Familia ya Naomi Marijani (36), imefanya maombolezo kwa ibada maalumu baada ya kuthibitika kuwa binti yao ameuawa.
Ingawa haijathibitika nani kamuua (kwani kesi ndiyo imeanza), pamoja na mume wake kukiri mbele ya polisi kuwa alimuua na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa nyumbani kwake Gezaulole, Kigamboni, Dar es Salaam na kisha kuzika mabaki shambani kwake Kijiji cha Marogoro, Mkuranga, taarifa za uhakika zinasema vinasaba vilivyopatikana katika mabaki yaliyopatikana shambani (DNA) vimethibitika pasipo shaka kuwa huo ulikuwa mwili wa Naomi.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, amezungumza na JAMHURI akaliambia yeye kwa upande wake “amemaliza kazi ya uchunguzi” ila matokeo ya kilichopatikana ameyawasilisha kwa waliompatia kazi hiyo, kwa maana ya polisi, hivyo hawezi kuzungumzia matokeo ya uchunguzi huo gazetini.
Vyanzo vya uhakika kutoka sehemu mbalimbali vimelithibitishia JAMHURI kuwa mabaki yaliyotolewa shambani, eneo ambalo mume wa Naomi, Luwongo, aliwapeleka polisi, vinasaba vyake (Naomi) vimeshabihina moja kwa moja na vya mtoto wake, Gracious, ambaye zilichukuliwa sampuli kutoka kwake.
“Ni hatua, hatuwezi kuzungumza kwa sasa ila uchunguzi umekuwa positive (chanya). Hii ni hatua katika kuhakikisha haki inatendeka,” amesema mmoja wa watoa habari wetu.
Licha ya uchunguzi wa mabaki ya mwili wa Naomi Marijani anayedaiwa kuuawa na kuchomwa moto na mumewe, Hamis Said Luwongo, maarufu kwa jina la Meshack, kukamilika kwa upande wa Mkemia Mkuu wa Serikali, mabaki hayo yameshindikana kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya ‘maziko’.
Awali ndugu waliomba kupewa mabaki kwa sharti la kupewa kibali maalumu na polisi kwa nia ya kuyazika kwa heshima zote za binadamu, hata hivyo, polisi walisema: “Kwa ugumu wa kesi hii, na kwa nia njema, ni vema mabaki haya yakatolewa kwa kibali cha mahakama,” kimesema chanzo chetu kingine.
Katika hatua za awali za familia ya Naomi kuomba mabaki ya mpendwa wao huyo kwa ajili ya taratibu za maziko hasa baada ya Mkemia Mkuu wa Serikali kukamilisha uchunguzi wa sampuli za mabaki ya mwili wa Naomi, maombi maalumu yaliwasilishwa.
Familia ilichukua hatua hiyo Agosti Mosi, 2019 kwa kuandika barua juu ya ombi la uthibitisho wa masalia ya Naomi pamoja na idhini ya kisheria ama ya kimahakama ili hatimaye waweze ‘kuzika’ baada ya uthibitisho wa kisayansi.
Hata hivyo Ofisi ya Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZCO) licha ya kupokea maombi ya familia hiyo ilichukua hatua nyingine kadhaa ikiwa ni pamoja na kuomba idhini ya kimaandishi kutoka mamlaka nyingine yenye dhamana ya kujibu maombi husika ya familia.
Agosti 3, 2019 familia ilipokea mrejesho kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwamba idhini iliyoombwa na familia ya kukabidhiwa masalia ya mwili wa Naomi ni ya kisheria, na inapaswa kutolewa na mahakama.
Hayo yote yalifanyika huku tayari kuna taarifa rasmi iliyotolewa na wakili wa serikali mahakamani, Julai 30, 2019 kwamba upelelezi haujakamilika.
Kutokana na mlolongo huo, familia ilibadilisha ratiba yake kwamba badala ya kufanya ibada ya ‘maziko’ ya mabaki ya mwili wa Naomi, basi ifanye ibada ya shukurani kwa ajili ya kitendo cha kubainika nini kilimfika Naomi.
Na Agosti 4, 2019 familia imeendesha ibada nyumbani kwa kaka wa marehemu, Wiseman Marijani, Mbweni jijini Dar es Salaam.
