Mwezi ujao Tanzania itakuwa mwenyeji wa kikao cha kilele cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (The Southern African Development Community – SADC) jijini Dar es Salaam. Ni kikao cha 39 kinachofanyika kila mwaka.
Historia ya SADC ni sehemu ya historia ya harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, historia iliyoanza na jitihada za pamoja za nchi huru za Kiafrika kwenye miaka ya sitini na sabini kushirikiana na vyama vya ukombozi kukabiliana na tawala za kibaguzi za Afrika Kusini, Rhodesia na za makoloni ya Ureno.
SADC kama chombo rasmi inatokana na Nchi za Mstari wa Mbele zilizounda ushirikiano usio rasmi kuunganisha nguvu kukabiliana na hujuma za Afrika Kusini na Ureno ili kushinikiza uhuru kwa wananchi wa maeneo hayo yaliyoshikiliwa kwa mabavu na kwa uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa na mataifa ya Magharibi.
Mwaka 1975 nchi za Mstari wa Mbele (Tanzania, Zambia na Botswana) zilitambuliwa rasmi kama kamati ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (Organization of African Unity – OAU). Angola, Msumbiji na Zimbabwe zilipopata uhuru nazo zikajiunga na Nchi za Mstari wa Mbele kusaidia vita ya ukombozi.
SADC tunayoifahamu sasa hivi imepitia mabadiliko kadhaa, ila historia inatujulisha kuwa iliundwa kukabiliana na njama za hujuma za utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini dhidi ya Nchi za Mstari wa Mbele zilizoratibu maamuzi ya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kidiplomasia dhidi ya Afrika Kusini na Ureno.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa mwenyekiti wa kwanza na pekee wa Nchi za Mstari wa Mbele, na alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa SADC. Hiyo pekee ingekuwa chachu kwa Watanzania kudadisi nini hasa umuhimu wa SADC na zipi zinaweza kuwa sababu za kuendeleza ushirikiano huu.
Leo hii SADC imepanuka na kuongeza nchi wanachama kumi: Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Namibia, Seychelles na Afrika Kusini – ikiwa na idadi ya watu milioni 277 na jumla ya pato la nchi wanachama la Dola za Marekani bilioni 575.5.
SADC ya leo imejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa madhumuni ya kuleta maendeleo miongoni mwa raia wa nchi wanachama.
Lakini ushirikiano huu unatambua kuwa maendeleo hayapatikani kwa kukuza uchumi pekee. Yanapaswa kuambatana na vipengele vingine muhimu vilivyosimama juu ya msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Hivi ni pamoja na kulinda na kudumisha amani na usalama, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watu wa ukanda huo.
SADC inasisitiza umuhimu wa kuwepo tunu za pamoja kusimamia shughuli za siasa, mifumo na taasisi zilizopo. Aidha, ipo miradi ya pamoja kwenye sekta mbalimbali kama nishati, miundombinu na mazingira.
Kama nchi waasisi za Mstari wa Mbele zilifanikiwa kusimamia vema majukumu kama kamati ya OAU na kuchangia juhudi za pamoja zilizoangusha tawala za kibaguzi na ukoloni wa Wareno, kuundwa na kuwepo kwa SADC kumeendeleza kazi muhimu ya kugeuza uhuru wa bendera kuwa uhuru madhubuti wa kisiasa na kiuchumi.
Vita ya ukombozi haikumaliza azima ya nchi zilizonufaika na ukoloni kuendeleza udhibiti wao wa watu na rasilimali za Bara la Afrika. Hujuma hizo ziliendelea na zinaendelea mpaka sasa.
Jitihada hizi za kujenga ushirikiano wa kikanda chini ya SADC na jumuiya za kiuchumi za kikanda za aina yake barani Afrika ni mlolongo wa mikakati inayokusudia kuimarisha Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, yenyewe ikiwa ni mkakati katika ngazi ya bara – ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Waafrika katika miaka 50 ijayo.
Kama Agenda 2063 ni nyumba, basi msingi wake unajengwa na ushirikiano wa kikanda uliopo katika maeneo ya Bara la Afrika; ndani ya SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki na jumuiya nyingine za aina hiyo.
Jitihada zote za kujenga ushirikiano na umoja zinaambatana na matatizo mengi. Mojawapo ni uwepo wa nchi kama Tanzania ambayo ni mwanachama wa jumuiya za aina hiyo mbili: SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hili, pamoja na changamoto nyingine ambazo zinachelewesha au kukwamisha utekelezaji wa mikakati ya pamoja, si tatizo, ili mradi zipo jitihada za kuzikabili na kuzitafutia suluhisho.
Jambo la msingi ni kuwepo nia thabiti ya kuimarisha ushirikiano, jambo ambalo hakuna shaka ipo Tanzania.
Kwenye kikao cha mwezi ujao Rais John Magufuli atapokea uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais Hage Geingob wa Namibia, nafasi itakayodumu kwa mwaka mzima. Mara ya mwisho Tanzania kushika nafasi hiyo ilikuwa mwaka 2003 chini ya Rais Benjamin Mkapa.
Kwa historia ya nchi za Mstari wa Mbele na ya SADC, tunaweza kusema kwa unyenyekevu kuwa heshima ile ya uasisi imerudi tena nyumbani, kama ambavyo tutasema hivyo hivyo iwapo uenyekiti utahamia Zambia au Botswana.
Huu ni wajibu mkubwa kwa Watanzania kukumbushana chimbuko la ushirikiano huu, kuulinda na inapowezekana kushiriki kikamilifu katika kuuimarisha na kuuendeleza.
Barua pepe: [email protected]