*Hutumia makaburi kumwomba Mungu
Wiki iliyopita JAMHURI ilifanya mahojiano maalum na kijana msomi aliyehitimu elimu ya chuo kikuu katika fani ya utawala wa biashara. Huyu si mwingine yeyote bali ni Gerald Nyaissa, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Mahojiano haya yalijikita zaidi katika suala zima la kuchangamkia fursa za kujiajiri na kujijenga kiuchumi, badala ya kusubiri kuajiriwa serikalini na kupata misaada kutoka kwa wahisani. Yafuatayo ndiyo mahojiano yenyewe:
JAMHURI: Wewe ni mhitimu wa chuo kikuu, lakini badala ya kuhangaika kutafuta ajira serikalini kama wasomi wengi wanavyofanya, umekuwa ukijizatiti kuchangamkia fursa za kujiajiri na kuajiri. Je, ni nini kinachokusukuma kufanya hivyo?
NYAISSA: Kwanza kabisa nakushukuru ndugu mwandishi kwa kufanya mahojiano haya na mimi. Ni kweli sijihusishi na wala sina shauku kabisa ya kuzunguka serikalini na katika makampuni binafsi kutafuta ajira licha ya kiwango kizuri cha ufaulu nilichonacho.
Msukumo mkubwa wa mimi kufanya hivyo unatokana na ukweli kuwa tatizo la ukosefu wa ajira linaendelea kukua kwa kasi ya ajabu na mtu au watu pekee wanaotegemewa na jamii kutoa suluhisho la tatizo hilo (wasomi) nao wamekuwa sehemu ya tatizo!
Ni aibu kukutana na kijana aliyehitimu chuo kikuu lakini bado analia tatizo la ajira sawasawa na kijana aliyeishia kidato cha pili na kushindwa kuendelea na masomo, licha ya ujuzi mkubwa wa maisha aliojichotea msomi huyu kule chuoni!
Mimi nimechagua kuwa sehemu ya jawabu kwa kuamua kujiajiri na kuajiri vijana wenzangu.
JAMHURI: Taja ni kwa namna gani umejaribu kuibua na kuanzisha miradi ya kujiajiri na kujijenga kiuchumi?
NYAISSA: Hapa historia yake ni ndefu, lakini nitajitahidi kueleza kwa kifupi.
Mara tu baada ya kumaliza elimu yangu ya chuo kikuu mwaka 2012 niliungana na wasomi wenzangu wapatao 12 tuliokuwa na dhamira ya kuanzisha mradi wa ufugaji kuku kwa njia bora. Hata hivyo, mradi huo haukufanikiwa kutokana na wenzangu kukosa uvumilivu. Baada ya kujikuta tumebaki wawili, tulianzisha mradi mwingine wa kilimo cha vitunguu maji katika Kijiji cha Kiziko wilayani Mkuranga, mkoani Pwani ambao hata hivyo, nao haukufanikiwa. Mradi huo haukufanikiwa kwani baada ya kujinyima na kutumia gharama nyingi mpaka kufikia hatua ya kuhamishia vitunguu shambani kutoka kwenye vitalu, visima vifupi tulivyokuwa tukitegemea kwa ajili ya umwagiliaji vyote vilikauka na kujikuta tukipata hasara kwani shamba zima lenye ukubwa wa ekari zaidi ya tatu lilikauka!
Baada ya hapo yule mwenzangu alikata tamaa na kwenda kutafuta ajira, lakini nilijipa moyo na kuendelea kutafuta fursa nyingine. Niliamua kwenda Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuona kama kuna fursa zozote za vijana na hapo nikaunganishwa na kampuni ya Godtec Tanzania inayofanya kazi ya kuwawezesha vijana kujiajiri. Huko nilikutanishwa na vijana wenzangu na kufanikiwa kuanzisha kampuni ya watu 27, kisha kuteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo. Hata hivyo, kampuni hii nayo iliendelea kusuasua kwa muda mrefu kutokana na watendaji wake wengi kukimbia na kuamua kuajiriwa. Niliamua kujiondoa na kuanzisha kampuni nyingine ambayo naendelea nayo mpaka sasa, inayojumuisha vijana wenzangu wachache niliotoka nao kwenye kampuni iliyopita. Tuko kwenye hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kilimo cha kisasa cha mbogamboga na matunda.
JAMHURI: Je, ni kwa kiasi gani umeweza kufanikiwa katika miradi uliyoanzisha?