“Tunawaalika watu wote kushiriki ibada ya kumshukuru Mungu kutufikisha kujua alipokuwa amefichwa Naomi na kumuomba Mungu asaidie haki itendeke mapema ili familia tupewe masalia ya mwili wa marehemu tuyazike kwa staha,” amesema Marijani.
Maneno ya familia
Akitoa neno la shukurani baada ya ibada hiyo, Msemaji wa Familia, Wiseman Marijani, ambaye pia ni kaka wa Naomi, amesema: “Tunayo imani kubwa sana na Serikali ya Rais John Magufuli na vyombo vyote vya dola, tunaamini vitasaidia ili haki ya Naomi ipatikane.
“Kwa sababu shauri hili limo mikononi mwa mahakama, hatutapenda kulizungumzia kwa namna ya kuingilia mahakama. Lakini tunaiombea mahakama kwa Mungu. Wote watakaohusika na suala hili katika mahakama au popote tunaomba hofu ya Mugu iwaongoze.
“Sisi familia tunaendelea kusikiliza maelekezo ya mamlaka husika zenye dhamana ya kutoa idhini kisheria kwa familia ili hatimaye kutupatia masalia tuweze kuyapumzisha kwa amani.”
JAMHURI limekuwa likifuatilia suala hili tangu awali kwa kuhusisha uchunguzi maalumu wa namba ya simu ya mtuhumiwa na kubaini kuwapo kwa mawasiliano yanayozua maswali mengi kiasi cha gazeti hili kuonyesha katika moja ya habari zake za uchunguzi kuhusu mauaji hayo, kwamba mtuhumiwa namba moja kuhusu kutoweka kwa Naomi ni mumewe, Hamis Luwongo.
Siku moja baada ya JAMHURI kuandika habari za uchunguzi, Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa likamhoji na kutoa taarifa kwa umma iliyomweka matatani mtuhumiwa. Mtuhumiwa amefanyiwa uchunguzi zaidi wa kipolisi uliobaini mambo kadhaa ikiwano Naomi kuuawa, kuchomwa moto eneo la Kigamboni na mabaki ya mwili wake kwenda ‘kufukiwa’ Kijiji cha Marogoro, Vikindu, Mkuranga.
Nyuma ya uamuzi huo ni mazingira halisi ya tukio lililomfika Naomi, mama wa mtoto mmoja, Gracious, mwenye umri wa miaka sita.
Gazeti hili la JAMHURI limeelezwa kuwa katika hali ya kawaida kuhusu kesi za mauaji, mara nyingi taarifa ya uchunguzi baada ya kifo inayofanywa ya kidaktari (postmortem) kwa mwili wa mtu aliyeuawa ndiyo hutumika kama mbadala wa kuendelea ‘kuushikilia’ mwili huo kama moja ya vielelezo ama ushahidi katika mwenendo wa kesi husika, lakini katika suala la Naomi, mambo ni tofauti.
Katika suala la Naomi, mwili haukupatikana, hivyo hakuna taarifa ya ‘postmortem’, bali kilichopo ni sampuli za mwili wake na ripoti ya uchunguzi wa kisayansi (DNA Report), hivyo hakuna namna zaidi ya kuhifadhi mabaki hayo kwa ajili ya mchakato zaidi wa uchunguzi na mwenendo wa kesi mahakamani.
Tayari mtuhumiwa wa mauaji hayo, Hamis Luwongo, amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka kwa kosa la mauaji chini ya Kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Mashitaka yalisomwa Julai 30, mwaka huu na Wakili Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Simon, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kuwa mshitakiwa alimuua Naomi Mei 15, 2019 huko nyumbani kwao Gezaulole, Wilaya ya Kigamboni huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Katika hatua ya sasa kisheria, kesi itaendelea kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hadi Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakapokamilisha kazi ya kupitia jalada la kesi hii na kuamua iwapo kuna kesi ya kujibu au la.
Ikiwa DPP au mwakilishi wake atabaini kuwa kuna kesi ya kujibu, basi mtuhumiwa ataandikiwa amri ya kufikishwa mahakamani, ambako atasomewa mashitaka na kuelezwa ushahidi utakaotumika dhidi yake.
Katika hatua hiyo, atapewa fursa ya kutamka jambo lolote, lakini ataonywa kuwa lolote atakalolisema linaweza kutumika dhidi yake wakati kesi hiyo ikianza kusikilizwa katika Mahakama Kuu.
