Mfuko wa Wanyamapori Africa (AWF) umesaidia wakulima wa mpunga na kokoa Kilombero kupitia Mradi wa Ukuaji wa Kilimo Shirikishi na Endelevu Kilombero katika kutoa elimu ya mnyororo wa thamani ili kuwa na kilimo chenye tija.
Katika mradi huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2017, AWF pamoja na wadau wengine imewezesha wakulima zaidi ya 500 katika kupata mbegu bora za kokoa na mpunga. Katika mradi huo shirikishi wakulima pia wanachangia mboji na kuandaa vitalu.
Akizungumza katika kilele cha Sikukuu ya Nane Nane mkoani Morogoro, Meneja Miradi wa AWF, Pastor Magingi, amesema tangu kuanza kwa mradi, zaidi ya Sh milioni 600 zimetumika katika elimu na mafunzo kwa wakulima.
“Mradi huu umewezesha kuelimisha wakulima wadogo wa kokoa na mpunga juu ya kilimo endelevu. Tumelenga zaidi katika mnyororo wa thamani hasa katika kuongeza ubora, matumizi bora ya ardhi na utunzaji mazingira,” amesema.
Ameongeza: “Lengo la mradi ni kuona kuwa kabla ya mradi kufikia ukingoni mwaka 2020 wakulima wengi wawe wamenufaika hasa kwa kujiongezea kipato cha kaya na mtu mmoja mmoja.”
Kwa mujibu wa maelezo yake, mafanikio katika mradi wa mpunga yameonekana kwa kuwa wakulima wameweza kupata na kutumia mbegu bora zinazozaa sana ili kupata mavuno ya kutosha.
Magingi amesema kabla ya mradi, katika ekari moja mkulima alivuna magunia 18 tu, lakini baada ya ushauri wa kiufundi na matumizi ya mbegu bora ekari moja inazalisha magunia 24 kwa wale wanaotegemea mvua na magunia 35 kwa waliounganishwa na mfumo wa umwagiliaji.
Licha ya kilimo cha mpunga na kokoa, mradi pia unajishughulisha na kuwezesha vikundi vidogo vikiwemo vya ufugaji nyuki, usalama wa maji na kilimo cha miwa.
Katika kuongeza thamani ya zao la mpunga, mradi unakusudia kuleta mashine za ‘solar’ ili kuwezesha wakulima kukausha mpunga hasa kipindi cha mvua.
Kwa mujibu wa Magingi, mradi umelenga kufikia wakulima zaidi ya 2,000 ili wanufaika wawe wengi zaidi kutokana na ukweli kwamba kilimo ndicho kimeajiri kundi kubwa zaidi kuliko sekta nyingine nchini.
AWF wamekuwa wakiendesha shughuli zao hizo katika vijiji 16 vya Tarafa ya Mgeta vilivyomo pembezoni mwa Hifadhi Asilia ya Kilombero na Udzungwa. Mradi huo hufadhiliwa na mashirika wadau ya BMZ/GNF ya nchini Ujerumani.