NYAISSA: Kwa kweli kwa kiasi kikubwa miradi niliyoanzisha kwa kushirikiana na wenzangu haikufanikiwa kama nilivyotarajia. Miradi yote niliyoanzisha na wenzangu tulianza kwa kuifungulia kampuni. Hivyo, orodha ya kampuni tulizofanikiwa kuanzisha kwa nyakati tofauti na kushindwa kuziendeleza ni pamoja na Tanzania Agribusiness Solutions, Agribusiness Africa Solutions na Sparke International Company Limited.
Kwa sasa namiliki kampuni za Nitume Sokoni Enterprises, inayojihusisha na mradi wa kilimo cha kisasa cha mbogamboga na matunda na Higher Level Tanzania Company, yenye mradi wa kuwaunganisha wanafunzi wa elimu ya juu nchini na kampuni za utoaji wa huduma na bidhaa ili kupata mahitaji yao muhimu kwa punguzo la bei. Pia kampuni hii itajihusisha na uhamasishaji wa wasomi wetu kuacha kutegemea kuajiriwa na badala yake wajikite katika kujiajiri na kuajiri wenzao.
Mbali ya miradi hii ya vikundi, mimi ni mtunzi na mwandishi wa vitabu. Kupitia vitabu vyangu viwili vya Students of Life na Makaburi Yameelemewa Utajiri, nimefanikiwa kupata fedha za kujikimu na kunirahisishia mizunguko ya mjini.
JAMHURI: Ni vikwazo gani umekuwa ukikumbana navyo katika uanzishaji na utekelezaji wa miradi yako?
NYAISSA: Swali zuri sana ndugu mwandishi. Kwa kipindi chote hiki nimekuwa nikikumbana na vikwazo vikuu vitatu, ambavyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara. Kwanza ni ukosefu wa uvumilivu, hasa kwetu sisi vijana. Mara nyingi tumekuwa tukitarajia matokeo ya haraka, na pale uhalisia wa mambo unapotofautiana na matarajio yetu, tumekuwa wepesi wa kukata tamaa.
Pili ni ukosefu wa fikra na mtazamo sahihi juu ya maisha miongoni mwa vijana nilioshirikiana nao kwa nyakati tofauti. Na tatu ni ukosefu wa uaminifu katika biashara. Vikwazo hivi vitatu vimenisababishia kuchelewa kupata timu sahihi ya vijana makini wa kufanya nao kazi. Suala la ukosefu wa mtaji wa fedha halijapata kuwa kikwazo kwangu. Si kwa sababu ninazo hizo fedha bali kwa sababu naamini kukiwa na timu nzuri ya vijana wenye ari na moyo wa dhati wa kujiajiri na kuajiri wenzao, ni rahisi sana kusaidiwa na Serikali, watu binafsi na taasisi mbalimbali za jamii.
JAMHURI: Je, unatumia mbinu gani kukabili vikwazo vya shughuli zako za kujiajiri na kujijenga kiuchumi?
NYAISSA: Zipo mbinu mbili ninazotumia. Kwanza ni sala. Mimi si mtu wa dini sana, lakini mara nyingi vikwazo vinaponizidi nguvu huwa natafuta sehemu “iliyotulia sana” na kuzungumza na Mungu kama marafiki wawili wanaofahamiana kwa muda mrefu.
Hapa ndugu mwandishi, ningependa kuzungumza kitu cha ajabu kidogo; sehemu iliyotulia sana ninayopenda kutembelea huwa ni makaburini! Hii ni kutokana na ukweli kwamba makaburini ndipo sehemu tajiri kuliko zote hapa duniani. Kule yamezikwa mawazo na ndoto bora zenye kuutajirisha ulimwengu, ambazo hazikutimia kwa sababu wafu wale hawakuweza kuitumia vyema fursa ya kuwapo kwao hapa duniani.
Kitabu changu cha Makaburi Yameelemewa Utajiri kimeelezea kwa kirefu suala hili. Nikiwa pale makaburini hujikuta nikipata nguvu mpya ya kukabiliana na vikwazo kwa kuamini kuwa siku si nyingi nami pia nitaungana nao pale ardhini, hivyo ninapaswa kufanya kazi bila kuchoka ili siku moja nistahili pumziko la amani. Pili, mimi ni msomaji mzuri wa vitabu. Kupitia usomaji wa vitabu mbalimbali nimepata uelewa mkubwa juu ya maisha. Chumbani kwangu nimejaza vitabu vya aina nne.
