Ukitumia dakika 60 kulalamika, umepoteza saa 1
Kulalamika ni mtihani. Unaweza kulalamika kuwa maua aina ya waridi yana miiba au kusifu kuwa miiba ina maua. Ukitumia dakika sitini ukilalamika, umepoteza saa moja. Kama una muda wa kulalamikia jambo, una muda wa kulitatua. Chukua hatua, ukiua muda ukilalamika muda unaishia kukuua. Chukua hatua, yashughulikie mambo unayoyalalamikia. Tafuta suluhisho. “Usilalamike bali chapa kazi zaidi,” alisema Randy Pausch. Kuna watu kumi na wawili ambao walikuwa wanalalamika kwa vile wana matatizo makubwa sana. Walikwenda kuomba ushauri kwa mtu mwenye busara. Aliwaambia sita wakae mkono wake wa kushoto na sita wakae mkono wake wa kulia. Aliwaambia kuwa kila mtu aandike tatizo lake kubwa sana kwenye karatasi, halafu wabadilishane karatasi na kubadilishana matatizo yaliyoandikwa. Baada ya kubadilishana karatasi na kila mmoja kusoma tatizo kubwa sana la mwenzake, wote walisema afadhali kubaki na tatizo la mwanzoni. Kulalamika ni mtihani.
Kuna aliyesema: “Ukitumia siku ya leo kulalamikia jana, hakufanyi kesho iwe nzuri zaidi.” Kulalamika usiwe mpango mkakati katika maisha yako, tengeneza mpango mkakati wa kubadili hali yako. “Kama hupendi jambo, libadili. Kama huwezi kulibadili, badili mtazamo wako. Usilalamike,” alisema Maya Angelou.
Nick Vujicic ambaye hana mikono wala miguu alisema: “Nina chaguo kumkasirikia Mungu kwa kile ambacho sina, au kushukuru kwa kile nilicho nacho.” Ambaye hawezi kudansi hulaumu uwanja kuwa una mawe.
Kuna mtoto aliyewalalamikia wazazi kuwa hawamnunulii viatu. Aliacha kulalamika alipoona mtu ambaye hana miguu. Kuna makundi ya watu yanayolalamika kila mara: wale wasiopata wanachokistahili na wanaopata wanachokistahili. “Baadhi ya watu wanalalamika kila mara; kama wangezaliwa kwenye Bustani ya Eden, wangetafuta mambo mengi ya kulalamikia,” alisema John Lubbock.
Jambo la kujua ni kuwa huwezi kuwa na tamu bila jasho, huwezi kuwa na furaha bila huzuni, huwezi kuwa na maisha bila kifo, huwezi kuwa na maisha bila maumivu na huwezi kuwa na mvua bila matope. Ukiomba mvua uwe tayari kukanyaga matope.
Mwanasaikolojia alipewa kibarua cha kujua mtazamo wa mapacha wa kiume Esau na Yakobo. Aliwaambia wazazi wao wawanunulie zawadi siku ya kuzaliwa kwao. Esau alinunuliwa kompyuta kubwa ya mezani. Alilalamika na kusema: “Mngeninunulia kompyuta ndogo ya kiganjani-palmtop.” Yakobo alipewa gunia la samadi. Alifurahi sana na kusema: “Nafurahi sana maua yetu nitayawekea mbolea. Hii ina maana kuna ng’ombe mahali fulani huenda tutakunywa na maziwa kila mara.” Yakobo alikuwa na mtazamo chanya. Esau alikuwa na mtazamo hasi. Wakati mwingine mtazamo hasi unasababisha kulalamika.
“Ulimi unaolalamika unabainisha moyo usio na shukurani,” alisema William Arthur Ward. Kila mara tazama jambo zuri ambalo uwepo wake unakufanya utoe shukurani. Badala ya kulalamikia msongo wa magari, shukuru kwamba una gari. Badala ya kulalamika kuwa vyombo vya kuosha baada ya mlo ni vingi, shukuru kwamba kuna aina nyingi za vyakula, mapochopocho ni mengi na kuna watu wa kula chakula.
Ukitumia dakika sitini kulalamika umepoteza saa moja. Kama unajipenda, usipoteze muda. Kama unayapenda maisha usipoteze muda. Muda ni kipindi baina ya sekunde, dakika, saa, siku, miezi, miaka, n.k. Muda ni wakati, wasaa, kitambo, muhula, musimu. Muda ni fursa ya kutenda jambo fulani. Tatua tatizo. “Unavyolalamikia matatizo yako zaidi, utakuwa na matatizo zaidi,” alisema Zig Ziglar.