Vikongwe waauwa

Operesheni haramu ya mauaji ya kinyama dhidi ya wanawake vikongwe, inayofanywa na kikundi cha Chinja Chinja isipodhibitiwa mkoani wa Geita, kuna hatari ya hazina hiyo muhimu kwenye Taifa kumalizika kwa kuuawa bila hatia.
Awali operesheni hiyo ilijikita katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani Tabora na Shinyanga, ambako wananchi wake waliamini suala la ushirikina kama sehemu ya maendeleo kwa kiwango kikubwa kabla ya vyombo vya dola kuitokomeza.
Hofu ya kutoweka kwa wanawake vikongwe katika Mkoa wa Geita kwa kuuawa bila hatia, kwa mwamvuli wa operesheni haramu ya kusaka wachawi, kamata kikongwe, ua, imetokana na ukweli kuwa mauaji haya yamezidi kuutikisa mkoa na sasa imekuwa haipiti siku bila kusikia kikongwe kachinjwa.
Majanga haya ya mauaji yanayofanywa chini ya mwamvuli wa kusaka wachawi mkoani Geita, kwa sasa ndiyo ‘habari ya mjini’ ambapo katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja zaidi ya vikongwe saba wameuawa bila hatia.
Kibaya zaidi, mauaji haya yanafanyika kwa kufuatana-fuatana huku staili ya mauaji hayo ikifanana, hali ambayo inaonesha muuaji ni mmoja au kikundi cha watu fulani.
Matukio hayo ni pamoja na lile lililotokea katikati ya mji wa  Geita kwa kumuua kikongwe Lidya Mhola (60), mkazi wa Mtaa wa Misheni, mjini Geita, kwa kukatwa panga akiwa nyumbani kwake.
Tukio la mauaji hayo limetokea Jumamosi, Julai 5, mwaka huu saa 2 usiku baada ya wauaji hao kumvamia kikongwe huyo akiwa nyumbani muda mfupi akitokea dukani. Matukio mengine ni pamoja na la Chanila Masaga (50), mkazi wa Kijiji cha Rwezela, Tarafa ya Bugando, aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana Juni 30 mwaka huu majira ya usiku.
Mbali na tukio hilo, jingine ni la mwanamke kikongwe Mwanamayila Mwanatenga (50), mkazi wa Kijiji cha Nyamtundu, Kata ya Busanda, wilayani Geita, aliyeuawa na watu wanaodaiwa ni watoto wake wa kambo waliotajwa kwa majina ya Masumbuko Nzari (36) na Makoye Nzari (25), ambao nao baadaye waliuawa na wananchi mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.
Yulita Boniventure (45), mkazi wa Kijiji cha Nyanguku, Kata ya Nyanguku, tarafani Geita Mjini aliyeuawa kikatili kwa kuchinjwa koromeo na watu wasiojulikana Mei 24, mwaka huu  majira ya usiku baada ya watu hao kufika nyumbani kwake kisha kubisha hodi na kumuuwa akiwa nje ya nyumba yake muda mfupi baada ya kuwafungulia mlango.
Tukio hilo pia lilitokea ikiwa ni siku nne tangu Nyanzala Kitunguru (75) kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana majira ya saa 1:30 katika Kijiji cha Nyawilimilwa Kata ya Kagu, wilayani Geita.
Pia Aprili 23, mwaka huu saa 2 usiku katika Kijiji cha Katoma wilayani Geita, watu wasiojulikana walifika nyumbani kwa Kulwa Kapalata (67)kuomba maji ya kunywa kisha kumshambulia kwa kumkata kwa mapanga kikongwe huyo na kusababisha kifo chake.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Aprili 27, mwaka huu vikongwe watatu waliuawa kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kagu, Butundwe na Kasamwa wilayani hapa kwa kushambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana. Waliouawa kwenye matukio hayo ni  Joyce Dotto (70), mkazi wa Butundwe ambaye aliuawa akiwa eneo la Shule ya Msingi Chikobe akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.
Mwingine ni Yombo Petro (50), mkazi wa Kasamwa, akiwa nyumbani kwake alivamiwa saa 1 usiku na watu watatu waliomshambulia kwa mapanga sehemu za shingoni na mikono na kusababisha kifo chake kisha wauaji wakachukua ng’ombe wawili na kuondoka nao. Kabula Yohana (60), mkazi wa Kitongoji cha Nchankungu, Kijiji cha Kagu, ambaye aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na kundi la watu wasiojulikana idadi yao. Mara baada ya kufanya mauaji hayo waliotoweka kusiko julikana.

