akanitumia barua ya kuniacha. Nikabadilisha kadi Kashekuro, nilikuwa naitwa Rukia, nikarejea jina langu Victoria, mpaka jina langu linafahamika. Tuwe wabaya au wazuri, lakini ninachowaambieni, wanaume msiache mke mkaacha na watoto wake, na haya yaliyotokea mimi nalia. Mkwe wangu ni mtoto wangu. Alipaswa kusema aje, tuyakalie kikao tuyazungumze.
“Kwenye ndoa yake alikataa kuja, akasema anaumwa, hatukuonana uso kwa uso akanitumia mtoto wa ndugu yangu. Unaweza kukuza mtoto hadi miaka 20, miaka 30, mtoto hajaumwa, mpaka leo imefikia hatua hii? Sijui ni kweli amemchoma kweli? Lakini mume wangu, natangaza, usiache mke ukaacha na watoto, watoto wanakuwa hawana malezi. Hawana malezi yoyote. Mtoto atafanya anavyojua yeye. Mkiachana, sikilizaneni, mjue mtoto anatenda nini.
“Kumbe yeye ugomvi anaujua, kwa nini asinipigie simu akaniambia wanataka kuachana? Ningelisema. Anajifanya eti mchungaji, mchungaji gani usiyejua mke? Anasingizia mama yake, roho yake mwenyewe. Mama yake asimsingizie.”
Dada wa kambo wa Hamis, Zelida Bartazar, amezungumza na JAMHURI na kusema: “Sijui amerogwa? Amefanya nini Mungu wangu? Kama ameua kweli Mungu ndiye ajuaye. Huyo baba yake, mchungaji, mtoto Hamis alipomwambia mke wake amepotea alichukua hatua ipi? Hapo katikati kuna nini humo? Kuna nini?”
Mei 15, mwaka huu, Hamis Luwongo anatuhumiwa kuwa alimuua na kumchoma moto mkewe, Naomi kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, kisha akaenda kuzika mabaki ya mwili wa Naomi katika Kijiji cha Maragoro, Mkuranga. Kesi yake ilitajwa na leo Hamis anafikishwa tena mahakamani Kisutu, Dar es Salaam kuendelea kupambana na tuhuma hizi.