Utaratibu huu wa kusomewa mashitaka ya awali unatokana na Kifungu cha 245 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka (kama ilivyorekebishwa mwaka 2002), kinachoipa mamlaka Mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi kumfungulia mashitaka ya awali mtuhumiwa (Committal Proceedings) wakati polisi wanakamilisha uchunguzi na kupeleka jalada lake kwa DPP kuandaa mashitaka ikiwa DPP au mwakilishi wake atajiridhisha kuwa kuna kesi ya kujibu kwa mtuhumiwa.
Ikiwa Hamis Said Luwongo atatiwa hatiani, Kifungu cha 25 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kinatamka kuwa adhabu ya mauaji ni kifo. Kifungu cha 26 cha sheria hiyo, kinamtaka jaji anayetoa adhabu hiyo kutamka bayana kuwa mtuhumiwa amehukumiwa kunyongwa kwa kitanzi hadi kufa.
Wiki iliyopita Gazeti hili la JAMHURI limechapisha mahojiano na baba wa Hamis, Mchungaji Said Luwongo, aliyesema mtoto wake Hamis aliishaanza kuona kuwa mwenendo wake maisha yake haukuwa mzuri, aliposema miaka mitatu iliyopita, Hamis amepata kutubu kwake akisema anataka kuachana na kutenda maovu: “Niliongea naye hapo katikati akanikubalia, nikamwongoza sala ya toba, lakini baada ya hapo hakurudi kanisani… nilimwombea kwenye simu, akaniambia: ‘Baba ninataka kumrudia Mungu maana haya maisha ninayoishi siyo.’
“Akasema ‘Maisha haya ninayoishi yana mwisho haya, kwa hiyo nimeona nimrudie Mungu’,” amesema Mchungaji Luwongo anayesema anajisikia aibu mno kuona mtoto wa mchungaji anatuhumiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa mkewe, ila akaongeza: “Kwa kujificha hisia, yuko vizuri sana. Alikuja hapa akasema anaangua nazi ampelekee mtoto matumizi baada ya mama yake (Naomi) kuwa amepotea. Usingeweza kuona hisia za aina yoyote. Alikuwa kama mtu ambaye hajatenda lolote.”
Watetezi wa haki za binadamu
Watetezi wa haki za binadamu wanaofuatilia suala hili wametaka polisi kupanua wigo wa washitakiwa. Wamesema kwa uzito wa tukio la mauaji, sheria iko wazi: “Ni vigumu kuamini kuwa Hamis kama kweli ameua, kama alivyosema pale polisi, aliua peke yake. Sheria iko wazi, kuwa mauaji yakitokea wanakamatwa washirika kabla ya mauaji, washirika wakati wa mauaji na washirika baada ya mauaji.
“Taarifa za kina zilizochapishwa na Gazeti la JAMHURI ambalo tunalipongeza kwa kufanya uchuguzi wa kina katika suala hili, ziko bayana kuwa huyu Bwana Hamis alikuwa na watu wanaomsaidia katika mpango huu. Hawa wafuatiliwe, wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria kupima kiwango chao cha ushiriki.
“Maelezo kwamba kulikuwapo imani za ushirikina, nayo yachunguzwe na kufanyiwa kazi. Kama kuna waganga wa kienyeji walichangia mauaji haya nao wakamatwe na kushitakiwa. Ni kwa njia hii tutaepusha mauaji ya kinyama katika nchi hii,” amesema mtetezi wa haki za binadamu aliyeomba asitajwe jina kwa sasa.
Naomi alidaiwa kutoweka nyumbani kwake Mei 14, 2019 na baadaye akawa hapatikani kwenye simu zake. Hamis (mume wake) hakutoa taarifa ya upotevu wa mkewe sehemu yoyote hadi Mei 19, 2019 alipokwenda kuwasiliana na wakwe zake, hali iliyowatia wasiwasi.
Wasiwasi uliongezeka alipowasilisha meseji alizosema alitumiwa na Naomi akimuaga kuwa amekwenda nje ya nchi na wasingeonana tena, hali iliyowasukuma kufanya uchunguzi, baadaye wakabaini kuwa alitumia simu yake kujitumia meseji kwa kutumia ‘sim card’ ya Naomi.
Hamis alikamatwa Julai 16 na amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo kesi yake imetajwa na kuahirishwa hadi Agosti 13, 2019.