Niliposoma maneno hayo katika Gazeti la Mwananchi toleo Na. 5098, Jumanne, Julai 8, 2014, ukurasa wa mbele (na maelezo uk. 4: Siasa) nilipigwa na butwaa!  
Lakini nilitaka nijiridhishe na kile nilichokisoma kwa kuwapigia simu wahusika — Gazeti la Mwananchi. “Haya mliyoandika mna hakika yametamkwa na Dk. Wilbrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)?”
Nikajibiwa, lililoandikwa na unachosoma ndicho tulichopokea kutoka kwa Dk. Slaa! Nikatuwama pwaa!
Akili yangu ilinirudisha nyuma wakati wa utawala wa Warumi kule Yerusalem pale Pilato kwa kiburi cha utawala alipotamka, “Quod Scripsi, scripsi” maana yake niliyoandika nimeyaandika (Yoh. 19:22).
Basi, mimi baada ya kusikia Dk. Slaa aliyatamka hayo yaliyoandikwa – “Makapi ya CCM” nikasema, ai, kumbe! Ni matamshi ya kiburi cha Pilato! Hapo basi nikajaa mawazo mengi juu ya uongozi wa juu wa Chadema.  
Wazo moja linanisumbua, je, ni kweli viongozi wakuu na wasomi hawa wanaweza kuwaita binadamu wenzao makapi? Kwa nini viongozi wakuu wa Chadema wanajaa ufedhuli (arrogance) namna hii? Hawawezi kuchagua maneno mazuri zaidi kuliko haya yenye kukashifu wanadamu wenzi wao?
Nikaanza kutafakari neno hili makapi. Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu tunasoma ‘kapi’ lina maana ya pumba, mabaki ya nafaka, takataka, chua. ‘Kapi’ huweza kumaanisha, mapepe au mambeta. Na kwa lugha za mitaani kapi ina maana kutokuwa makini katika utendaji, kutokuwa na mawazo tulivu.
Kwa namna ilivyotumika hapa, makapi ni mabaki yasiyokidhi vigezo vinavyotakiwa. Kwa Kiingereza huitwa ‘rejects’ yaani kilichokataliwa, kibovu, hafifu, duni.
Kwa maana hiyo basi, naona si sahihi kabisa watu hao kuitwa ‘makapi’. Lakini Dk. Slaa alinukuliwa kusema, “Kutokana na tamaa ya kuingiza watu wengi kwenye Bunge, vyama vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwapokea wanachama wa CCM wanaoshindwa kwenye kura za maoni na baadaye kuwapa nafasi ya kugombea ubunge, lakini safari hii hawatakuwa tayari kufanya hivyo”. Hapo niliachwa hoi na kutafakari mantiki ya haja namna hii. Kumbe, yeyote anayeshindwa kwenye kura ya maoni ni kapi!
Kwa mtazamo huo wa Dk. Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema, nikarudi nyuma (recall) kukumbuka yaliyompata katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa ubunge kule Karatu mwaka 1995. Dk. Slaa huyu huyu akiwa mwana-CCM damdam alichuana na mwana-CCM mwenzake, Patrick Qorro (Mungu amrehemu) kuwania Jimbo la Karatu.
Kura za maoni Wilaya ya Karatu, na Mkoa wa Arusha ziliwapambanisha wana-CCM hao safi kwenye uteuzi wa mwisho wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Astaghafirulah! Jina la Dk. Slaa mwana-CCM safi likatupwa (rejected) na jina la Qorro likateuliwa. Je, Dk. Slaa anakumbuka alipokeaje uamuzi huo wa NEC Taifa mwaka 1995?
Hatua ya kwanza ya Dk. Slaa ilikuwa kuhama kutoka CCM na kwenda kwenye upinzani – Chadema ambako alifanikiwa kuwa mbunge na kumgaragaza vibaya Qorro. Kwa maneno ya sasa ya Dk. Slaa (going or judging by the yard slick of Dr. Slaa himself) ni sahihi kabisa NAYE NI MAKAPI YA CCM. Ni rejects wa CCM mwaka ule wa 1995.