DC  Geita awaasa wananchi

Akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Bugulula hivi karibuni kwenye mkutano wa kijiji hicho, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie, aliyefika kijijini hapo kusikiliza kero za wananchi, aliwataka wananchi kuwafichua wageni wanaoingia kijijini hapo kinyemela, hali ambayo inaweza kusaidia upatikanaji wa wahalifu kwa uharaka zaidi.

Wananchi watoa ya moyoni

Baadhi ya wakazi wa Geita ambao wameguswa na wimbi hilo la mauaji vikongwe linaloendelea hususani katika Wilaya ya Geita, wakizungumza na JAMHURI walikwenda mbali zaidi kwa kulalamikia mabadiliko ndani ya Jeshi la Polisi yaliyofanywa hivi karibuni na Mkuu wa Jeshi hilo Tanzania (IGP), Ernest Mangu, kwa kumhamisha aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai mkoani Geita (RCO), Simon Pasua.
Walidai kutokuwa na imani na uhamisho huo wa RCO Pasua kwa kile walichodai kwa kiasi kikubwa baada ya kuhamishwa Geita matukio ya uhalifu yameongezeka.
Katika Mtaa wa Nyankumbu, Kaliwa Maningu pamoja na mfanyabiashara wa duka la nguo, Mathias Matono, kwa nyakati tofauti wamesema taarifa za uhamisho huo ziliwashtua kwani katika kipindi cha miezi minne alichowatumikia, RCO Pasua kabla ya kuhamishwa matukio hayo yalipungua tofauti na alipoondoka matukio hayo yanaongezeka kila kukicha.
Wamesema kuwa ulinzi shirikishi jamii ulikuwa umeimarika zaidi kutokana na taarifa zilizokuwa zikitolewa na wananchi kwa kiongozi huyo na zilifanyiwa kazi kwa wakati, hatua ambayo ilisaidia kupungua kwa matukio ya uhalifu.
Walitolea mfano wakati RCO Pasua hajahamishiwa Geita, kulikuwa na wimbi la uvamizi wa maduka ya M-Pesa kwenye maeneo mbalimbali Geita ikiwamo katika Kijiji cha Nyankumbu, Kata ya Kalangalala, mitaa ya Safari na Msalala, matukio ambayo yalifuatana-fuatana na kuwafanya waishi kama wakimbizi kwenye nchi yao, lakini RCO Pasua alipoletwa Geita alivunja mtandao huo wa uhalifu.
“Ninyi waandishi wa habari ni mashahidi, kwa muda mrefu matukio ya ujambazi hususani kwetu sisi wafanyabiashara wa maduka ya M-Pesa ilikuwa karibu kila siku tunavamiwa, lakini RCO Pasua alipoletwa hapa hakuna tena ujambazi na hii yote ni kwa kuwa amekuwa si mtu wa kukaa ofisini,” amesema Boniphace Kazaula, mfanyabiashara Mtaa wa Safari na kuongeza:
“Pasua ni mtu anayeijua vema dhana ya polisi jamii maana yuko karibu na sisi wananchi, tofauti na viongozi wengine wa jeshi hilo ambao mara nyingi wamekuwa ni miungu-watu na ndiyo maana tulimpa ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa za uhalifu na alizifanyia kazi, sasa tunajiuliza IGP Mangu aliyajua haya au ametumia vigezo gani kutuondolea kiongozi wetu?” Alihoji Kazaula.
Kuhusu mauaji ya vikongwe, wananchi hao walidai kama yalikuwapo si kwa kiasi kikubwa kama ambavyo kwa sasa yametawala kila sehemu za Geita. Hivyo wamemwomba IGP Mangu kuangalia upya suala hilo hasa ikizingatiwa kuwa, RCO Pasua amewatumikia wananchi wa Geita kwa muda mfupi lakini kwa weledi unaotakiwa, na kwamba iwapo atarudishwa mkoani hapa wakashirikiana na Kamanda wa Polisi aliyepo, Joseph Konyo, ambaye naye amekuwa mpelelezi wa siku nyingi kama ilivyo kwa RCO Pasua, wanaamini matukio haya yatatoweka.
Katika mabadiliko hayo, Pasua alihamishiwa Mjini Magharibi Zanzibar huku aliyekuwa Kamanda wa Polisi Geita, Paulo akipelekwa Morogoro na nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoani Mwanza, Joseph Konyo.

