Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi ni mahabusu ambaye nimo gerezani kwa amri ya mahakama nikituhumiwa kesi ya kubambikiwa ya mauaji. Nimo gerezani tangu Mei 08, 2016 mpaka hivi sasa unavyosoma barua hii.
Mheshimiwa Rais, sababu ya kupewa kesi hii ni kutokana na askari polisi wa Kituo cha Usa-River [jina limehifadhiwa] ambaye kwa sasa ameamua kuishi na mke wangu. Nimebambikiwa kesi kwa jambo ambalo sijawahi kuliwaza wala kulitenda.
Mheshimiwa Rais, maneno haya ninayoyaeleza ni ya kweli, kwani askari huyu alikwishawahi kuja RCO wa Mkoa wa Arusha wa wakati huo, George Katabazi, kwenye moja ya vikao vyake hapa gerezani Januari 29, 2018 akiwa ameambatana na Mwanasheria Mkuu – Kanda ya Kaskazini, Mheshimiwa Marandu. Niliwaeleza kuhusu unyama niliofanyiwa, lakini malalamiko yangu hayakufanyiwa kazi, hivyo bado ninaendelea kuteseka gerezani bila hatia yoyote na hili linanifanya nione nchi na jamii wamenitupa.
Mheshimiwa Rais, Oktoba 22, 2018 alikuja Jaji Mfawidhi Kanda ya Kaskazini, Mheshimiwa Jaji Moses Mzuna, naye nikamweleza kuhusu kesi yangu na namna nilivyopewa haya mauaji ambayo sikutenda.
Kesi yangu ya msingi ilikuwa ni kukamatwa na mali inayosadikiwa kuwa ni ya wizi yenye CC. No. 13/2015 na kesi hii ilikwisha kutolewa uamuzi Machi 16, 2016 mbele ya Mheshimiwa Mwita katika Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai, Wilaya ya Arumeru, lakini cha kushangaza nilipoachiwa tu mahakamani hapo hapo nilikamatwa tena na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Usa-River.
Niliendelea kushikiliwa kituoni na ilipofika Mei 18, 2016 nikapelekwa mahakamani na kusomewa shitaka la mauaji mbele ya Hakimu Devotha Msofe katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru. Mheshimiwa Rais, mauaji hayo siyafahamu. Mahakamani ninatakiwa nisijibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Tarehe hiyo hiyo ndipo nikapelekwa Gereza Kuu la Arusha na ilipofika Mei 23, 2016 nikarudishwa tena mahakamani hapo na kuunganishwa na mshitakiwa mwingine aitwaye Juma Shabani. Nilipomuuliza mshitakiwa huyo akanieleza kuwa naye alikuwa na kesi ya kumwibia Mzungu mmoja, lakini wakampa kesi ya mauaji yenye P.I No. 27/2015. Shabani amekuwa gerezani kwa mwaka mmoja kabla ya mimi kuunganishwa naye kwenye kesi ambayo hata siijui.
Mheshimiwa Rais, Februari 05, 2019 katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria alikuja Jaji Mwinyi Panzi akiwa ameambatana na Mwanasheria wa Serikali wa Kanda, Mheshimiwa Marandu pamoja na viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha na wengine wengi.
Nikamweleza Jaji Panzi kama nilivyopata kumweleza Jaji Mzuna. Ilipofika Februari 7, mwaka huu Mwanasheria wa Kanda, Mheshimiwa Marandu alitoa maelekezo kuwa niandike barua ya malalamiko, na kwa kweli nilifanya hivyo. Nakala ninazo. Lakini Februari 13, 2019 RCO aliwatuma askari wake kuja gerezani kunihoji. Nikawapa maelezo yote tukiwa katika Ofisi ya Usalama hapa gerezani.
Mheshimiwa Rais, baada ya maelezo yangu hayo, askari walibaini ukweli wa mambo kwa namna nilivyobambikiwa kesi na namna askari aliyeshiriki kunifanyia maovu haya alivyoamua kuishi na mke wangu. Askari huyo naambiwa amehamishwa kutoka Usa-River na inadaiwa kuwa amepelekwa Loliondo, Ngorongoro.
Mheshimiwa Rais, kulingana na mamlaka uliyonayo na kwa kuwa wewe ni mtetezi wa wanyonge kama mimi, ninakuomba rais wangu mpendwa unisaidie nitoke gerezani. Kuwemo kwangu humu ndani ni mateso na kumevuruga kabisa maisha ya familia yangu.
Naamini unafahamu mambo haya yanayoendelea katika ngazi za chini, hasa kwenye mahakama, naomba unisaidie nitoke, kwani ninaona kesi hii nimebambikiwa kutokana na maelekezo ya baadhi ya watu wenye mamlaka fulani. Naomba ufuatilie suala langu na naamini utabaini kuwa nimekueleza ukweli, tena ukweli kabisa.
Asante sana. Nakutakia kazi njema za ujenzi wa taifa letu na Mungu akubariki sana.
Wako mtiifu,
Mah. No. 1832/2015 – Elibariki Sylvester,
Gereza Kuu Arusha.