Mgogoro wa ardhi uliodumu miaka mitatu sasa baina ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mahiga na familia ya Dionis Mashiba, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, unaonekana kupuuzwa na mamlaka wilayani hapa.
Mtanziko huo ulioanza mwaka 2016, unatokana na kile kinachodaiwa kuwa familia ya Mashiba kuingia kwenye eneo la Mwalimu Majenga huku Idara ya Ardhi ikishutumiwa kushindwa kuutatua.
Kutokana na hali hiyo, mgogoro huo uliopo Mtaa wa Ngumo ‘A’, Kata ya Ngudu unaoelezwa kukua siku hadi siku unadaiwa huenda ukasababisha uvunjifu wa amani iwapo hautapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Licha ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ya Kwimba, Mtemi Msafiri, aliyehamishiwa na Rais John Magufuli wilayani Chato, Geita kuwahi kuushughulikia, lakini baada ya kuondoka uliibuka upya.
Mwalimu Majenga amesema kuwa jirani yake huyo amekuwa akibadili mipaka na kuingia ndani ya eneo lake kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Amesema kuwa, kwa sasa familia hiyo ya Mashiba imeanzisha ujenzi wa msingi wa nyumba kuziba eneo jingine analodai kuwa ni njia, huku upande wa eneo lake (mwalimu) pia likiingiliwa bila idhini yake.
Majenga amesema mwaka 2008 alilipa Sh 100,000 Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ili apimiwe eneo lake ingawa hakupewa stakabadhi kwa kile alichoeleza kuwa aliambiwa kitabu cha stakabadhi kimekwisha.
Anadai kuwa ingawa malalamiko yake ya kuingiliwa kwenye ardhi kwa muda mrefu alikwisha kuyafikisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pendo Malebeja, lakini bado hayajapatiwa ufumbuzi.
“Nanyanyaswa! Nanyanyasika pengine ni kwa sababu mimi ni mwanamke.
Amesema Oktoba 9, 2018 alimwandikia barua mkurugenzi wa halmashauri hiyo akiomba ulinzi wa mali yake na kutodhulumiwa haki yake ya kumiliki ardhi.
Katika barua hiyo aliyoituma kwa mkurugenzi wa halmashauri, Majenga ameandika: “Aprili 2008 nilinunua eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Niliwashirikisha serikali ya mtaa katika ununuzi huo. Na baadaye Ofisi ya Ardhi kabla ya kuanza kujenga. Nao bila ajizi walifika katika kiwanja/eneo nililonunua kwa Shija Lupoja na watumishi kutoka ofisi ya ardhi waliweka mipaka na kunielekeza namna ya ujengaji.
“Na kwa mara ya pili nililipa Sh 50,000. Mwaka 2011 nilikamilisha ujenzi na kuhamia katika nyumba yangu. Mwaka 2016 nilianza kuendeleza sehemu ya eneo langu la nyuma ndani ya mipaka ya umiliki wangu na mipaka niliyowekewa na ardhi kwa kuweka msingi wa nyumba nyingine, jambo lililozua mgogoro.
“Uongozi mpya wa mtaa ulitaka kubomoa msingi. Mgogoro huu uliisukuma Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kwimba kufika eneo ninalomiliki. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wewe (mkurugenzi wa halmashauri) ukiwa mmoja wao. Baada ya utafiti na maelezo yangu na uongozi wa mtaa yalibainika:- Nilikuwa nimejenga kihalali katika eneo langu, uovu na hila za wasiopenda maendeleo ya wengine, chuki binafsi zimetawala, hakukuwa na njia kama ilivyodaiwa na walalamikaji baada ya uwekaji wa mipaka, bali uchochoro.
Kwa mujibu wa barua hiyo ya Majenga aliyoituma kwa Mkurugenzi Malebeja, aliyoitoa nakala ofisi ya ardhi, Takukuru na idara nyingine nyeti, imeagiza mambo matatu ili kumaliza mgogoro huo.
“Mti upande wa kaskazini (kwa Ng’wana Malemve) ukatwe ili kuacha njia, jambo ambalo Mwenyekiti wa Mtaa aliachiwa atekeleze. Hadi sasa miaka miwili imepita maagizo hayakutekelezwa.
Majenga amewataja wenzake anaodai waliwekewa mipaka ya maeneo yao kwa mujibu wa mpango mji, baada ya kulipa gharama ya upimiwaji kuwa ni; Mwalimu Charles Said, Albert Constantine, Ng’ana Malemve, mzee Kato, mzee Bala naye mwenyewe, kwamba waliahidiwa kupewa kiwanja na ofisi ya ardhi ya halmashauri, hadi sasa hawajapewa.