Kikongwe anena

Mmoja wa kikongwe (62), Mkazi wa Kijiji cha Bugulula wilayani Geita, aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa usalama wake, akizungumzia mauaji dhidi yao aliitaka jamii kuwaona na wao kama binadamu wenzao na si kuwawinda kama wanyama na kuwaua kana kwamba wanao ushahidi kwamba wao ni wachawi.
“Tunashangaa tunauawa eti tukihisiwa wachawi…hatupewi hata haki ya kusikilizwa kabla hawajatuhukumu… na wanaotuua ni watoto wetu wa kuzaa, hivi sisi tumewakosea nini? Hawajui kama nasi ni binadamu kama wao? Jamani tunaomba Serikali itulinde, ichukuwe hatua za haraka tutakwisha mwanangu,” amesema.
Hata hivyo, alishangaa kuona kundi linaloandamwa zaidi ni lile la wanawake tu katika jamii, kana kwamba wanaojihusisha na uchawi ni wao na si wanaume wazee.
“Wanatupa adhabu kubwa sana sisi wanawake utadhani hakuna wanaume wachawi, hawa watoto wetu wangeacha ujinga huu kwani wanadanganywa na wakishatuua wanabaki kupata laana…watuache jamani Serikali itusaidie,’’ amesema kwa uchungu kikongwe huyo.

Takwimu za mauaji

Takwimu zinaonesha katika kipindi cha mwaka 2013 vikongwe 15 waliuawa kikatili mkoani Geita kwa imani za kishirikina na migogoro ya urithi wa mashamba na mifugo katika wilaya za Geita, Chato na Bukombe, idadi ambayo kwa sasa inaonesha hali imetisha kutokana na ukweli kuwa waliouawa hadi sasa ni zaidi ya takwimu hizo.

Matukio ya mauaji

Tukiachilia mbali takwimu hizo za mwaka jana, mwaka 2012 mauaji ya vikongwe yaliutikisa Mkoa wa Geita likiwamo tukio la wanawake wanne — watatu wakiwa vikongwe — kuuawa kinyama wakituhumiwa wachawi. Wanawake hao ni Ester Konya (55), Lolencia Bangili (70), Kulwa Mashana (65) na Rosa Masebu (65).
Chanzo cha wananchi hao kuwaua ni tukio la mtoto Diana Salu (5) kuliwa na fisi katika Kijiji cha Kakubilo, hali ambayo ilileta mtafaruku kwenye kijiji hicho kwa wananchi kuanza msako wa nyumba kwa nyumba wanazoishi vikongwe hao, wakiwatuhumu kumfuga fisi aliyemla mtoto huyo pasipo na uthibitisho wowote.
Mbali na wanawake hao kuuawa mkoani Geita, mwingine ni Maua Ikoti (60), mkazi wa Kasang’hwa, wilayani Geita aliyeuawa kinyama kwa kukatwa mapanga nyumbani kwake saa 6 usiku.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasang’hwa,  Maganiko Ndiomali, alisema wauaji hao walimkata kwa panga kikongwe huyo sehemu za kichwani, mikono, shavuni na kwenye matiti na kumuua na kwamba pamoja na mayowe yaliyopigwa na watoto wa marehemu ya kuomba msaada, juhudi za wananchi kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili kuwatia nguvuni hazikuzaa matunda.
Kikundi hicho cha Chinja Chinja ambacho kwa sasa kinawanyima vikongwe usingizi mkoani Geita, ndicho pia kinachodaiwa kuhusika na mauaji ya kikatili dhidi ya mwanamke Mondesta Nchambi (53), mkazi wa Kitongoji cha Isabilo, Kijiji cha Nyakarango, wilayani Chato, mkoani Geita, kwa kumchinja shingo kwa kutumia kitu chenye ncha kali kisha kutenganisha kichwa na kiwiliwili chake Septemba 26, 2012. Mauaji hayo yalifanyika katika kipindi kisichozidi wiki nne.
Pia Juni 17, 2013 Jacob Simbakira (52), mkazi wa Kijiji cha Mwekako, wilayani Chato, Geita aliuawa na watu wasiojulikana kwa kuchinjwa shingo na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili chake.
Kana kwamba mauaji hayo yamehalalishwa, Septemba 14, 2013 kikundi hicho cha Chinja Chinja kilimuua Ester Mashenene (61), mkazi wa Kitongoji cha Bugayambelele, Kijiji cha Katoro, Geita.
Haya ni baadhi tu ya matukio yaliyoripotiwa kwenye vyombo vya dola na yapo mengine ambayo yamekuwa yakifichwa na baadhi ya viongozi wa maeneo husika wasiowaaminifu, kutokana na kinachodaiwa kuzibwa mdomo na watuhumiwa wa mauji hayo.

