Watanzania tumejiandaa kupokea ugeni mkubwa kwa wakati mmoja, kuanzia wiki ya kwanza ya Agosti hadi ile wiki ya tatu. Macho ya dunia yatakuwa Tanzania kufuatilia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Wakati wageni wanaanza kuingia nchini kwa ajili ya vikao vya awali vya wataalamu pamoja na kikao cha makatibu wakuu, kabla ya kile cha wakuu wa nchi na serikali, tumeona viongozi kadhaa wakieleza kuhusu utayari wa nchi kuwakaribisha wageni wenye hadhi hiyo kwa mpigo katika kipindi cha zaidi ya miaka 16.
Wengi wa waasisi wa mataifa yanayounda SADC wanayo kumbukumbu nzuri ya Tanzania, kama hawakupigania uhuru wakitokea hapa nchini, basi walipewa mafunzo ya namna ya kupambana na wakoloni katika nchi zao na hatimaye kujipatia uhuru.
Tanzania tunakwenda kuchukua uenyekiti wa SADC, hiyo ikiwa na maana kwamba Rais Dk. John Magufuli anakwenda kuchukua nafasi ya uenyekiti wa taasisi hiyo yenye nguvu kusini mwa Bara la Afrika. Mbali na ajenda ya uenyekiti wa SADC, tukipeleke Kiswahili kwenye nchi hizo 15 zaidi.
Nchi wanachama wa SADC ni Tanzania, Congo DRC, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Botswana, Lesotho, Eswatini, Namibia, Angola, Msumbiji, Madagascar, Mauritius na Seychelles. Mchangayiko huo wa nchi 16, unazo lugha mchanganyiko pia.
Nchi zote hizo zinazungumza lugha za wakoloni wake, zipo zinazozungumza Kiingereza, Kifaransa huku nyingine zikizungumza Kireno. Tanzania tunayo nafasi ya kukinadi Kiswahili chetu, maana si lugha ya kikoloni, lakini pia ni moja ya lugha zinazokua kwa kasi sana duniani.
Baadhi ya nchi ndani ya SADC zimeanza kuonyesha nia ya kuanzisha somo la Kiswahili katika mitaala ya shule zao, moja ya nchi hizo ni Afrika Kusini. Kwa hakika kama SADC ikiridhia Kiswahili kikaanza kutumika kama lugha rasmi ya kanda, wananchi zaidi ya milioni 240 watakwenda kunufaika.
Yapo manufaa ya kuzungumza Kiswahili, moja ya manufaa hayo yakiwa ni wananchi wote kusikilizana kwa kuzungumza lugha moja, jambo jingine ni biashara miongoni mwa wananchi wenyewe.
Rais Magufuli amekuwa kielelezo kikubwa cha kupambana na mambo kadhaa, jambo la kukipeleka Kiswahili katika nchi za SADC na kukifanya lugha rasmi, litakuwa moja ya mambo makubwa ambayo yatakuwa yamefanywa na Tanzania, hivyo kutimiza ndoto ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.