Je, ina maana hafai kwa uongozi kwa vile amekuwa kapi kutoka CCM? Mbona alifanikiwa kupata ubunge wa Karatu, na hivi sasa ni Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani? Kama hakuwa mmoja wa makapi aeleze aliingiaje kwenye chama cha upinzani na alitokaje kule CCM?
Je, kuna tofauti gani kati ya namna alivyotoka yeye CCM na namna walivyotoka akina John Shibuda, aliyeshindwa katika kura za maoni kule Maswa Magharibi au Freddy Mpendazoe kule Segerea?
Dk. Slaa anajitetea kwa kusema, “Tatizo lile lilitokana na ugeni”. Ninamuliza, ugeni wa kutoka wapi? Je, mwaka 1995 upinzani katika Chadema haukuwa na hilo tatizo la ugeni? Mbona, daktari mzee anajichanganya kwa blablaa zisizo na mashiko (kisilogism?).
Hebu tutafakati maneno haya katika Biblia Takatifu Bwana wetu Yesu Kristo anasemaje juu ya unafiki na upofu wa wanadamu. Tunasoma maneno haya, “Basi mbona wakitazama kibanzi kilichokuwa ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huangalii? (Luk. 6:41). Yeye mwenyewe ni kapi (reject) wa CCM, lakini anawaona wenzake sasa kuwa makapi ya CCM! Jamani, binadamu kweli hatujijui na tu rahisi kusahau tulikotoka! Hapa Dk. Slaa hakuwa na sababu za msingi kutamka maneno yasiyostahili namna hii.
Enzi za utumwa wa Mwarabu walikuwapo manokoa, wale watumwa wazoefu. Hawa manokoa walikuwa wakatili kwa kupiga watumwa wenzao kuliko Waarabu mabwana wenyewe. Hapa sasa nokoa, kapi la CCM kwa uzoefu wake wa siku nyingi kwenye upinzani anakuwa mkali zaidi kuliko waasisi akina mzee Edwin Mtei wa hivyo vyama vya upinzani!
Hoja yangu ya pili kwa uongozi wa juu wa vyama vya upinzani ni matumizi potofu ya maneno au misamiati. Wachague maneno ya staha na ya kiutu. Nilishangazwa wakati mmoja Mheshimiwa David Kafulila alipohoji mambo fulani fulani katika chama cha Chadema kuhusu uongozi wa juu wa chama.
Dk. Slaa inasemekana alijibu kwa mkato kabisa na kwa dharau kuwa hawezi kujibizana na ‘sisimizi’. Hapo ni wazi neno ‘sisimizi’ kwa binadamu siyo sahihi; kwa kadiri ya imani yetu ya Kikristo inajulikana kuwa mwanadamu aliumbwa na Mungu. Neno la Mungu linasema hivi; Mungu akasema, “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; (Mw. 1:26) kwa hiyo Kafulila na Slaa wote ni sawa kwa maana wameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu!
Basi, kumtusi mwenzako kuwa ni ‘sisimizi’, inamaanisha nawe unayetamka hayo u sisimizi, sivyo? Imani ya kwanza ya CCM sote tunaijua inasema hivi, ‘Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja’. Kwa maneno mengine inasema ‘Binadamu wote ni sawa’. Sasa kwa imani yetu hiyo na kadiri ya haki za binadamu, tunajua kila mwanadamu yu sawa kabisa na mwanadamu mwingine.
Kwa hiyo, si sahihi hata kidogo kiongozi wa chama kumwita mwanachama au mtu mwingine yeyote jina lisilofaa kama hivi ‘sisimizi’ au ‘kapi’, hivyo nashauri viongozi wa juu wa Chadema wajitahidi kuonesha utu wao hata katika matamshi ya kila siku. Je, wakijashika dola watatuitaje sisi?
Kwa fikra zangu, kuna mitazamo tofauti kati ya viongozi wa juu wa Chadema. Katibu mkuu amewahi kutamka eti Kafulila ni sawa na sisimizi tu. Mwenyekiti wa Chadema katika harakati za kuhalalisha ndoa ya UKAWA anamteua Kafulila kuwa Waziri Kivuli katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hapo tueleweje mwenendo wa uongozi wa Chadema?