Chanzo cha ukatili huo

Kutokana na mauaji hayo ya kikatili yanayoendelea kufanyika mkoani Geita, JAMHURI ambao wanalaani vikali ukatili huo, wameamua kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kushamiri kwa matukio hayo kwa kuongea na wadau mbalimbali.
Uchunguzi umebaini kuwa ni urithi wa ardhi yakiwamo mashamba makubwa na mifugo, imani potofu, wananchi kuwa na imani za kishirikina, umaskini, wananchi kutokuwa na elimu ya kuzifahamu haki za kuishi za binadamu na waganga wa jadi matapeli ndiyo kiini cha ongezeko la mauaji haya ya wanawake vikongwe Geita.
Hivyo, kutokana na sababu za kiuchumi na umaskini wa wananchi, watu wanaokodiwa na kujipitia pesa hiyo haramu, huamua kutekeleza kazi za mauaji ya kulipiza kisasi kwa kuwaua vikongwe. Hii hutokea kwenye familia ambazo zimefiwa na ndugu zao zenye imani kwamba vifo vya jamaa zao hao vilitokana na kulogwa.
Mauaji hayo hufanyika baada ya ndugu waliofiwa na jamaa zao kwenda kwa waganga wa jadi matapeli na kuoshwa dawa za uongo na kuelezwa uongo kwamba vifo hivyo si mkono wa Mungu, bali vilitokana na kulogwa na mara nyingine waganga hao hubashiri mtu aliyehusika na kifo hicho na balaa huanzia hapo.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa mbali na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kifungu cha 14 na 16 kutamka wazi kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kuheshimiwa utu wake, elimu hiyo haijasambaa kwenye maeneo mengi ya Geita — kuanzia vijijini hadi mijini — huku wengine kudai hawajui Katiba ya sasa inafananaje!
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakifanya mambo yao ndivyo sivyo pasipo kujua kwamba kuwaua vikongwe si suluhisho la kutokuwapo vifo, matatizo ya kiafya na kiuchumi katika familia zao.
Hata hivyo, imebainika kuwa vikongwe wanaolengwa kuuawa ni wale ambao waume zao walishafariki dunia, na kwa mila walizonazo baadhi ya makabila wao ndiyo warithi wa mali hizo, hali ambayo baadhi yao hujifanya ‘hamnazo’ na kusahau kuwa wana watoto wakubwa wa kiume tena wameoa, ambao nao huzitolea macho mali zile zile ambazo tayari vikongwe hawa walikwishachagua mjukuu mmoja kati yao aliye karibu yake, ndiyo wanaanza kuwarithisha mali, hali ambayo inaleta chuki kati ya kikongwe, watoto na wajukuu.
Imeelezwa kuwa kutokana na chuki ya nani arithi mali hizo, ndipo wale watoto wanaanza kutengeneza mipango ya kumuua bibi yao, ambapo kuna watu maalum wanaolipwa pesa kwa ajili ya kutekeleza mauaji kwa kutumia mapanga. Sasa wamebuni mbinu nyingine ya kutumia aina fulani na vishoka vidogo wanawapiga vikongwe sehemu za uti wa mgongo ili wafe bila kupiga kelele.
JAMHURI imebaini pia kuwa wahusika wakuu wa mauaji ya vikongwe ni watoto, ambao huwalipa ujira wauaji kutokana na hofu ya kuua na baada ya kitendo hicho hukimbilia kwa waganga wa jadi kwenda kuoshwa dawa ili kuondoa laana ya kuua wazazi wao.