Kwanza ni vitabu vya dini za Kikristo na Kiislamu — Spiritual books, pili ni vitabu vya taaluma mbalimbali — Academic books, tatu ni vitabu vya kujijenga kifikra — Personal development books na nne ni vitabu vya uelewa wa jumla — General knowledge books. Kusoma vitabu ni sehemu ya maisha yangu.
JAMHURI: Ni mtu au watu gani ambao wameonekana kukutia moyo katika jitihada zako za kujiajiri na kujijenga kiuchumi, na wamekusaidiaje?
NYAISSA: Sina orodha ndefu ya watu wa aina hii, hasa kutokana na wengi kuendelea kunishangaa kutokana na uamuzi wangu wa kutotaka kabisa kuajiriwa. Wazazi wangu wamekuwa chachu kubwa ya mimi kuendelea na mapambano, kutokana na kunipa uhuru mkubwa wa kujiamulia mambo yangu mwenyewe bila kuniingilia. Pia dada yangu, Lilian Reuben Nyaissa, amekuwa karibu yangu sana akinitia moyo na kuniombea. Mtu mwingine ni Dk. Reginald Mengi, ambaye siku zote amekuwa na bidii ya kusaidia wananchi kuachana na utegemezi wa kiuchumi.
Kupitia mashindano yake ya kuibua mawazo bora ya biashara na kujijenga kiuchumi ya “tweet na Mengi”, nimefanikiwa kuibuka mshindi mara mbili mfululizo, na pia ndiye aliyegharimia uchapishaji wa kitabu cha Makaburi Yameelemewa Utajiri. Nje ya Tanzania, kuna watu wawili wanaonijenga sana kila siku kupitia hotuba zao kwa njia ya mtandao. Watu hao ni Pastor Myles Munroe kutoka visiwa vya Bahamas na Louis Farrakhan kutoka Jumuiya ya Kiislamu ya The Nation of Islam ya nchini Marekani.
JAMHURI: Hadi sasa kuna jambo lolote au kazi yoyote unayoweza kujivunia kwamba umeifanya kwa manufaa ya jamii kwa jumla?
NYAISSA: Ndiyo. Kitendo cha kutotaka kuajiriwa licha ya ugumu wa maisha ninaokabiliana nao mpaka sasa, ni hatua kubwa ninayojivunia. Hapa ndugu mwandishi ningependa wasomaji wetu waelewe jambo moja; kwamba kuajiriwa si jambo baya na ninaposema sitaki kuajiriwa sina maana ya kwamba wenzangu walioajiriwa ni wajinga au hawako katika njia sahihi, bali ninamaanisha kuwa kwa jinsi hali ilivyo sasa ni kwamba jahazi la waajiri limeelemewa na waajiriwa, na njia sahihi ya kuliokoa lisiendelee kuzama ni kuchagua kuwa sehemu ya jahazi (jawabu) badala ya kuwa sehemu ya abiria (waajiriwa).
Ni aibu kusikia wananchi, hasa vijana wasomi, wakiilalamikia Serikali kuwa vijana kutoka mataifa ya nje, hususan Kenya na Uganda wanamiminika nchini kwa wingi na kuchukua nafasi zetu za ajira! Haya ni malalamiko yanayopaswa kutolewa na wasomi wenye mawazo mgando. Mimi ninaamini wananchi wa Kenya, Uganda na mataifa mengine ndiyo wanaopaswa kulalamika kwamba Watanzania wanatunyang’anya nguvu kazi ya mataifa yetu.
Kama vijana wa Tanzania tukitawaliwa na fikra za kujiajiri na kuajiri wenzetu, basi tutajikuta tukiwaajiri wasomi hao kutoka mataifa ya nje. Pia najivunia vitabu vyangu viwili vilivyoko sokoni sasa ambavyo vinaendelea kubadili fikra na mitazamo ya vijana wenzangu.
JAMHURI: Una mipango gani ya baadaye katika mikakati ya kujiajiri na kuajiri wengine kwa lengo la kujijenga kiuchumi?
NYAISSA: Mipango yangu ya baadaye ni kuanzisha asasi yangu binafsi itakayoitwa Youth Inspire Africa Organization, kwa lengo la kuwahamasisha na kuwasaidia vijana wenzangu wa Kiafrika kujitambua na kujiajiri badala ya kusubiria kuajiriwa. Ndoto yangu ni kuhakikisha tatizo la ajira linakuwa historia barani Afrika kwa sababu hatustahili kucheza ngoma hii ya ukosefu wa ajira.