Amesema katika kutafuta haki yake hiyo, suala hilo alikwisha kulifikisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Simon.
“Baada ya kuona ninazidi kunyanyasika, nilipeleka malalamiko yangu kwa mkuu wa wilaya. DC akaniambia nisubiri Mwenge upite ndipo ashughulikie, lakini hadi sasa kimya.
Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo ya Dionis, Jonas Dionis, kijana wa familia hiyo amekiri kuwapo kwa mzozo huo wa ardhi baina yao na Mwalimu Majenga.
Amesema suala hilo lilikwisha kufikishwa serikalini, hivyo wanasubiri uamuzi wa mamlaka husika kwani na wao wanamlalamikia mwalimu huyo.
“Sisi ndio tulitakiwa tuyalete kwako, siyo yeye aje kwako kutoa haya malalamiko. Amefanya kinyume chake, sisi ndio tulipaswa tukuletee malalamiko hayo, umeona eeh!
“Yaani hilo ndilo jibu, maana sisi hilo eneo tumelimiliki kuanzia mwaka 1994, umeona. Neema amekuja hivi karibuni miaka isiyozidi hata 10. Sisi si wavamizi, sisi tumekutwa.
“Kama sisi tuliokutwa na kuvamiwa tunaulizwa na tutashtakiwa, sawa.
Yeye ametukuta na ametuvamia. Haya mambo yapo serikalini. Kama sisi tutakuwa tumemwingilia basi, kama yeye ametuingilia; mamlaka, sheria na taratibu si zipo?” amesema Jonas Dionis.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngumo ‘A’, Daniel Lusangija, alipoulizwa kuhusu mgogoro huo akahoji: “Neema Majenga ndiye anayelalamika au Dionis?”
Alipojibiwa Neema Majenga ndiye anayelalamika kuingiliwa eneo lake, aliomba atafutwe baada ya dakika 10. Hata hivyo, baadaye alipotafutwa simu ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Kiongozi mmoja wa kimila wa eneo hilo (Nsumbantale), Willy Masalu, amesema mzozo huo wa ardhi unachochewa na familia ya Dionis kuingia ndani ya eneo la Mwalimu Majenga.
“Anaonewa sana Mwalimu Neema. Imekuwa kama yupo Rwanda wakati hii ni nchi ya amani. DC aliyeondoka (Mtemi Msafiri) aliushughulikia mgogoro huo kwa karibu sana na angelikuwapo hili tatizo lingekwisha.
“Wakambandika kuwa ni hawara yake. DC aliyepo sasa na yeye amelishughulikia lakini kwa sasa sijui wamefikia wapi na Neema,” amesema Nsumbantale Masalu.
Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Wickriph Benda, alipoomba kuzungumzia mgogoro huo alikataa akiomba aulizwe mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Pendo Malebeja, alipoulizwa amekiri kuyafahamu malalamiko hayo ya Mwalimu Majenga, akisema anaamini suala hilo litamalizika muda si mrefu.
“Hayo maeneo hayajapimwa, hivyo tunatarajia kuanza upimaji shirikishi maeneo yale. Naamini litakwisha, labda lije upya.
“Hilo eneo nilishafika pale. Napajua,” amesema Mkurugenzi Malebeja, kauli iliyopingwa na ofisa mmoja mwandamizi wa wilaya hiyo, aliyedai zoezi la upimaji viwanja eneo hilo la Ngumo halipo kwa sasa.
Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kwimba, Maijo Faustine, kwa upande wake anamtuhumu Mwalimu Majenga, akidai ndiye anayechochea mgogoro huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Simon, anakiri kuufahamu mgogoro huo na amemshauri Mwalimu Majenga kuhama eneo hilo na kwenda kujenga kwingine.
DC Senyi amesema ushauri mwingine anaoona unafaa katika utatuzi wa mtanziko huo ni kusubiri upimaji shirikishi utakapofanyika ili kubainisha mipaka halali ya eneo hilo.
“Au Neema Majenga anaweza kununua maeneo yote yanayomzunguka hapo ili kumaliza mgogoro huu,” amesema mkuu huyo wa Wilaya ya Kwimba.
Alipoulizwa ni kwa nini mzozo huo usitatuliwe haraka, badala ya kumshauri mlalamikaji kuhama eneo hilo au kusubiri upimaji wa ardhi utakapofanyika, DC Senyi akasema: “Busara inahitajika zaidi.”