Nini kifanyike

Mchungaji wa Kanisa la Heri Wenye Moyo Safi la Mjini Geita, Mathayo Yaya, ameomba viongozi wa madhehebu yote ya dini kuelekeza nguvu zao kuwahubiria watu ukweli wa Biblia kuhusu kuwaheshimu wazee pamoja na kuwafundisha vijana umuhimu wa kuwapo wazee katika jamii.
Huku akinukuu baadhi ya maandiko yaliyo kwenye Biblia Takatifu, Mchungaji Yaya, anasema “Kuua vikongwe ni dhambi mbele za Mungu, ukisoma katika kitabu cha Kutoka 20:12 inasema: ‘Waheshimu baba na mama’ hivyo ni jukumu letu viongozi wa dini kujikita katika kuwahubiria watu ukweli wa Biblia kuhusu kuwaheshimu wazee, pia tuwafundishe vijana umuhimu wa kuwapo kwa wazee katika jamii yetu, kwani bila hivyo wazee wetu ambao ni hazina muhimu itatoweka.
“Mimi hapa mwezi wa nane mwaka huu natimiza miaka 50 kwa lugha nyingine nitakuwa nimetimiza umri wa kuanza kuwindwa, unadhani bila mikakati madhubuti tutaendelea kuishi kwa hofu ilhali Bibilia imeweka wazi mambo yote ya kuyazingatia kama wanadamu’’.
Mchungaji Yaya aliishauri Serikali kuacha kutoa holela vibali vya uganga na badala yake vitolewe kwa waganga wa jadi ambao imejiridhisha nao kwamba wanatoa huduma halali, na wale wanaofanya kazi kinyume cha taratibu za uganga pasipo kuwa na vibali wasakwe na kukamatwa ili wafikishwe mahakamani mara moja maana ndiyo chanzo cha mauaji hayo.

Mganga wa jadi anena

Kwa upande wake, James William, Mganga wa Jadi maarufu wilayani Geita, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa waganga wa jadi, alidai kuwa si waganga wote ni matapeli kama inavyodaiwa bali wapo wachache wanaochafua utaalamu huo wa tiba za jadi.
“Ukisema kwamba sisi waganga ni matapeli na ndiyo tumekuwa chanzo cha mauaji ya vikongwe unakosea, ninachotaka kukueleza ni kuwa wapo matapeli waliojivika joho la uganga ndiyo wanaosababisha hata sisi tunaotoa tiba kisheria tuonekane matapeli, kwani mimi kama mtoa tiba za jadi lazima kwanza nitambue kwamba sisi binadamu tunazaliwa huru na sawa nikishalitambua hilo siwezi kumpa mtu maelekezo ambayo hatima yake ni kuondoa uhai wa mwenzangu,’’ amesema William.
Alivishauri vyombo vya sheria kutoa adhabu kali kwa waganga ambao watabainika wanaendesha shughuli za kuwatapeli watu na kwa wauaji wa vikongwe, maana mbali na kuondoa uhai wa mtu pia wanasababisha matatizo makubwa kwa familia husika baada ya kuondokewa na mtu aliyekuwa nguzo yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa azungumza

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, mbali na kuthibitisha kuwapo kwa matukio hayo, aliitaka jamii kutambua kuwa kuwaua wazee kwa hisia za uchawi ni unyama unaoleta machungu na chuki kwa familia ya aliyeuawa na kwa Taifa kwa ujumla.
Kamanda Konyo alifafanua kuwa hayo yote ni makosa ya jinai na kwamba atendaye makosa hayo akikamatwa anachukuliwa hatua kwa mjibu wa sheria. Ameitaka jamii kuachana na imani potofu za upigaji ramli kwani baaadhi ya waganga wa jadi ni waongo na wagombanishi.
Akizungumzia mkakati wa Jeshi la Polisi kukabiliana na matukio hayo, Konyo amesema kuwa wanatarajia kuanza msako wa kuwakamata waganga wote wa jadi wasio na vibali kisha kuwafikisha mahakamani. Amesema kuwa hilo litasaidia kupunguza mauaji hayo ambayo yanaacha kilio, chuki na simanzi isiyoelezeka kutoka kwa baadhi ya familia ambazo ndugu zao wameuawa.
“Mkoa wa Geita kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe. Hali hiyo inavuruga sifa ya mkoa wetu na si kwamba yanatokana na uchawi peke yake au imani za kishirikina, bali mauaji haya pia yanatokana na wanafamilia kugombania mali za urithi katika jamii.
“Hivyo, sisi kama Jeshi la Polisi tumejipanga kuanza kazi ya kukamata waganga wa jadi wasio na vibali na kuwafikisha mahakamani. Pia tunawaasa vijana kutumia ujana wao kuleta mabadiliko hasa katika suala hili la mauaji ya wazee wetu,” alieleza Konyo.