Labda nielezee kidogo dhana hii. Ni kweli kuna tatizo kubwa sana la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana duniani kote. Mataifa makubwa kiuchumi ya Marekani, Ufaransa, Italia, Uingereza, Hispania na mengineyo yanalia sana kuhusu ukosefu wa ajira. Ndugu mwandishi, mataifa haya ni stahili yao kulia ukosefu wa ajira kwa sababu yameamua yenyewe kujiita “mataifa yaliyoendelea” na kitu chochote kilichoendelea lazima waliokiendeleza wakose kazi ya kufanya. Lakini hali haiko hivyo barani Afrika, hususan nchini Tanzania. Sisi ni “mataifa yanayoendelea” ambayo yana kazi kubwa ya kujijenga kiuchumi, hivyo basi ni upunguani kuicheza bendi hii ya ukosefu wa ajira.
JAMHURI: Una wito gani kwa vijana wasomi wanaosubiri kuajiriwa serikalini?
NYAISSA: Wito pekee nilionao kwa vijana wasomi ni kuwaasa waache kusubiria kuajiriwa, badala yake wajikite katika kuchangamkia fursa na kutengeneza ajira kwa vijana wenzao. Elimu ni kama mwanga umulikao gizani na kuonesha njia, hivyo basi sisi tuliopata bahati ya kufika vyuo vikuu tuna wajibu wa kutangulia mstari wa mbele na kuonesha njia badala ya kuishia kulalamika na kusubiri Serikali ituajiri.
Na wale tulioamua kujiajiri tuache visingizio vya ukosefu wa mitaji fedha kama sababu ya kushindwa kwetu, kwani tukifuatilia historia za watu wengi waliofanikiwa hawakuanza na mitaji hiyo tunayolalamikia kuikosa. Kubwa ni kujiamini, kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kuwa na macho yenye kuziona na kuzitambua fursa na kuwa waaminifu katika mambo yote tunayoyafanya na kuyanena.
JAMHURI: Una wito gani kwa jamii katika suala zima la ujasiriamali na kujiajiri?
NYAISSA: Wito nilionao kwa jamii yangu ya Watanzania; kwanza ni kuwaomba waendeleze amani hii tuliyonayo kwani bila amani na utulivu hatuwezi kuendeleza ujasiriamali. Pili ni kuwataka Watanzania watambue kuwa Taifa letu lina kila sababu ya kuwa Taifa lenye sifa za kipekee duniani. Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa utajiri wa maliasili baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Lakini pia Tanzania ni nchi pekee kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo sehemu kubwa ya eneo lake lenye rutuba halitumiki.
Zaidi ya asilimia 75 ya eneo la Tanzania ni mbuga, maji, mapori ya akiba na hifadhi za Taifa! Eneo la Tanzania ni asilimia 52 ya eneo lote la nchi tano za Afrika Mashariki. Wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu milioni 45 pekee, nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja zina jumla ya watu wanaofikia milioni 90.6, hivyo kuifanya Tanzania kuwa lulu katika shirikisho hilo.
Ukubwa wa eneo la Tanzania ni sawa na eneo la nchi za Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Jamhuri ya Ireland na Uingereza kwa pamoja. Nirudie wito wangu wa kuwataka Watanzania wenzangu tuchangamkie fursa mbalimbali za ujasiriamali na kujiajiri, badala ya kutegemea kuajiriwa au misaada kutoka ulaya.
JAMHURI: Ulizaliwa lini na wapi, ulianza shule lini mpaka kuhitimu chuo kikuu na umesomea taaluma gani?
NYAISSA: Nilizaliwa tarehe 19 Agosti, 1988 wilayani Serengeti mkoani Mara, na kisha kupata elimu yangu katika Shule ya Msingi Kenyamonta na Shule ya Sekondari Ngoreme zote za Wilaya ya Serengeti kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2006. Baadaye nilijiunga na Shule ya Sekondari Azania ya jijini Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha sita mwaka 2006, kisha nikajiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa mafunzo ya elimu ya juu ambapo mwaka 2012 nilihitimu shahada ya awali ya utawala katika biashara.
Huyu ndiye Gerald Nyaissa, msomi anayependa kuchangamkia fursa za kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa serikalini. Ni mfano mzuri unaostahili kuigwa na vijana wengine hapa Tanzania.