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 baadhi yetu tulikuwa tunajiuliza ni kwa mtaji gani Chadema wanaweza kumudu kutumia chopa (helikopta) kujinadi? Jibu la rahisi tuliambiwa wapo vigogo kule Moshi wanafadhili uchaguzi huo.
Wengine tulikuwa kama akina “Tomaso (a doubtful Thomas), ni kweli nchi hii ina vigogo wa kuhimili gharama kubwa namna ile? Kutegemea ruzuku haingewezekana, maana bungeni wajumbe wengi walikuwa ni wa CCM, wakifuatiwa na wa CUF, hivyo Chadema ruzuku yao kutoka serikalini kamwe isingaliwawezesha kumudu gharama zile.
Ilikuja kutokea hisia ya fedha kutoka nje ya nchi. Ufadhili wa Wazungu wa Ulaya. Basi, dhana (speculation) ya baadhi yetu ililenga chama cha Liberal cha Uingereza, walioonesha urafiki kwa Chadema. Kumbe juzi juzi hapa Ijumaa Julai 4, 2014, kigogo mmoja wa Chadema katufumbua macho.
Ilikuwa ni katika kipindi kile cha katika Star TV, “Tuongee Asubuhi” wakati Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke katika majadiliano na Mkurugenzi wa Sera na Utafiti katika chama hicho yalifichuka madudu!
Mwenyekiti yule alikosoa uongozi wa mabavu au ubabe katika Chadema. Na alisema wazi wazi kuwa Chadema wanafadhiliwa na CDU (Christian Democratic Union) cha Ujerumani. Mwenyekiti alisema Chadema waliomba fedha kwa Uchaguzi Mkuu na wakaletewa fedha nyingi tu.
Kwa mshangao wa kiongozi yule, kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha zile na matanuzi kwa viongozi. Kwa masikitiko sana, mwenyekiti yule alisema haelewi kwa vipi chama chake kimeshindwa hata kujenga ofisi ya makao makuu ya chama hicho kwa fedha zilizokuwapo.  
Lakini kwa mshangao akasema CUF wamejenga ghorofa kule Buguruni yaliko makao makuu yao. NCCR-Mageuzi wamejenga ofisi za makao makuu pale Ilala, lakini Chadema pamoja na mbwembwe nyingi za kuruka na chopa hawana jengo lao la ofisi za makao makuu. Ile dhana au hisia kuwa Chadema walikuwa wanafadhiliwa na nchi ya Ulaya sasa ikawa ni kweli, maana hapo kilitajwa chama cha CDU cha Ujerumani.
Pili, wakati wa mazungumzo yale katika Star TV, mwenyekiti huyo alitoboa siri ya chanzo cha UKAWA. Alisema CDU iliwaagiza Chadema waungane na CUF na NCCR-Mageuzi wenye wabunge katika Bunge la Jamhuri kupata nguvu kuu ya kumudu mjadala wa Katiba. Kumbe sasa tunaona UKAWA imeanzishwa kwa shinikizo la wakubwa kutoka nje ya nchi.
Ndiyo tuseme UKAWA si msukumo wa wanachama wenyewe. Na kwa sababu ya shinikizo namna hiyo, yale maneno ya mwenyekiti wa Chadema kule kwenye Baraza Kuu la Januari 28, 2013 pale Diamond Jubilee, Dar es Salaam kuwa CUF ni CCM ‘B’ na Mheshimiwa Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa na Rais ni CCM ‘B’; sasa yamesahaulika na akalazimika kuyameza matapishi yake kukidhi matakwa ya CDU wafadhili kutoka Ujerumani.
Ikabidi hata yule ‘sisimizi’ wa katibu mkuu awe mmoja wa mawaziri kivuli katika Bunge kwa upande wa wapinzani. (Siri nzito UKAWA – UHURU toleo Na. 21862 la Jumamosi tarehe 5 Julai 2014 Uk. 1-2)

Itaendelea