Wiki iliyopita katika sehemu ya 7 hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Je! Kutabasamu walijifunza wapi? Au unadhani kuna jamii fulani ilitoka huko ilikotoka na kuwafundisha ishara hizi? Jamii zote walijifunza ishara hizo kabla ya lile gharika la zimwi na walipokimbia wakatoka na ishara hizo ambazo zinaendelea hadi leo miongoni mwa jamii zote duniani. Akaniangalia tena kisha akaendelea:” Endelea…

 “Masalakulangwa alipolitumbua lile zimwi watu wote humo tumboni walikuwa wanafanana sana kwa mambo mengi. Mambo yalianza kubadilika pale walipotoka tumboni mwake. Watu wa kwanza kwanza kutoka walielekea Mashariki kutokana na kukimbia kwa muda mrefu, zile nywele zao zilianza kunyumbuka kutokana na mwendo kasi wa jamaa hao. Vilevile hata rangi ya ngozi zao ikaanza kuchubuka,” akaniangalia ili aone kama ninamfuatilia masimulizi yake. Kisha akendelea:

 “Kundi la pili walielekea Kaskazini, wao pia kutokana na kukimbia kwao kwa muda mrefu nao pia walichubuka na kuwa weupe. Ndiyo asili ya watu wa Ulaya ya sasa. Kutokana na mwendo kasi mkali, nywele zao zilibadilika hadi kuwa nyeupe na singa kutokana na upepo. Walioelekea Magharibi pia walibadilika, lakini wao hawakuathirika sana kama wale walioelekea Mashariki ambao baadhi yao hata macho yaliathirika. Si unawajua watu hao?

“Kundi la mwisho walitoka tumboni wamechoka sana na wakaelekea Kusini ambako wao walibakiza ile rangi yao ya asili kwa vile hawakukimbia sana. Hata hivyo, baadhi yao ambao walijifanya kukimbia kwa kasi walianza kuchubuka, lakini bahati nzuri nywele zao hazikunyumbuka na kuwa za singa. Tunao hadi leo. Haya yalitokea mamilioni ya miaka iliyopita.

“Na kwa akili zako ninajua kabisa huelewi kwa sababu umekunjwa ukakunjika! Na kwa taarifa yako hata rafiki zangu Wasukuma wao ndio walikuwa wa mwisho kutoka tumboni mwa lile dude. Na walikuwa wamengojea kwa muda mrefu zamu yao ifike. Ilipofika walitoka wakiwa wamechoka na wakaamua kukaa hapa hapa itakavyokuwa na iwe. Hawa ndio kizazi kipya. Kizazi cha sasa. Kwa hiyo asili ya Wasukuma ni hili dude.

“Bwana, bila shaka sasa unaona asili ya watu wa sasa. Zamani waliishi wote bila ubaguzi. Lakini baada ya ukombozi aliofanya Masalakulangwa wametawanyika duniani kote wakihofia wasije wakamezwa tena. Je, wewe unapenda hilo dude lije likumeze au unapenda yale maisha ya kunyanyaswa na jirani yako?

“Wewe unahangaika kutafuta chakula. Lakini yeye na mke wake wanagombana eti mume hajaleta maini ya chakula cha mbwa! Hakuna haki. Dunia ya Masalakulangwa ni ya watu wenye usawa. Wote wahangaike, wote watafute. Hakuna wanyonyaji.” Alimalizia yule bibi akaniangalia kwa makini. “HAPA KAZI TU”.

Jamani bibi huyu alinichanganya kama karanga nisijue uhalisia wa maisha na nini hasa huyu bibi alikuwa anakusudia kuniambia. Je, ni kweli kuwa asili ya kabila la Wasukuma ni hili dubwasha lililouawa na Masalakulangwa? Kutawanyika kwa watu katika dunia hii ni kutoka pale kwenye mhimili wa lile janga ni maneno yasiyoeleweka na pengine kusadikika?

Lakini yule bibi alinihadithia kwa kujiamini sana na wakati mwingine ninashawishika nikubaliane na nadharia hii ya uwepo wa watu na wanyama wao hapa duniani. Mtawanyiko ambao upo hadi leo wakiwa wametawanyika na kutoaminiana na kujiona eti tabaka hili ni bora zaidi.

Baadaye yule bibi alinifungia hirizi moja kichwani na nyingine miguuni na zingine mbili ubavuni. Hao ndio walikuwa mapolisi wangu wa kunilinda, yule bibi alinielezea utafika nyumbani kwenu ila itakuwa baada ya muda wa miaka kama mitatu. “Ni lazima usafishwe, utokane na uchafu wa huku, maana hii ni kama dunia nyingine”. Yule bibi akamalizia.

Nilitaka kujua maana ya hiyo sentensi akajibu: “Utapitia vikwazo fulani lakini kutokana na hirizi nilizokupa, Mzimu wa Masalakulangwa utakusimamia. Utavuka tu babu ukawaone ndugu zako na jamaa zako. Jipe moyo.”

Rafiki yangu Bulongo Gwike, mimi sikumwelewa vizuri bibi huyu. Nikamkazia macho na hapo ndipo nikagundua kuwa umri wake ulikuwa umekubuhu. Alikuwa kikongwe na kwa kweli hata sura yake ilikuwa imebadilika na kuwa ya mnyama. Ila kwa hakika alikuwa na nguvu ajabu. Sasa sina hakika kama huyu alikuwa ni mtu kama sisi au la!

Alinisogelea akaniangalia kwa huruma ya mzazi, akanikumbatia akawa ananisemea maneno kwa lugha ambayo mimi sikuwa ninaielewa. Labda alikuwa ananibariki katika safari yangu nisafiri salama. Alibakia amenikumbatia namna hii kwa muda mrefu na baadaye akatoweka.

Ninasema alitoweka kwa vile ni kweli kabisa kuwa nilipokuja kuzinduka hakuwepo mtu tena sehemu hiyo. Nilikuwa nimebaki peke yangu.

Ni kweli huku nyumbani mlikuwa mmefuta kabisa wazo la kuniona tena labda huko mbinguni ambako kwa kawaida ni lazima kila binadamu afike, ila baada ya kufuliwa kama chuma mpaka anakuwa safi, ndipo unakwenda kuonana na Bwana Mungu wako. Hakuna mtu atakayepotea, kwani sisi sote ni lazima twende kwa Mola tunayefanana naye.

Ila tu utachelewa kutokana na matendo yako mabaya. Niliendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani. Baada ya kusafiri kwa siku nyingi, hatimaye nilifika kwenye nchi ambayo ilifanana sana na ya huku kwetu; isipokuwa nchi hiyo ilikuwa na vioja vyake.

Kwa mfano, siku moja nilihudhuria mahakamani, na kwa vile yale mazindiko ya huyu bibi wa mwisho yaliendelea kunilinda, watu wote pale mahakamani eti walikuwa hawanioni. Mahakamani kulikuwa na kesi ambayo ilinichanganya sana pengine ikanisaidia kuzinduka na kuanza kujitambua.

Kesi hii ilikuwa kabambe na kali kweli kweli. Ilikuwa hivi:- Baada ya hakimu kukaa kwenye kiti chake cha enzi, mshtakiwa Mama Judith White, ambaye ni Mzungu wa taifa la Uingereza aliletwa kizimbani akisindikizwa na askari wa kike wawili. Shauri lake likawa tayari kusikilizwa na hakimu huyo kama ifuatavyo:-

Shahidi wa kwanza alisimama ili atoe ushahidi wake dhidi ya Bibi Judith. Alidai kuwa, siku moja alipokuwa akiwinda na mbwa wake Jack na Tom, walimkurupusha sungura. Kutokana na uhodari wa mbwa wale, waliendelea kumsogelea yule sungura. Kuona hivyo, yule sungura aliwachenga wale mbwa na kuanza kukimbilia upande wa yule shahidi, kwa wakati huo huo mbwa walikuwa tayari kumkamata na kumraruararua yule windo lao wakati wowote.

Sungura kuona kuwa jitihada zake zinakwama na angeweza kuuawa na wale mbwa wakati wowote, alijitosa kwenye kichaka kilichokuwa karibu kabisa na shahidi huyu. Kuona hivyo shahidi alikimbia kwenye kichaka hicho ili amkamate yule sungura kabla Jack na Tom hawajamrarua.

Kwa mshangao mkubwa, shahidi alipomkamata yule sungura, akageuka sura na kuwa Bibi Jidith, ambapo kwa wakati huo wote alikuwa anatweta kwa nguvu kwa sababu pumzi zilimbana kwa sababu ya kukimbia… Shahidi alijaribu kumuuliza mama huyu maana ya jambo hili, lakini bibi huyu hakujibu chochote. Shahidi aliogopa sana tangu hapo. Akawachukua mbwa wake na kuanza kurudi nyumbani akiwa taabani kwa mawazo.

Bwana Bulongo Gwike, haya sikuyaona ila kwa vile yalitajwa mahakamani, nina uhakika kuwa ni ya ukweli! Si rahisi kwa mtu kuzungumza uongo mbele ya Pilato – Hakimu.

Shahidi wa pili alikuwa Bibi Judith mwenyewe. Aliieleza mahakama jinsi siku moja walivyokuja jamaa watatu. Mmoja alikuwa Mzungu, mwingine Mwarabu na wa mwisho alikuwa mtu mweusi – Mwafrika. Watu hawa alidai mama huyu kuwa eti walimuomba ajiunge katika shughuli zao za kichawi. Lakini mama huyu eti alikataa kata kata. Hata hivyo watu hawa waliendelea kuja na kumbembeleza kwa siku kadhaa. Maudhi ya watu hawa yalipozidi aliamua kukubali. Akajiunga!

Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya kujiunga? Usikose sehemu ya tisa yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu Na. 0755629650.